na Edward Ibabila (Butiama) na Saada Said (Zanzibar)
MKUTANO wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliomalizika jana kijijini Butiama, umeonyesha dalili za wazi za kuhofia kuundwa kwa serikali ya mseto kabla ya mwaka 2010.
Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka ndani ya kikao hicho, zinaonyesha kwamba pamoja na wajumbe wa CCM na wa Chama cha Wananchi (CUF) kwenye kamati ya muafaka, kukubali kuundwa kwa serikali ya mseto Zanzibar kabla ya uchaguzi ujao wa mwaka 2010, mpango huo umepingwa na wanachama wengi wa CCM kutoka visiwani Zanzibar.
Kikao hicho kiliendelea mpaka usiku huku ajenda ya suala la muafaka likizua mvutano mkubwa miongoni mwa wajumbe wa kikao hicho hasa wale wa kutoka Zanzibar.
Kabla ya kujadiliwa suala hilo, kikao hicho kilijadili ajenda ya hali ya kisiasa, usalama ndani ya chama na serikali na suala la hali ya uchumi kabla ya wajumbe kupumzika.
Baada ya hapo, wajumbe waliingia kujadili ajenda ya muafaka Zanzibar na mmoja wa wajumbe alilidokeza Tanzania Daima kuwa mjadala huo uliwagawa huku wajumbe kutoka Zanzibar wakipinga kuwepo kwa serikali ya mseto visiwani humo.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Amani Abeid Karume ndiye anayetajwa kuwaongoza baadhi ya wanachama wa chama hicho kupinga kuwapo kwa serikali ya mseto visiwani Zanzibar.
Habari hizo zinaeleza Rais Karume hayuko tayari kwa sasa na hususan kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, kuunda serikali ya umoja wa kitaifa itakayokuwa na Waziri Kiongozi atakayetokana na CUF.
CUF kimeshajadili mapendekezo yaliyotokana na mazungumzo ya muafaka na wamekubaliana na ajenda zote, ikiwemo ya kuanzishwa kwa serikali ya mseto kabla ya mwaka 2010.
Ajenda nyingine iliyodaiwa kuzua mjadala mkubwa ni ya baadhi ya wana CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi kufilisiwa na kunyanganywa mali zao.
Akifungua kikao hicho juzi, Rais Jakaya Kikwete, aliwatoa hofu baadhi ya watu, hususani wanaotuhumiwa kwa ufisadi kuwa, chama hicho hakina mpango wa kutaifisha mali zao.
Rais Kikwete alisema ingawa kikao hicho kitajadili masuala mazito yanayohusu chama na serikali, lakini hakitajadili mageuzi ya kisera au kiitikadi.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete ilionyesha dhahiri kuwagawa wajumbe wa mkutano huo, ambao baadhi yao walitaka wanachama waliotuhumiwa kwa ufisadi watoswe.
Kutokana na kauli hiyo, habari kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa kikao hicho zinaeleza kuwa, wengi wamekatishwa tamaa na kuelezea kauli hiyo kama ni ya kuwataka wanaowatuhumu viongozi kwa rushwa kuacha kufanya hivyo.
Wakielezea jinsi kauli hiyo ya Kikwete ilivyopokelewa ndani ya kikao hicho, walisema wana CCM ambao wanatuhumiwa katika kashfa ya Richmond na EPA, ambao kwa muda wote kabla ya kutolewa kwa kauli hiyo, walikuwa kimya huku wakionekana wazi kuwa na wasiwasi, walichangamka na kuwa miongoni mwa watu walioshangilia.
Aidha, habari zilieleza kuwa baadhi ya wajumbe walikuwa na matarajio makubwa kuwa kashfa ya Richmond na EPA zingekuwa miongoni mwa ajenda muhimu katika vikao hivyo.
Walisema kama ajenda hizo zingejadiliwa, kwa vyovyote vile yangetokea maamuzi mazito dhidi ya wanachama wa chama hicho, ambao kwa namna moja au nyingine wanahusishwa katika tuhuma hizo.
Habari zinaeleza kabla ya kuanza kwa kikao hicho, baadhi ya wajumbe walilumbana vikali huku wengi wakitaka waliohusika katika kashfa hizo wapewe adhabu kali, ikiwa ni pamoja na kufilisiwa mali zao na kufutiwa uanachama.
Katika malumbano hayo, wajumbe wachache walionekana kutounga mkono hoja hiyo kwa madai kuwa itazidisha makundi ndani ya chama, jambo ambalo walidai litaathiri mshikamano wa chama hicho.
