Muungano wa Tanganyika na Zanzibar: Una faida gani na kwa manufaa ya nani?

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar: Una faida gani na kwa manufaa ya nani?

Nyinyi mambo ya Zanzibar au tuseme ya Unguja na Pemba yanawahusu nini?

Kwanini hamushughulikii matatizo yenu kwanza huko bara mkayamaliza?

Ya Wazanzibari waachieni wenyewe au ndio mnatuonyesha kwamba nyie ndio Watawala na Zanzibar ni Koloni lenu.

Kabla ya kuleta hoja ukumbini, fanyeni utafiti wa chanzo cha madai yao hao watu.

Hii habari ni ya zamani, chunguza sababu na yaliishia vipi sio kuendekeza fitna tu miongoni mwa Wazanzibari kwa maslahi yenu.

Hata mfanye nini Zanzibar bila ya Tanzania/Tanganyika inawezekana.

si mjitenge baadaye muombe kurudi
 
Hata hawajavunja bado huu wa Tanganyika na Zanzibar sasa wemeshaanza Pemba na Unguja? Itakula kwao hadi watafika hatua watoto watawaambia wazazi wao waachane kwa sababu watoto hao hawakuwepo wakati wazazi hao wanaoana.

Hahah,umefikiria mbali sana ndugu yangu. Ni kweli, sometimes tuiachie nature ichukue mkondo wake. Kiimani pia kila jambo linakuja na sababu yake, Mungu ibariki Tanzania.

Tukirudi nyuma kujiuliza why this o that haisaidii kitu,tuweke mikakati ya kujikwamua kimaisha kwa kupambana na linalotukwamisha.
 
Ama nyinyi mnajidanganya sana tena sana tu.

Kabla ya kuja na fitna zenu, Zanzibar mliikuta huru na yenye uchumi imara usiotetereka na haikuwa inategemea nchi yoyote ile katika uso huu wa dunia.

Enter Nyerere kwa ujanja na chuki zake:

"If I could tow that island out into the middle of Indian Ocean, Id' do it."

Baada ya miaka 47, Zanzibar imerudi nyuma miaka kadhaa kutokana na fitna za Tanganyika.

Mnadhani Zanzibar haijiwezi kujiendesha wenyewe? Kabla ya hapo mlipotuvamia ilikua ikoje?

Wazanzibar wameshamjua adui yao na hawaingii tena fitna zenu na muda si mrefu mtajikuta mnatafunana wenyewe kwa wenyewe kwa kuendekeza ufisadi na kuchunana ngozi.

Zanzibar will rise again and the Second Republic can not be stopped.


*"Ule wakati wetu na Nyerere tlikuwa tunakubali lakini hawa vijana wa leo hwakubali, Bw. Sitta, ITS OVER*". - Hassan Nassor Moyo, former SMZ/SMT Minister and ASP/CCM Veteran.
"Its now or never" - Mansour Yusuf Himid, Minister SMZ/MNEC CCM



 
Halafu wa bara wanaishi zanzibar wanaonewa vibaya, kuanzia na taasisi za serikali ya zanzibar hadi watu binafsi, hamna pa kupeleka malalamiko,
nina ushahidi wa mwanafunzi aliyetoka dodoma kuja kwa mafunzo training ya kitalii, aliharibiwa na wanaume wawili, alichanwa kotekote na kuumizwa vibaya, kisha wakamtupa akiwa na kinyesi na damu mwili mzima, baba yake mzazi alikuja baada ya wanafunzi wenzake kumpigia simu, alishindwa la kufanya hadi akaamua kumtibu mwenyewe na kukimbia nae. Hamna ushirikiano wowote kwa serikali au watu.
 
Nyerere kwa kweli duh! Alisema mkishaanza sisi Watanganyika na hawa Wazanzibari mtajikuta kuwa kwa Wale waZanzibari kumbe hakuna Mzanzibari bali kuna Mpemba na Muunguja. Akasema na Bara vile vile, mkishawatenga Wazanzibari mtaanza kujikuta kumbe kuna Wachagga na wapo Wasukumu. Ndipo akasema "dhambi ya ubaguzi haikomi, ikishaanza kula haikomi".

Sasa hata muungano wenyewe haujafika mwisho wameanza mambo ya Uunguja na Upemba! na Dar itakuwa ni kati ya Wapwani na Wabara?

Mwanakijiji, naona unaunga mkono jambo ambalo halina uthibitisho, labda kwa sababu unalipenda...!

Kuna uhakika wowote kama kweli kuna walio andika barua kupeleka Umoja wa Mataifa!?


