Honourable Omar Sheha, Mussa [ CCM ]
Chumbuni Constituency
Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi hii ya kuchangia kwa maandishi chini ya Kanuni ya 49(7) na kwamba nakupongeza wewe kwa kuteuliwa kwako kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa mwaka 2005 hadi 2010.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru wananchi wa Jimbo langu la Chumbuni kwa kunichagua kuwa Mbunge wao kwa kipindi hiki cha 2005 hadi 2010; na kwa jumla nawashukuru vile vile kukipa ushindi Chama cha Mapinduzi kule Jimboni kwangu Chumbuni kwa nafasi ya Rais na ya Mbunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 uliofanyika tarehe 12 Desemba, 2005.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, sasa naomba kuchangia hotuba ya Rais Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ukurasa wa 16 hadi 17 juu azma yake ya kuimarisha Muungano wetu pamoja na kuondoa kero za Muungano zilizobakia na kuiwezesha Zanzibar kupata maendeleo zaidi ya kiuchumi katika kipindi chake cha Awamu ya Nne ya Serikali ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, katika kuteleleza azma hiyo ya kuondoa kero za Muungano na kuisadia Zanzibar ipasavyo, basi mambo yafuatayo yazingatiwe:_
(a) Uhusiano wa kifedha uliokuwepo baina ya iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kabla ya Muungano wa mwaka 1964 na baada ya Muungano wetu Aprili, 1964.
(b) Utaratibu wa sasa ulioleta kero, hasa kwenye eneo la kodi za Muungano (Fiscal Policy) ambapo nahisi ndio kero kubwa baina ya pande mbili.
(c) Kutekeleza na kufanya jitihada za kuondoa mambo ambayo ni vikwazo vya Muungano wetu kama ilivyokwishaamuliwa kwenye taarifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, taarifa ya Kamati ya Shellukindo ya tarehe 27 Septemba, 1994, ambayo ni taarifa ya Serikali ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikifuatilia nini kilitokea baada ya Muungano wetu wa hiari, hasa mahusiano ya kifedha yalivyokuwa baina ya pande zetu mbili baada ya Muungano wa Aprili, 1964. Serikali zote mbili, ile ya Mapinduzi Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano, walikuwa ni Wanachama wa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (East African Currency Board).
Mheshimiwa Spika, baada ya Uingereza (waliokuwa watawala wa eneo la Afrika Mashariki) kuzipa uhuru nchi zote nne za Afrika Mashariki - Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar mnamo kipindi cha miaka 1961 hadi 1963, nchi zetu mbili (ambapo sasa ni moja inayoitwa Tanzania), zilimiliki mtaji kwenye Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, ambao ulirejeshwa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, mnamo mwaka 1992 hadi 1994 pande mbili za Muungano zilikubaliana kuwa IMF, Shirika la Fedha la Dunia, wapewe kazi ya kuchunguza uhusiano huo wa kifedha na katika ripoti yao ya Machi 1994, ilishauriwa kuwa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 1965 ibadilishwe ili Zanzibar nayo kupewa haki ya hisa zake kwa mujibu wa mtaji wake uliorejeshwa Tanzania kutoka Bodi hiyo ya Sarafu ya Afrika Mashariki mwaka 1966 hadi 1972.
Mheshimiwa Spika, baada ya kazi hiyo na Ushauri wa IMF ilikubaliwa na pande zetu mbili kuwa tusitazame nyuma kwa kuepuka kugombana, bali tupige mstari na kukubaliana yafuatayo kuanzia mwaka 1994 (Miaka 30 baada ya Muungano wetu):-
(a) Tuwe na Benki Kuu moja, Sarafu moja;
(b) Tuwe na Mamlaka Moja ya Fedha, Sera moja ya fedha; na
(c) Tuwe na usimamizi mmoja wa Mabenki na vyombo au Taasisi za Fedha.
Mheshimiwa Spika, hayo yalitekelezwa na pande zote mbili na kuanzia Julai, 1995 sheria mpya ya BOT ilianza kutumika pande zote mbili za Tanzania na kuiwezesha Zanzibar kupata gawio la 4.4% pamoja na kufungua na kuweka hesabu zake ndani ya Benki hiyo hadi sasa.
Mheshimiwa Spika, mgao huo wa faida ya BOT kwa Zanzibar, mwaka 1995 ulifanywa kwa formula ya muda tu na ripoti yenyewe ya IMF ya Machi/Aprili 1994 ilieleza hayo. Sasa ni miaka kumi na nne imepita bado gawio la Zanzibar limebaki pale pale. Hili ni kero kubwa la Muungano.
Mheshimiwa Spika, ili kuondoa kero hiyo kubwa kuliko zote, Tume ya Pamoja ya Fedha (Joint Finance Commission) iliyokwishaundwa chini ya kifungu cha 134 cha Katiba ya Tanzania, sasa imalize kazi yake ya kupendekeza kwa Serikali zote mbili, ili kuona mgao wa hisa wa Zanzibar unaboreshwa na kufikia angalau ya 11% au zaidi, kama mtaji wa Zanzibar ulivyokuwa ndani ya Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, ambao umetajwa kwenye Ripoti ya IMF (Appendix II) ukurasa wa 16.
Mheshimiwa Spika, yakifanyika hayo kwenye eneo la uhusiano wa kifedha, basi Tanzania itakuwa imeondoa kabisa kero hiyo kubwa ya Muungano.
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la Kodi za Muungano (Fiscal Sector) kero kubwa ni utaratibu wa sasa ambao uliwekwa tokea mwaka 1977. Utaratibu wa sasa ambao unatekelezwa na SMT na ambao unaumiza upande mmoja na utaratibu huo ni wa kubakisha kodi za bidhaa zinazozalishwa Tanzania Bara na ambazo hutumika kwa wananchi wa Zanzibar (Consuming Area) kodi hizo kubakia Bara. Bidhaa kama Sigara, Bia, Saruji, Soda na kadhalika, kodi za Viwandani VAT na Excise Duty ambazo ni kodi za forodha, ni vyema sheria zote husika zibadilishwe katika Awamu hii ya Nne, ili kero hii iondoke, kwani Zanzibar hainufaiki pamoja na kodi ya mapato (PAYE).
Mheshimiwa Spika, endapo Serikali ya Muungano itafanya mabadiliko hayo kwenye sekta ya fedha (Monetary) na sekta ya Kodi (Fiscal) basi Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne pamoja na Bunge lake hili, itawezesha Zanzibar kufaidika milele na kudumisha Muungano wetu kwa kuondoa kero hizi. Zanzibar nayo, itaweza kulipa mchango wake wa Muungano kutokana na Mapato yatokanayo na Monetary/Fiscal Sector.
Mheshimiwa Spika, yote hayo ili yatendeke, Tume ya Fedha ya Pamoja, ambayo sasa imeanza kazi zake, iharakishe hayo na Wizara za Fedha na Muungano zishirikiane kusimamia hayo na mapendekezo ya awali yaanze kutekelezwa angalau kuanzia Julai, 2006
Mheshimiwa Spika, baada ya hayo, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa tarehe 30 Desemba, 2005.