- Hoja binafsi kwa wazalendo ipo mezani!
- Operesheni megua muungano Zanzibar kuanza jimbo kwa jimbo!
Na: Malik Nabwa
Zamani mtoto akilia sana usiku tukimchombeza kwa nyimbo. Tukianza na nyimbo za kuchezea watoto kuanzia makwaya kwaya kamndindiliya, adi adi. Tukiona hanyamazi tunaimba nyimba za Samba. Kisha msewe, tarazia, kibandiko, boso, mbware, na kama mtoto bado hanyamazi tukimpiga ubeleko. Ndani ya mbeleko akiendelea kulia tukimuoshakwa maji maana tukidhani ana joto. Yakishindwa yote haya mtoto bado hasikii dawa na anaendelea kulia sasa tukimtisha kwa babu mduma. Zote hizi ni juhudi tu za kumreburebu mtoto anyamaze maana kilio ni ghasia na hunyima watu raha.
Na muungano wetu wa Tanzania ni mithai ya mtoto mlizi. Tumekwisha kila rai kuutaka Muungano huu ama uondoke, au basi angalau urekebishwe ili unufaishe sehemu zote mbili sawasawa lakini wapi?. Juhudi hizi zimeshindikana. Tulitaka muungano uangaliwe upya, tukaonekana tunabwabwaja tu. Tukataka tupunguziwe mambo ya Muungano yasio na faida bado kimya. Baya zaidi Raisi wetu aliepo madarakani kila jambo analoletewa na wasaidizi wake husema hilo ni la Muungano kwanza nalipitie bara huko ndio lijadiiwe hapa. Tumeona hivi karibuni jinsi mamilioni ya Brunei yalivyorudishwa hivi hivi kwa Rais kukataa nchi hiyo kuisaidia Zanzibar kama nchi akisisitiza kupitia Muunganoni kwanza. Kwa haya machache na mengine mnayoyajua na kuyaona kwa mato yenu ni dalili tosha kuwa njia mbadala ya kujinasua haipo.
Kumwaga damu haina haja na si katika njia nzuri ya kudai haki iwapo haina ulazima. Tulishajaribu ikashindikana mara moja hiyo. Lakini kwa sasa kuna njia mbadaa ya kuutumia umma wa Zanzibari kuitatua hili. Ninaposema nguvu ya umma sikusudii tuandamane, la hasha. Katika Operesheni Megua muungano visiwani hatukusudiii kabisa kuingia barabarabani. Bali tutatumia utaratibu sahihi wa sheria na katiba ya nchi na tukishikamana kiukwei basi tutafanikiwa muda si mrefu. Wazalendo wenzangu, kampeni MEGUA haina nia ya kuuvunja muungano. Neno MEGUA maana yake kuunyofoa nyofoa kidogokidogo mpaka tukajua moja. Kupata haki yetu au kuufanyia marekebisho Muungano huo ukawa wa manufaa zaidi kwa kila mmoja wetu. Ikishindikana hivyo tutaendelea kuumegua hadi tuumalize. Nyumba isiyo nguzo haisimami, na hii ndio falasafa ya Operesheni MEGUA. Na ili tuuangushe huu ni kuumegua nguzo zake muhimu.
Operesheni megua itaendeshwa na wazaendo wenyewe. Haitagharimu hata senti kumi lakini itahitajai umakini na kujitolea kulikotukuka. Operesheni hii itafanyika katika kila jimbo.Zanzibar ina majimbo hamsini na wawakilishi hamsini pia. Shida yetu juu ya hili sio wabunge bali ni Wawakilishi. Kwa vile katiba ya Zanzibar inaruhusu wananchi kupiga kura ya maoni juu ya kila mabadiliko ya katiba Operesheni MEGUA itakitumia kipengee hiki kukusanya maoni ya wananchi katika kila Jimbo kuhusu jambo moja moja la Muunagano ambalo wananchi hawalitaki. Tutaandaa barua rasmi (Muundo na kiambatisho kitawekwa hapa baada ya wazo hili kupitishwa na wazalendo) itakayaopelekwa kwa mwakilishili wa kila jimbo baada ya kupata ridhaa za wanajimbo na sahihi zao kuhusu kukubali au kukataa jambo Fulani la Muungano.
Baada ya maoni ya wananchi katika kila jimbo yakipata kuungwa mkono barua hiyo na dodoso yenye orodha ya wanajimbo walio wengi kutia saini kutokubali suali hilo kinachofuata hapo ni kumpa barua hiyo na dodoso Mwakilishi na kumtaka alifikishe wazo lile au hoja hile jumba la kutungia sheria huko Mbweni; yaani Baraza la wawakilishi. Zoezi hili litakuwa gumu lakini likisimaiwa vizuri linaweza kuleta athari kubwa sana katika jamii zetu. Itakapofikia hatua tukapata angalau majimbo 30 tu yakafanikisha zoezi hili na barua hizo kuwasilishwa mikononi mwa Wawakilishi huku baadhi ya kopi zikiwekwa kama kumbukumbu kwa taasisis za kiraia na zile za Kimataifa basi utakuwa tumefanya kazi kubwa. Kitakachobakia ni kwa Wawakilishi kusuka au kunyoa. Ni juu yao kuamua kuyafikisha maoni yetu kunakohusika au kuyakalia na kutoyafanyia kazi, ili kusubiri tuwaoneshe hasira zetu kwa kutowachagua au hata kuwaengua nyadhifa zao kwa kushindwa kutufikishia matakawa yetu kunakohusika.
Katika fomu hiyo tutaorodhesha baadhi ya mambo ya muungano ambayo kwa sasa lazima yaondolewe kama mambo ya Muungano na kuachwa kuwa chini ya nchi husika; Zanzibar na Tanganyika. Mambo kama vile TRA, bandari, Mafuta, NECTA, na Mambo ya Nje n.k yatakuwemo katika dodoso atakayoulizwa mwana jimbo na kutoa maoni yake.Lakini kabla ya huko ni nafasi yako mzalendo kutoa maoni yako juu ya hili.
Wazalendo, mnaonaje wazo hili? Linafaa? Tutaweza? Nasubiri maoni yenu. Sina mengi leo!
Wakatabahu
Nabwa