Kwa nini msitafute uthibitisho wa hiyo barua kwanza... tatizo ni nini!?
 
makaimati, msijidanganye kwa vijisenti vya watalii wa italy, walioletwa na zakia menghji na balozi wa tanzania italy ali karume, mnajua utalii ni mvuke tu, chochote tu kitokee watalii hawaji tena, pia jua bara tuna bahari clean na yenye mchanga mweupe kama zanzibar, ambavyo vitu vinavyoleta watalii wa holiday kupumzika beach, sisi licha ya kisiwa cha mafia, hapa dar tuna bongoyo na mbudya na vingine vingi tu.
 
Mkuu Pharaoh, hatujinganyi na wala hatushindani na nchi kubwa kama Tanganyika hata kidogo. Wazanzibari wanajua potential yao na limitation zao pia lakini wanataka fursa ya kujiamulia mambo yao wenyewe tu.

Tanganyika imetubana sana Mkuu hatufurukuti hata kidogo na kila tukitaka kujipapatua, mnatugonga nyundo nzito.
 
Halafu wa bara wanaishi zanzibar wanaonewa vibaya, kuanzia na taasisi za serikali ya zanzibar hadi watu binafsi, hamna pa kupeleka malalamiko,
nina ushahidi wa mwanafunzi aliyetoka dodoma kuja kwa mafunzo training ya kitalii, aliharibiwa na wanaume wawili, alichanwa kotekote na kuumizwa vibaya, kisha wakamtupa akiwa na kinyesi na damu mwili mzima, baba yake mzazi alikuja baada ya wanafunzi wenzake kumpigia simu, alishindwa la kufanya hadi akaamua kumtibu mwenyewe na kukimbia nae. Hamna ushirikiano wowote kwa serikali au watu.

Mkuu Pharaoh,

Mimi ni mmoja wa watu ambao sifurahii vitendo vyovyote visivyokuwa vya kibinaadamu, iwe vimemkuta mtu wa Bara au Zanzibar. Hicho kisa unachokizungumzia ni kisa cha kinyama ambacho kilipaswa kulaaniwa na kila mtu. Siwezi kuisemea Serikali lakini inauma zaidi kwamba huyo dada hakuweza kupata hata msaada wa raia wema. Inasikitisha sana, inauma na inachefua.

Jambo moja ambalo hukulieleza ni iwapo watuhumiwa walikamatwa na wakaachiwa na Polisi au hawakujulikana. Kama hawakujulikana na kwa hali ilivyo ya Zanzibar ya sasa, sio jambo la ajabu kuwa wahusika walikuwa ni wenzake kutoka Bara maana taarifa za Wazanzibari kufanya vitendo hivyo ni vigumu kuingia akilini ingawa pia inawezekana.

Hili la kuwa hatuna ushirikiano si la ukweli (siisemei Serikali) kwani mimi binafsi nnao marafiki wengi kutoka Bara tena Waislam na Wakristo. Naao marafiki TTCL, NMB, TRA, GAPCO,MECCO, JWTZ na sehemu nyingi sana nyenginezo na tunaishi nao na tunashirikiana VIZURI sana tu.

Nikupe mfano mwengine labda utashangaa:

Mimi kuna mzee mmoja wa Kinyamwezi tumejuana tokea mwaka 1961 sehemu za Kaskazini ya hapa, wakati huo nafundisha huko. Nilipohamihiwa hapa, tuliondoka nae na nimeishi nae mpaka amefariki hivi mwaka juzi tu. Aligongwa na gari na nimemgharimia matibabu yake na nimemuuguza mpaka amepona na amekufa mwaka juzi tu na nimemzika kwa gharama zangu na msaada wa ndugu na marafiki. Hakupata kurudi tena kwao na wala hakutamani kuondoka hapa nyumbani pangu. Nimeishi nae kwa amani sana. Mifano hii ipo mingi tu.

Tatizo la Wazanzibari sio Watanganyika bali ni mfumo huu wa "MUUNGANO" ambao nchi moja kubwa inaikalia nchi moja ndogo na kuipora madaraka na mamlaka yake.

Ikiwa kwa miaka 47, kero hazikuondoka, ni vyema tukajiangalia upya maana "MUUNGANO" wenyewe umekua kero
 

Mwanakijiji, naona unaunga mkono jambo ambalo halina uthibitisho, labda kwa sababu unalipenda...!

Kuna uhakika wowote kama kweli kuna walio andika barua kupeleka Umoja wa Mataifa!?


Kwa nini msitafute uthibitisho wa hiyo barua kwanza... tatizo ni nini!?


Mkuu hilo ni kweli na kuna mdau kalitolea ufafanuzi vizuri tu.

Maneno ya Nyerere sisi hatuyajali sana maana yeye ndie aliemtisha Karume kuwa Waarabu watarudi lakini yeye ndie aliemwambia Dr. Omar ?(the late VP),

"Viongozi wetu hawana la maana kuwaeleza wananchi wao, isipokuwa Hizbu,imefanya hili na Sultani alikuwa akifanya lile na lile.Jee, jamani vijana wetu tuliokuwa nao, hivi sasa ni nani anaeijuwa Hizbu ni nani anaemjuwa Sultani? Hivi kweli hamna zaidi ya haya kuwaeleza wananchi?"

