Maalim azuiwa Zanzibar
na Mohammed Abduralhman
ZIARA ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, kutembelea wagonjwa katika hospitali za wilayani Unguja na Pemba imeingia dosari, baada ya kuzuiliwa kutembelea Hospitali ya Mkoa Kaskazini Unguja iliyopo Kivunge.
Hamad juzi alitembelea wagonjwa waliopo majumbani, lakini Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Zanzibar imemzuia kutembelea hospitali hiyo kwa kile kilichoelezwa sababu za kitaalamu.
Ujumbe wa Maalim Seif ulikuwa umeambatana na Mwenyekiti wa CUF, Wilaya ya Kaskazini A Unguja, Bakari Makame, Katibu wa jimbo hilo, Khamis Abass na Mbunge wa Viti Maalumu wa CUF, Mwajuma pamoja na Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu na Mawasiliano ya Umma, Salum Bimani.
Kiongozi huyo amezuiwa kutembelea katika hospitali hiyo na Daktari Dhamana wa Hospitali ya Kivunge, Mtumwa Ibrahim, ambaye alisema kutokana na sababu za kitaalamu, ujumbe huo hauruhusiwi kutembelea hospitali hiyo. Hata hivyo hakufafanua zaidi.
Alisema ni kweli uongozi wa hospitali ulipokea ombi la ujumbe huo kutaka kuruhusiwa hospitalini kuwajulia hali wagonjwa wanaopatiwa matibabu, lakini kutokana na sababu hizo haikuwezekana.
Kutokana na sababu za kitaalamu haitawezekana kutembelea wagonjwa katika Hospitali ya Kivunge, alisema daktari huyo Dhamana, katika barua yake ya Oktoba 5, mwaka huu.
Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Bimani, alisema CUF imesikitishwa na uamuzi huo, kwa vile umewanyima haki wagonjwa kusalimiwa na kupatiwa msaada.
Bimani, alisema ni jambo la kushangaza wakati Maalim Seif anazuiwa kuwatembelea wagonjwa, wananchi mbalimbali wanaruhusiwa kuwatembelea katika hospitali hiyo hiyo.
Alieleza kuwa tangu ziara ya Maalim Seif kuanza kuwatembelea wagonjwa hospitalini na majumbani, kumekuwa kukijitokeza matatizo mbalimbali, ikiwamo huko Micheweni ambako wafanyakazi wa hospiatli walitakiwa kujieleza ni kwanini walimruhusu katibu mkuu huyo wa CUF kutembelea hospitalini hapo.
Alisema CUF imeamua suala hilo kulikabidhi kwa kiongozi wa upinzani katika Baraza la Wawakilishi, ili kuhoiji kwanini serikali inafanya hivyo.
Tangu kuanza kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, Maalim Seif amekuwa katika ziara ya kutembelea wagonjwa majumbani, hospitalini na ziara hiyo aliianzia katika mikoa miwili ya Pemba na sasa inaendelea kisiwani Unguja.
Akiwa kisiwani Pemba, katibu mkuu huyo alitembelea hospitali za Mkoani, Abdalla Mzee, Wete na Micheweni, na kutoa misaada kwa ajili ya wagonjwa, ikiwemo mashuka ya kutandikia vitanda na vyandarua.
Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, aliwataka viongozi wa CCM Zanzibar kuwa na utamaduni wa kutembelea wagonjwa hospitali ili kuwa karibu na wananchi.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Mpendae, Makamba alisema viongozi wanapotembelea wagonjwa na kubeba zawadi kama vile matunda, kunajenga faraja kwa wahusika.
source:
http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/10/8/habari3.php