Wakati huo huo, Chama cha Wananchi (CUF) kimesema hakitaki kuingizwa katika serikali kwa ajili ya kutaka umaarufu na madaraka, lakini kinataka kuundwe serikali yenye sura ya umoja wa kitaifa kwa lengo la kuwakutanisha Wazanzibari wote.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, alipozungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Garagara, Jimbo la Mtoni.
Alisema kutokana na uzoefu alioupata, chama chake kimeona ni busara kuingizwa katika serikali kwa sababu kitakuwa karibu zaidi na mwenendo wa kazi za serikali kwa kuwa mwafaka uliopita wakati wa Dk. Salmin Amour haukutekelezwa.
Alisema muafaka mwingine ambao ulitiwa saini na kusimamiwa na Rais Amani Abeid Karume pia ulishindwa kutekelezwa, hivyo mazoea yanaonyesha kutokuwepo uaminifu, lakini CUF ikiwemo ndani ya serikali, itafanya kazi pamoja na CCM, hivyo mambo yanayokwama yataweza kukwamuliwa. Wenye dhana kuwa sisi tunataka madaraka No, hatutaki madaraka, tunataka kufanya kazi karibu na wenzetu, ili kuijenga nchi yetu, wale wenye kufikiri tunaingia kwenye serikali kwa mlango wa nyuma, hawatujui lengo letu, sisi lengo letu jamani ni kuishi kwa amani katika nchi hii, hatutaki madaraka, tunataka kuondosha chuki na uhasama wa muda mrefu, alisema Maalim Seif.
Alisema Zanzibar kumekuwepo na chuki na uhasama kwa miaka kadhaa hivi sasa, hivyo kuwepo kwa serikali ya pamoja ambayo itawawakilisha wananchi wote itamaliza hali hiyo.
Maalim Seif alisema nchi haiwezi kwenda na kupata rehema na baraka iwapo kuna watu wenye roho mbaya na chuki dhidi ya wenzao, hivyo ni vema kukaa pamoja na maslahi ya taifa na vizazi vijazo na sio busara kuendeleza kuzozana mara kwa mara jambo linalochangia kukosekana amani na baraka.
Katibu Mkuu huyo wa CUF alisema hakuna baraka inayoweza kuingia katika nchi kama kuna mivutano na chuki miongoni mwa wananchi na viongozi.
Mimi ni muumini sana, naamini kabisa na nina hakika tukikaa pamoja nchi yetu itapata baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwani hivi sasa hatupati baraka kutokana na mivutano na chuki zilizopo, tukaeni kuijenga nchi yetu jamani, wenzangu CCM nchi hii
nchi hiii
haya, alisema.
Alisema iwapo Rais Salmin na Rais Karume wangeuchukua ushauri wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Zanzibar leo hii kusingekuwa na mgogoro kama huu kwa kuwa mwaka 1995 alishauri kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, lakini alipuuzwa.
Katika hatua nyingine, Maalim Seif alisema endapo CCM hawatatoa jibu la kuwaridhisha wananchi, chama chake na ulimwengu utafahamu nani mwenye dhamira mbaya kwa Tanzania, kwani CUF imeingia katika mazungumzo kwa dhamira njema na kuzingatia maslahi ya taifa lake.
Aidha, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani Zanzibar wameanza kupiga debe kushirikishwa katika serikali ya mseto kabla hata ajenda hiyo kufikiwa utekelezaji wake.
Hali hiyo imeanza kujitokeza siku chache baada ya Maalim Seif kutangaza kamati ya pamoja ya mazungumzo imekubaliana kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, kama hatua ya kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
Katibu Mkuu wa TADEA, Juma Ali Khatib alisema hatua ya mazungumzo iliyofikiwa katika muafaka huo ni muafaka katika kujenga umoja wa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Hamad Mussa Yussuf, alisema suala la serikali ya mseto ni jambo linalohusu katiba, hivyo ni vema vyama vyote vikashirikishwa kabla ya hatua ya utekelezaji.
Alisema matatizo ya Zanzibar yatapata ufumbuzi wa kudumu kama katiba itaandikwa upya na sheria zote za uchaguzi kurekebishwa.
Msimamo huo hauna tafauti na kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa NLD, Rashid Ahmed Rashid ambaye alisema chama chake kinasubiri maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM, ili kiweze kuchukua hatua, kwa vile vyama vya CCM na CUF havina haki kubadilisha katiba peke yao bila ya ridhaa ya wananchi wote.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Ambar Khamis, alisema hatua za mazungumzo zinazoendelea zinafaa kungwa mkono, lakini mjadala wa utekelezaji wake, lazima na viongozi wa kambi ya upinzani washirikishwe.
Source: Tanzania Daima