The guy was simply an inteligent psycopath.
 
Bila kujadili Muungano Katiba mpya haijadiliki
Joseph Mihangwa

MOJA ya matakwa ya Muswada wa Marejeo ya Katiba wa mwaka 2011 ambao mchakato wake umeanza kwa njia ya maoni ya wananchi, ni kutoguswa au kuzungumziwa kwa suala "nyeti" la Muungano ambalo kwa mtazamo wa Serikali madarakani, ni "fumbo la imani" lisiloweza kujadiliwa.

Katazo hilo limezua miguno na malalamiko mengi miongoni mwa wananchi wakielezea kuwa, kitendo hicho cha kuwekewa mipaka ya maoni juu ya Katiba wanayotaka ni "demokrasia ya kuongozwa" [guided democracy] au kushinikizwa, inayowakweza watawala juu ya wananchi ili watawala hao waonekane wao ndio taifa na taifa ndilo wao.

Huko Zanzibar, wananchi wamechana hadharani mbele ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, nakala za muswada huo wakitaka suala la Muungano lizungumziwe, na kwamba wapewe Katiba ya Tanganyika kwanza.

Akichangia hoja, mmoja wa waasisi wa Muungano Visiwani, ambaye alikuwa Waziri wa Sheria na Katiba wakati Tanganyika na Zanzibar zikiungana mwaka 1964, mzee Hassan Nassor Moyo, alisema amekuwa shahidi wa makubaliano ya Muungano jinsi ulivyofikiwa na kuendeshwa kwa mikwara, na kwamba hakuna asichokifahamu. Kwa hiyo, alitaka suala la wananchi kupewa uhuru wa kujadili Muungano wao lipewe nafasi kubwa.

"Mnatuambia tusizungumze suala la Muungano, mnataka tuzungumze nini hapa wakati jambo hilo ndilo la msingi; mnataka tuzungumze nini?", alihoji.

Akasisitiza kuwa, kosa la kutowashirikisha wananchi juu ya Muungano wanaoutaka, kama ilivyokuwa mwaka 1964 lisirudiwe tena, ikizingatiwa kuwa hivi sasa vijana wamesoma, sio wajinga walivyokuwa wakati huo.

Mzee Moyo; huku akionyesha Hati [Mkataba] ya Makubaliano ya Muungano, alidai kuwa makubaliano hayo [juu ya mambo kumi na moja tu] yamekiukwa na hivyo Mkataba wa Muungano kuvunjwa, na kwamba, kwa sasa vijana hawawezi kupangiwa mambo kama ilivyokuwa huko nyuma.

Naye Waziri wa Katiba wa Zanzibar, Abubakar Khamis Bakari alisema, utaratibu uliotumiwa kuandaa muswada huo si sahihi kwa kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar haikushirikishwa wakati wa kuandaa rasimu hiyo.

Kuna mantiki katika malalamiko haya kwa sababu kuu mbili: kwanza ni kwamba, tunapozungumzia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunazungumzia Mkataba wa Muungano huo [Articles of Union] kwa mambo yanayoziunganisha Tanzania Bara na Zanzibar. Kwa sababu hiyo, bila Mkataba wa Muungano hakuna Muungano, na hivyo hakuna Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Vivyo hivyo, kwa kuwa Katiba ya Muungano inagusa mambo ya nchi mbili – Tanzania Bara na Zanzibar, kwa sababu hiyo inagusa pia Katiba ya Zanzibar inapofika suala la mgawanyo wa madaraka [distribution of powers] ndani ya Muungano, na hivyo kufanya suala la Muungano lisiepukike hivi sasa tunapojadili suala la Katiba mpya.

Hili la mwisho ndilo limekuwa kiini cha kero za Muungano tangu kuanzishwa kwake hadi sasa, kiasi kwamba Muungano wetu leo ni gari bovu juu ya mawe.

Tushukuru mfumo wa kidikteta wa Chama kimoja, kwamba tumeweza kufika hapa tulipo pamoja na mapungufu hayo kwa sababu tu hoja zenye matakwa ya wengi ziliweza kuzimwa kwa kiatu kizito huku tukijiliwaza kwa dhana ya "amani na utulivu" wakati ukweli ni kinyume chake.
Watanzania wangali wanazikumbuka "choko choko" za Muungano za miaka ya 1970 kwa baadhi ya Wazanzibari kudai kurejeshewa Visiwa vyao [Unguja na Pemba] "vilivyomezwa" na Tanganyika kufuatia Muungano mwaka 1964.

Sote tunakikumbuka kipindi cha "Kanda za Kiroboto" [The Kiroboto Tapes] kilichotangazwa moja kwa moja kupitia Redio Sauti ya Zanzibar, jambo lililowaacha wengi mdomo wazi, wakiuliza ni vipi kipindi hicho kitangazwe kupitia Redio ya Serikali ya Zanzibar!

