ZIARA ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yussuf Makamba, hapa Zanzibar, imewaweka roho juu baadhi ya vigogo wa SMZ, wanaohofia kupoteza nyadhifa zao.
Hofu hiyo inatokana na taarifa kuwa, ajenda kuu iliyojadiliwa wakati Makamba alipokutana na viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), wakiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad, ni kuundwa kwa serikali ya mseto.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya mawaziri kuanza kudadisi ajenda kupitia baadhi ya viongozi wanaoshiriki mazungumzo hayo na baadhi ya waandishi wa habari wanaofuatilia habari zake.
Nyinyi kama waandishi, kwa nini hamuwaulizi kwa nini wanayafanya mazungumzo hayo kuwa siri wakati ni mambo yanayohusu maslahi ya taifa na yanagusa wananchi? alihoji waziri mmoja mwandamizi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Hofu kubwa zaidi ya viongozi hao, inatokana na ukweli kwamba, iwapo itaundwa serikali ya mseto, upo uwezekano mkubwa wa baadhi yao kupoteza nyadhifa zao ili kutoa nafasi kwa wale wa CUF kuingia serikalini.
Kutokana na unyeti na ugumu wa siasa za Zanzibar, Makamba alikuwa mwangalifu na hata mara moja hakulizungumzia suala la mpasuko katika mikutano yake yote ya hadhara katika mikoa mitatu ya Unguja aliyotembelea.
Hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na serikali au chama visiwani hapa, lakini Rais Abeid Amani Karume, amekuwa akisisitiza kila mara kuwa, hakuna mpasuko wa kisiasa visiwani hapa.
Taarifa zilizoenea Zanzibar kwamba Maalim Seif na naibu wake, Juma Duni Haji huenda wakateuliwa kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, zimezidisha wingu la hofu.
Wengi wanaamini kuwa iwapo hilo litatokea, itakuwa ni mwanzo wa safari ya kuingia katika Baraza la Mawaziri la Rais Karume.
Hali hiyo imezidi kuwa mbaya zaidi, kufuatia kiti cha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, Amina Salum Ali, kubakia wazi tangu Oktoba mwaka jana, baada ya kujiuzulu kufuatia kuteuliwa kuwa Kamishana wa Umoja wa Afrika huko Umoja wa Mataifa.
Wadadisi wa mambo wanahisi kuwa, baadhi ya viongozi wa SMZ na CCM Zanzibar, walishanusa mwelekeo wa ziara ya Makamba, na ndio maana hata mapokezi yake hayakuwa ya kishindo kama inavyokuwa kwa viongozi wengine.
Ziara hiyo ya Makamba na kuanza kwa mazungumzo hayo, kumewafanya wanasiasa machachari kisiwani hapa kuwa watulivu, na kuacha kutoa kauli zao kwamba, hakuna mseto wa muhogo.
Baadhi ya viongozi waliamua kuzua safari za ghafla, kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kutokana na kukwepa kujihusisha na ziara hiyo ambayo imeacha gumzo kubwa kisiwani hapa.
Wapo walioogopa kuhudhuria katika mikutano ya Makamba kwa hofu ya kuulizwa jinsi wanavyozitumia mali za chama. Viongozi wengi wa CCM visiwani hapa, wamehodhi magari ya chama, na kwa kiasi kikubwa wanayatumia kama yao binafsi.
Kitendo cha baadhi ya maofisa wa kitengo cha uenezi kuhudhuria mikutano ya Makamba kwa kutumia daladala, pia kiliwapa wasiwasi mkubwa watu hao, wanaohodhi magari ya chama.
Viongozi wachache tu walihudhuria mkutano wa mwisho wa Makamba kuhitimisha ziara yake, uliofanyika katika viwanja vya Mpendae. Baadhi ya viongozi wanahoji kwa nini mkutano unaomhusisha kiongozi mkubwa kama Makamba ukapangwa kufanyika maeneo ya vichochoroni.
Baadhi ya wana CCM walisema, wanashangazwa na mahudhurio madogo ya mawaziri, makatibu wakuu na wakurugenzi, kwa vile si kawaida Zanzibar mkutano wa hadhara wa CCM ufanyike bila ya viongozi hao kuonekana wakiwa na mashati yao ya kijani.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria mkutano wake wa mwisho Zanzibar, ni Waziri Kiongozi mstaafu, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Brigedia Jeneral mstaafu, Adam Mwakanjuki na Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Yussuf Khamis.
Wengine ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Ramadhan Ferouz, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Mgharibi, Abdallah Mwinyi na watendaji wa CCM mkoa.