Hivi sasa nipo katika moja ya nchi za kiarabu, nimefurahi kuona wao bado wanaendeleza utamaduni ambao tulikuwa nao hapo zamani Africa na sasa tunauacha. Majuzi rafiki yangu mmoja anasema alimpeleka mpwawe kwenda kuona mchumba aliyechaguliwa na wazazi, na mambo yote yamewekwa sawa. Ikanikumbusha mbali kipindi hicho nasi tulikuwa tukichaguliwa wachumba, lakini aah! mbona wazazi wetu waliishi tena vizuri tu na miaka mingi bila kuachana. Sisi leo tunajichagulia wenyewe wachumba hata mwaka bado kila mtu na lake, naamini baada ya kupewa mke/mume kikubwa kinakuwa huyu ndiye mwenzangu ktk hali zote. Muungano wetu unafanana na wanandoa waliooana kwa ridhaa ya wazazi, mzee wetu Karume na mzee wetu Nyerere waliamua kwa niaba yetu kama inavyosemwa na wengi. Lakini kama ndoa muungano ni kitu kizuri, iwe tumeungana kwa ridhaa na maoni yetu wenyewe au kuunganishwa kama ilivyo sasa. Kinachoonekana wenzetu wengi wa visiwani hawapendelei kuwa ktk huu muungano, na kila kasoro itakayoonekana wataitumia hiyo kuonyesha kuwa muungano si sawasawa. Nifahamuvyo mimi si kwamba bara hatuzioni hizi kasoro la, ila cha thamani ni kipi muungano au kasoro?. Kawaida vinapoungana vitu viwili kuzaa kimoja, vitu hivyo hupoteza asili yake na huo ndio muungano. Huwezi kuungana halafu ukawa tena bado vile vile, huo hautakuwa muungano ni ushirikiano. Hadithi hii nzima inanikumbusha nyumba ya rafiki yangu mmoja tuliyeshibana sana, kipindi alichooa alipata taabu sana. Mke kila leo kwao, nini mama kaniita, kesho kuna hili nyumbani, keshokutwa sababu hii. Alipata taabu kweli, alijaribu kutafuta msaada wa ushauri ikashindikana, na bahati mbaya ni ndoa ya kikristo akawa hana jinsi tena. Nyumba iliyumba sana, kwa sababu tu binti alijiona ana kwao. Hakuwa anajali lolote linaloweza kutokea kwa kuwa mama yupo, ikatokea bahati mbaya mama yake akafariki dunia ikawa safari za kwenda kwa mama zimekufa tena. Huwezi kuamini binti akatulia kweli, nyumba imekuwa na amani na sasa hata maendeleo yanaonekana, maana wanashirikiana. Inaonekana ndugu zetu wa Zanzibar wanaamini bado wanaye mama wa kumkimbilia, wanaamini kama si huu muungano saa hizi wangekuwa mbali, Mama angeshawasaidia. Kwa mwelekeo huu watakapotambua kuwa mama waliyefikiria kuwa yupo hayupo wamechelewa. Kilichotakiwa ni kutambua kuwa sisi ni ndugu na hawa wazee wetu hawakukosea kutuunganisha, kwani wameunganisha ndugu. Inaweza kuonekana walikuwa na sababu zao, lakini haitabadilisha undugu wetu. Hata tukiamua kuwa leo basi kila mtu ashike njia yake bado tutakuwa ndugu tu, ingewezekana kabisa kuwalazimisha viongozi wetu waweze kushuhughulikia kasoro zilizopo maana hakuna asiyeziona lakini kwanza iwepo nia. Na nia ni je tunautaka muungano au hatuutaki?, hizi sababu haziwezi kufanya muungano ukaonekana ni kitu kibaya hivi. Hebu fikiria wale waliooana kwa mapenzi ya wazazi, unafikiri hawakuti kasoro?. Inakuwa ni siri yao, kwao kikubwa ni ndoa yao na ndio maana wazee wetu zamani waliweza kuishi mpaka kifo ndio kikawatenganisha. Kasoro zipo na zitaendelea kuwepo, wala zisiwe sababu, mseme tu kwamba jamani eeh! kila mtu achukue ustaarabu wake tumempata mama wa kutusaidia kutoka kwenye huu umaskini!. Tutawaelewa tu, wala msiwe na hofu.