Watanzania hawajasahau pia jinsi Rais Aboud Jumbe alivyopigwa buti nje ya ulingo kwa kunyang'anywa madaraka ya urais mwaka 1984 kwa "kosa" la kutaka kupata ufafanuzi sahihi juu ya muundo sahihi wa Muungano unaotumika. Na kwa tabia yetu ya mbuni, tulitangaza "kuchafuka kwa Hewa Visiwani", ndiye Jumbe, licha ya kufukuzwa urais wa Zanzibar alipewa "kifungo cha nje" nyumbani kwake Mji Mwema, Dar es Salaam ambako anaishi hadi leo.

Suala la Zanzibar kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu [OIC] bila ridhaa ya Serikali ya Muungano, mwaka 1992, na hoja ya kundi la Wabunge 55 [G.55] kutaka kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika, ni moja ya mitikisiko inayoonyesha dhahiri kwamba mambo si shwari ndani ya Muungano, na ambayo yanatakiwa kupata ufafanuzi sahihi ndani ya Katiba mpya.

Utasemaje kwamba mambo ni shwari wakati huko Zanzibar Watanzania wamegawanyika kwa misingi ya ubaguzi wa "Wazanzibari" na "Wazanzibara" ndani ya "nchi" moja?

Yalipogunduliwa mafuta huko Visiwani hivi karibuni, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitamka wazi kwamba Serikali ya Muungano isithubutu kuingiza pua yake Visiwani kwa hilo, wakati Katiba ya Muungano inatamka wazi mafuta ni suala la Muungano [Ibara ya 4 – Katiba]. Serikali ya Muungano imefyata mkia kwa jambo la Kikatiba lililo wazi.

Septemba 2005, pengine kwa kujisahau, au kwa kudharau Katiba ya nchi na Muungano, Rais Amani Abeid Karume, alituma salaam za rambi rambi kwa Rais George W. Bush kwa maafa ya New Orleans nchini Marekani, yaliyosababishwa na kimbunga Kartrina, kama Rais na kwa niaba ya Wazanzibari, wakati hakuwa na mamlaka ya kufanya hivyo, isipokuwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano tu.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 4, suala la Ushirikiano wa Kimataifa ni la Muungano na mwenye kauli juu ya hilo ni Rais wa Tanzania pekee. Kwa hiyo, Rais Karume alivunja Katiba ya nchi ama kwa makusudi, au kwa kutoelewa au kwa hulka ya kudharau Muungano; huku akijua nini alichofanya.

Hili halikusemwa na waliokuwa madarakani kwa sababu hakuna anayejali matakwa ya Muungano tukiambiwa "Muungano ni suala nyeti" lisilopaswa kuzungumziwa hivi hivi tu.

Iwe hivyo isiwe, ukweli ni kwamba Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar hauwezi kuendelea kuchukuliwa kama "suala nyeti" lisilojadilika badala ya kuchukuliwa kama "suala tete".

Huu ndio msimamo mpya aliokuwa nao Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1993 alipohutubia Bunge mbele ya Rais Ally Hassan Mwinyi na kubainisha kwamba, suala kuhusu muundo gani wa Muungano Watanzania wangependa utumike, ni agenda inayojadilika, ingawa yeye alikwishaweka wazi msimamo wake juu ya ama kuendelea na mfumo wa serikali mbili wa sasa, au kuundwa kwa Jamhuri ya Tanzania, yaani kuigeuza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa nchi moja yenye serikali moja.

Lakini sote tunajua kwamba, Wazanzibari hawawezi kukubali kuundwa kwa nchi yenye serikali moja. Hii ndiyo hofu yao tangu mwanzo ya Zanzibar kumezwa na Tanganyika.

Na kama hivyo ndivyo, na kwa kuwa hali ya sasa imeshindwa kukidhi demokrasia, amani na utulivu, nini kifanyike kurekebisha hali na kuimarisha Muungano? Je, tuendelee kuzika kichwa mchangani mithili ya mbuni? Je, hatukutahadharishwa na Mwalimu Nyerere, kwamba "afichaye ugonjwa kilio kitamuumbua"? Ukweli kilio kimetuumbua mara nyingi na tutaendelea hivyo. Sasa Zanzibar ni nchi yenye Katiba yake na taasisi zote kufanya iitwe nchi!

Katika hali tete kama hii, watu wenyewe, na si viongozi wao, waachiwe kuamua mwelekeo na hatma yao ya kisiasa. Ni makosa kwa serikali kutanguliza mbele maslahi ya walio madarakani na kufifisha haki ya watu ya kuamua au kutatua matatizo yanayowasibu.

