Maoni ya katuni.
Kinachofurahisha ni kwamba Watanzania wengi hawaongelei kuhusu kuvunja Muungano na kama wapo basi wanayasema hayo kichini chini, isipokuwa kinacholalamikiwa na wengi ni kero katika Muungano huo unaotumiza miaka 46 leo. Ni kero, kero kila siku kero.
Kwamba muungano wetu huu wa damu, licha ya kuwa wa aina yake duniani, unatoa fursa kibao zenye manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili ni ukweli usiokuwa na pingamizi. Pengine ndio maana tunadhani kwamba mwenye mawazo ya kutaka uvunjike ana matatizo kichwani ama ana lake jambo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wasomi na wanasiasa wa hapa nchini na wenzao kutoka nchini jirani zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki, walikutana jijini Dar es Salaam, nao wakaishauri Tanzania kutatua kwanza kero zilizoko katika Muungano kabla ya kuingia katika Shirikisho la Afrika Mashariki (EAC) miaka miwili ijayo.
Baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa yakitajwa kuwa na kero ni pamoja na uendeshaji wa nchi, masuala ya kodi na biashara pamoja na rasilimali kama vile za mafuta na gesi. Yamekuwepo pia malalamiko kuhusu ukiukwaji ama uongezwaji wa mambo ya Muungano bila wananchi kushirikishwa, na pia Wazanzibari wamekuwa wakilalamika kwamba hawanufaiki sana na Muungano kama wenzao wa Bara. Suala la Rais wa Zanzibari kuwa waziri katika baraza la mawaziri, nalo limekuwa likitajwa kama kitu kinachowachefua Wazanzibari wakiona kama linampunguzia hadhi raisa huyo. Haya yote ni mambo yanayoweza kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.
Licha ya kuwepo kwa wizara maalum inayoshughulikia masuala ya Muungano iliyo chini ya ofisi ya Makamu wa Rais, kinachoonekana ni kwamba kero hizi zimeendelea kuwepo. Ni vigumu pia mtu leo hii kusimama akaona waziwazi namna wizara hii ilivyotatua kero za Muungano kwa muda wa takriban miaka mitano toka Rais Jakaya Kikwete aiunde.
Lakini, kwa mujibu wa wasomi na wanasiasa waliokutana mwishoni mwa wiki, msingi wa kero hizi uko kwenye sheria za nchi yetu, hususan sheria mama, yaani Katiba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Utafiti wa masuala ya siasa kutoka Uganda, Agustine Ruzindana, alitoa taarifa ya utafiti wao ikionyesha kwamba matatizo ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar yanatokana na baadhi ya vipengele vya Katiba kushindwa kueleweka kwa pande hizi mbili za muungano.
Alisema ili kumaliza dosari hizo ni lazima katiba ya nchi ifanyiwe marekebisho ili pande zote za Muungano ziweze kuamini kwamba zinanufaika nao.
Alisema licha ya utafiti kuonyesha kwamba Wazanzibari wanaupenda Muungano, lakini wengi wanaona kama hauwanufaishi sana. Hata hivyo, alisema wenzao wa Bara walio wengi hawaamini kama Wazanzibari wana kero ambazo pengine bila Muungano wasingekuwa nazo.
Katika mkutano huo wa wasomi na wanasiasa, Dk. Sengondo Mvungi alifafanua kwamba wakati wa kuunda Muungano, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume, walikubaliana vipengele vinane, lakini kwa sasa vimeongezwa na kufikia 11.
Lakini akasema, kwa bahati mbaya sana, wananchi wa pande mbili hizi hawajui vipengele vya zamani vinasemaje na vilivyoongezwa vinazungumzia nini.
Kitu kingine ambacho kimeanza kujitokeza ni Wazanzibari, tena kupitia baraza la wawakilishi kuhoji mambo mengi ya Muungano na mwisho wa siku kupitisha maamuzi ambayo taratibu yanaonekana kama yatarudia ama yanapunguza nguvu za Muungano wetu.
Tunadhani kwamba lazima tuwe na dhamira ya kweli katika kutatua kero za Muungano kwa kukaa pamoja na kuzungumzia ikiwa ni pamoja na kupitia upya katiba na sheria za nchi yetu zinazoonekana kuwakwaza wananchi wa pande hizi mbili.
Ingawa hili linawakera baadhi ya watu, lakini si vibaya tena ukaanzishwa mjadala wa nchi nzima kuhusu aina ya Muungano ambayo wananchi wanaitaka likiwemo suala la serikali tatu.
Kitu kingine muhimu ni kutoa elimu kwa wananchi wa pande hizi mbili kuhusu mambo muhimu ya Muungano, yaani wayajue yale yaliyokuwepo na yaliyoongezwa na umuhimu wake.
Tunaamini viongozi wetu wakiamua kuweka nguvu katika eneo hilo, kero za Muungano zinaweza kuisha kabisa kabla hatujaingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
CHANZO: NIPASHE