Hali hii ndiyo inayokaribisha matumizi ya nguvu na mabavu katika chaguzi chini ya demokrasia iliyokabwa koo na kuongozwa kwa sababu tu watu fulani wasingependa kuona matokeo kinyume na matarajio yao, na kuwa suala la demokrasia kufanya kazi eti lina ugumu wake. Ugumu gani huo? Kwa nani, na kwa nini?

Kuna ugumu gani kama watu wataamua kutumia kura zao kuamua jinsi wanavyotaka watawaliwe? Na kama upo, kwa nini tunauficha, au kwa nini tumeulea hata watu waamue gizani kwa kufichwa ukweli? Kwa kuuficha umma mambo na kuupotosha katika kufikia maamuzi, basi, hatuwezi kukwepa kuitwa "wahaini" wa kustahili kitanzi.

Nchi yetu sasa inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, unaosisitiza kuheshimiwa kwa uhuru wa kuamua na matakwa ya watu, badala ya kuongozwa na matakwa ya viongozi, na pengine kwa matumizi ya nguvu na ulaghai ili kuungwa mkono uhuru huo ambao ni haki ya kikatiba lazima ulindwe.

Nini kinachosababisha mitafaruku ndani ya Muungano mara kwa mara? Kama Wazanzibari hawapendelei mfumo wa serikali moja kama njia ya kumaliza mitafaruku kwa hofu ya kumezwa, nini kifanyike kuridhisha pande zote ili Muungano uendelee kwa amani na utulivu?
Majibu ya maswali haya yatapatikana kwa kuangalia tu historia ya Muungano wenyewe, kuona kilichotarajiwa, udhaifu na mapungufu yanayorekebishika.

Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar uliofikiwa April 26, 1964, ulitokana na sababu kubwa mbili: Sababu ya kwanza ni hofu ya Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, kupokonywa madaraka na wanamapinduzi wenzake Visiwani, hasa wale wa kikundi cha siasa za mrengo wa kushoto wakiongozwa na hayati Abdulrahman Babu [Umma Party] na Abdallah Kassim Hanga [ASP].

Nyerere aliwahi kukiri kwamba, Karume alipendekeza wazo la Muungano kwake kwa mara ya kwanza walipokutana Dar es Salaam [Januari 15, 1964] kuzungumzia suala la "Field Marshal" John Okello, mmoja wa walioshiriki katika mapinduzi ya Januari 12, 1964, ambaye pia ndiye aliyetangaza mapinduzi hayo kupitia Redio ya Taifa, Zanzibar. Lakini dhana hii haina nguvu baada ya ushahidi mwingi kuonyesha kwamba Karume alishinikizwa.

Sababu ya pili ni shinikizo la nchi za Magharibi kutaka Zanzibar iungane [na kumezwa] na Tanganyika ili kuviokoa Visiwa hivyo kuangukia upande wa kambi ya Kikomunisti ya Warusi na Wachina kufuatia mapinduzi Visiwani enzi hizo za vita baridi, kati ya nchi za kibepari za Magharibi na za kisoshalisti za Mashariki.

Ndiyo maana siku ya Muungano, Marekani, Uingereza na Tanganyika, ziliandaa majeshi kuivamia Zanzibar kama wananchi wangeasi au kuupinga Muungano uliopangwa. Kwa hiyo, kwa Marekani na Uingereza ilikuwa moja tu kati ya mambo mawili: ama Muungano au nguvu za kijeshi zitumike kuharibu mapinduzi ya Zanzibar. Huu ndio ukweli juu ya chimbuko la Muungano; sababu zingine zinazotolewa ni za kudandia tu.
Kuungana kwa nchi hizi mbili kulifanyika haraka haraka kiasi kwamba hapakuwa na muda wa kuandaa Katiba madhubuti ya Muungano. Kilichofanyika ni kwa viongozi wa nchi hizi mbili, Rais Nyerere na Karume kufikia makubaliano ya dharura na mambo mengine muhimu kuachwa kwa matarajio ya kuwekwa sawa baadaye hali itakapokuwa shwari. Hata hivyo hali hiyo haijatokea na inazidi kuchafuka kwa jina la kero za Muungano.

Mazungumzo juu ya Muungano yalifanyika kwa siri ya hali ya juu sana. Kumbukumbu zilizopo na maelezo ya waliokuwa madarakani enzi hizo yanaonyesha kuwa, si watu wengi katika Serikali ya Tanganyika na Baraza la Mapinduzi Zanzibar waliojua kilichokuwa kikitokea. Mbali na Nyerere na Karume, wengine waliojua kilichokuwa kikifanyika walikuwa mabwana Rashid Kawawa, Oscar Kambona, Abdallah Kassim Hanga na Salim Rashid.

Mazungumzo yalipokamilika, Nyerere alimwita Mwanasheria wake Mkuu wa Serikali, Roland Brown na kumwagiza aandae haraka sana Hati ya Makubaliano ya Muungano bila mtu mwingine kujua. Hati hiyo [Articles of Union] iliandaliwa kwa muda mfupi mno siku hiyo [21/4/1964] na kutiwa sahihi April 22, 1964, kisha kupelekwa Bungeni haraka haraka kuridhiwa kuwa Sheria [Acts of Union] Aprili 25, 1964; na Aprili 26, Muungano ukatangazwa.

Kwa upande wa Zanzibar, Karume kabla ya kutia sahihi Mkataba huo, alimpa Mwanasheria wake Mkuu, Walfango Dourado, likizo ya lazima ya dharura ya siku saba; badala yake akamwita Mwanasheria kutoka Uganda, Dan Wadada Nabudere, kuja kumshauri juu ya Hati hiyo ya Muungano iliyowasilishwa na Tanganyika. Wote, Brown na Nabudere walihudhuria majadiliano kati ya Nyerere na Karume. Bado ni fumbo kubwa kwa nini Dourado hakushirikishwa; lakini inaaminika ni kwa sababu ya msimamo wake mkali wa kikomunisti kwamba asingeridhia Mkataba huo.

Hati za Muungano [Articles of Union] zilizotiwa sahihi na marais hao zilitoa picha na dira tu ya Muungano na mambo mengine yaliachwa kushughulikiwa na Tume ya Katiba iliyokuwa iteuliwe kupendekeza Katiba kabla ya kuitishwa Bunge la kupitisha Katiba ndani ya muda wa miezi 12 tangu Muungano.

Kama tunavyofahamu, Tume hiyo haikuundwa na Muungano uliendelea kuendeshwa kwa kutumia Katiba ya Muda [Interim Constitution] kwa miaka 13, hadi 1977 ilipopitishwa Katiba ya Kudumu kwa mapendekezo ya Tume iliyoteuliwa kuona uwezekano wa kuunganishwa kwa Vyama vya TANU na ASP. Tume hiyo ya Chama si ile inayotakiwa chini ya makubaliano ya Muungano na Sheria za Muungano.
Nini kilitokea? Kwa nini Tume ya Katiba haikuundwa? Majibu ya swali hili ni muhimu katika kuelewa chanzo na sababu za mgogoro wa Kikatiba unaoukumba Muungano wetu.

Dhana moja inaeleza kwamba, Tume hiyo haikuundwa kwa sababu Viongozi Wakuu hao wawili walianza kujuana vizuri na kugundua tofauti zao kuonyesha kwamba wasingeweza kufanya kazi pamoja kwa muda mrefu kutokana na tofauti za mitizamo. Hapa kulikuwa na Nyerere, msomi na mwenye hulka ya utawala wa nguvu asiyeyumba; na kulikuwa na Karume mwenye kisomo duni na "msanii" kwa tabia, kwa vitendo na asiyeshaurika lakini mwenye kujiamini na mwenye msimamo mkali.

Kwa watu hawa wenye tabia na misimamo kinzani, haikuwa rahisi tena kuunda Tume kuweza kupata maridhiano ya maana kwa jambo kama Muungano. Kwa hiyo waliishia kubakia na Muungano hohe hahe, usio na mbele wala nyuma, na Katiba ya muda isiyomaliza kipindi cha mpito kuendesha nchi.

Wachambuzi wa mambo ya siasa wa enzi hizo walibaini mapema kuwa, Muungano huo ulikuwa ukielekea kubaya kama busara isingetumika kuuokoa. Hadi leo busara haijatumika, badala yake unaongozwa kwa akili ya kichwa cha mbuni.

Wengine wanathubutu hata kutabiri kwamba, kama Karume angeishi miaka mingine kumi, Muungano huu ungekoma sawia. Wakati huo huo nyufa katika Muungano ziliendelea kujitokeza kwa kasi kubwa.

Kutoundwa kwa Tume ya Katiba na kutoitishwa kwa Bunge la Katiba kuweka sawa mambo muhimu ya Muungano, kuliwapotezea Watanzania nafasi nzuri ya kuwa na Muungano imara na unaoeleweka; badala yake nchi iliendeshwa kwa Katiba ya "mbavu za mbwa", isiyokuwa na kichwa wala miguu. Hiki ndicho chanzo cha migogoro yote ya Muungano.

Ni kwa sababu hii Muungano wetu umeendeshwa kwa nguvu za kisiasa na kwa vyombo vya dola badala ya Sheria na busara kutawala chini ya Katiba makini. Ni tabia kwamba mahali busara inaposhindwa kutawala, udikteta huingia, demokrasia hufa, amani hupotea, hofu na machafuko hujongea kuangamiza taifa lenye mgawanyiko.

Kama waasisi wa Muungano wetu wangezika tofauti zao mapema na kuteua Tume ya Katiba, mapungufu ya Muungano yangerekebishwa mapema na Muungano kuimarika.

Mpaka leo, wataalamu wa mambo ya Katiba wanakiri kwamba mfumo wa Muungano wetu haueleweki na haumo kabisa katika miundo ya Katiba duniani kote. Na kwa kuwa tumejijengea tabia ya mbuni, hatuwezi kuliona hilo; tunakiri, lakini kwa maelezo kwamba "Muungano wetu ni wa pekee na wa aina yake", kuashiria unafiki na uvivu wetu wa kufikiri.

Sawa; unaweza kuwa Muungano wa aina yake, lakini je, umeleta matunda? Kwa muda mrefu tumejivunia amani; mbona Muungano huu unaendelea kuwa chanzo cha kuvunjika kwa amani na kudhoofika kwa umoja wa Kitaifa?

Jaribio la kutekeleza yale yaliyokusudiwa kufanywa na Tume ya Katiba iliyokuwa iundwe 1964, lilifanywa [na kushindwa] mwaka 1977 na Tume ya Chama, kutokana na tabia iliyojengeka ya kuuona Muungano kama suala nyeti kiasi kwamba hakuna aliyethubutu kuhoji msingi halisi wa Muungano wakati wa kuandaa Katiba ya 1977.

Hata hivyo, tabia ya kuuona Muungano kama "patakatifu" kwa mtu kutotia miguu na viatu imepitwa na wakati kufuatia kuingia kwa mfumo wa vyama vingi. Tume ya Jaji Nyalali ililibaini hili na kutoa mapendekezo yake, lakini mengi yalitupiliwa mbali na Serikali kwa kugusa suala "nyeti" la Muungano.

Kwa mfano, Tume ya Nyalali ilipendekeza kuundwa kwa Tume ya kuandaa Katiba mpya ilivyoelekezwa katika Hati ya Muungano, kama njia pekee ya kurekebisha kasoro na kero ya Muungano. Serikali ilikataa pendekezo hilo na kero zinazidi kushamiri. Tutaendelea na migogoro ya Muungano hadi lini, kwa mwendo huu?

Wanaotetea mfumo wa Serikali mbili wa sasa hawaoni mbele, wala hawakumbuki tulikotoka. Si kweli kwamba, mambo yaliyoshinikiza Muungano miaka 47 iliyopita bado ni muhimu katika mazingira ya sasa na yajayo: Misisimko ya vita baridi imekwisha; njozi za Umoja wa Afrika za Kwame Nkrumah na Mwalimu Nyerere si mwongozo tena; wala mfumo wa demokrasia ya vyama vingi hauwezi kubeba furushi la mzoga wa chama kimoja kwa mazingira ya sasa.

Kutumika kwa vipengere vya Muungano visivyoeleweka ili kukidhi tu biashara ya kisiasa kwa wanasiasa, kumekatisha tamaa wengi na hakuwezi kuimarisha Muungano. Matumizi ya nguvu dhidi ya hoja na changamoto juu ya "utawala bora" ni ishara ya kulinda biashara hii.
Kwa mfano, tunapomfanya Rais wa Zanzibar kuwa Mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano maana yake nini? Kwamba naye anawajibika kwa Rais na kwa Bunge la Muungano kama walivyo mawaziri wote? Maamuzi ya Baraza la Mawaziri yanamhusuje kama Rais wa Zanzibar? Anayatekelezaje Zanzibar? Kama nani?

Rais wa Zanzibar anapotembelea Bara na kutenda shughuli za kiserikali, anafanya hivyo kama nani? Kama Rais wa Zanzibar au mgeni ziarani nchini "Tanzania" au kama Waziri?

Haya ni maswali magumu yanayotaka kupitiwa upya na ili kuelewa aina gani ya Muungano unaotakiwa. Na maadam Zanzibar haiko radhi kupoteza hadhi yake ndani ya Muungano [ingawaje Tanganyika imekubali kupoteza hadhi na jina lake], hatuwezi kukwepa kufikiria juu ya Muundo wa Shirikisho kama tunataka Muungano huu udumu.

Mazingira ya kisiasa ya sasa yanaruhusu mjadala juu ya jambo hili kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya Muungano, hususan enzi za wababe wawili, Marais Nyerere na Karume ambao hawakusikia la mtu. Wametuachia Katiba isiyokidhi matakwa ya Muungano na tabia ya nidhamu ya woga kwa maangamizi ya jamii.

Migogoro ya kisiasa ndani ya Muungano ni dalili tu za ugonjwa unaosumbua Muungano, wala si ugonjwa wenyewe. Hizi ni homa za mara kwa mara lakini ugonjwa mkuu umo ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, kwamba endapo tutaendelea kuuficha, kilio kitatuumbua muda si mrefu. Tumechoka kutibu homa za mara kwa mara; sasa ni wakati wa kutibu ugonjwa wenyewe kwa njia ya Katiba mpya.
 
Kitu kinacho ramble along bila paragraph wala vituo yani huwa kinaniumiza macho.

Jamani, darasa la tatu hamkufundishwa kutenganisha pointi?
 
Masuala yasio na majibu katika Muungano

Posted on April 22, 2011 by zanzibaryetu
Othman Masoud Othman ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar akiwasilisha mada katika Mkutano Maalum ulioandaliwa na Zanzibar Law Society siku ya kuadhimisha miaka 41 ya Muungano katika Hoteli ya Bwawani Zanzibar tarehe 23.4.2005 wakati huo Othman alikuwa ni Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP).

MASUALA YASIYO NA MAJIBU KATIKA MUUNGANO

[Mada imetayarishwa na Kuwasilishwa Katika Mkutano Maalum ulioandaliwa na Zanzibar Law Society Kuadhimisha Miaka 41 ya Muungano. Hoteli ya Bwawani Zanzibar tarehe 23.4.2005]

UTANGULIZI

Tokea kuasisiwa hapo tarehe 26 Aprili, 1964 Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ndio uliozaa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania umekuwa na sifa mbili kuu. Sifa moja ni ile ya kuwa nyenzo au kitambulisho cha umoja wa kitaifa Tanzania, na hivyo wale wanaojinadi kwa uzalendo na hisia za umoja wa kitaifa wamekuwa wakijinasibisha na kuupenda mno Muungano na kuahidi kuulinda kwa gharama zozote. Mapenzi haya ya Muungano yamepelekea hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuwa na kifungu mahsusi cha kuwataka Viongozi wa Kitaifa (Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamo wa Rais, Waziri Mkuu na Rais wa Zanziba) kula kiapo cha kuulinda Muungano kabla ya kuanza kazi zao (Kifungu cha Katiba ya Muungano). Aidha Sheria ya Vyama vya Siasa inakiondolea sifa ya kutosajiliwa chama chochote cha Siasa ambacho Katiba yake au sera zake ni za kutaka kuvunja Muungano. Hii ni kusema kwamba Katiba na Sheria zetu zinakataza wananchi kuwa na mawazo ya kuvunja Muungano. Huu ni ulinzi na mapenzi makubwa kwa Muungano.
Sifa ya pili ni kuwa Muungano umekuwa ni kitu kinachotambuliwa na kukubaliwa na wale ‘WANAOUPENDA’ na “WASIOUPENDA” kwamba una kasoro nyingi – lugha ya siku hizi huitwa KERO za MUUNGANO. Fedha, wataalamu na muda mwingi umetumika katika kutafuta suluhisho la Kasoro au Kero hizo, lakini mafanikio yamekuwa madogo mno (kama yapo). Kuna wanaosema kuwa Kasoro au Kero za Muungano zimekuwa zikiongezeka badala ya kupungua. Wanaosema hivyo mimi nawaunga mkono. Naamini yeyote atayetafakari

kwa makini atawaunga mkono. Hivyo, suala la msingi ni kwa nini kipenzi hiki cha Taifa la Jamhuri ya Muungano kinachoitwa MUUNGANO ambacho sote tunakubali kuwa kinaumwa tokea uchanga wake hadi leo, miaka 41 tokea kizaliwe, kimeshindwa kupatiwa dawa pamoja na Tanzania kuwa na mabingwa wa dawa za kisiasa na pamoja na juhudi kubwa za mabingwa hao bado MUUNGANO unaumwa zaidi. Wapo wanaodai kuwa dawa ipo na inajulikana lakini pengine inaonekana ni chungu sana kupewa kipenzi hicho cha Watanzania!!.

1.2 Ni maoni yangu kwamba MUUNGANO una kasoro za msingi za kimaumbile. Kasoro hizo ni miongoni mwa sababu za MUUNGANO kuwa na KERO sugu. Kasoro hizo za maumbile ni kuwepo kwa masuala ya msingi ya kikatiba ambayo hayana majibu ama kutoka ndani ya Katiba, Sheria, Sera na hata kutoka kwa watendaji.

1.3 Katika Waraka huu nitajaribu kueleza juhudi mbali mbali za kuondoa Kero za Muungano ambazo zimeshindwa kuondoa Kero hizo. Juhudi hizo na kushindwa kwake ni kielelezo cha kuwepo kwa kasoro za maumbile katika Muungano. Aidha nitaeleza baadhi ya Masuala yasiyo na Majibu katika Muungano. Maswali hayo ni kielelezo cha kasoro za maumbile na ni miongoni mwa sababu za kushindwa kupatiwa dawa KERO za Muungano. Kwa kuelewa mambo hayo mawili pengine itatusaidia sote kwa pamoja kutoa mapendekezo ya kusawazisha KERO za Muungano.

2.0 JUHUDI ZA KUONDOA KERO ZA MUUNGANO

2.1 Katika kutekeleza shughuli za Muungano matatizo kadhaa yamejitokeza ambayo yamepelekea kuwepo zinazoitwa Kero za Muungano.

Tatizo la siku za mwanzo kabisa la Muungano lilijitokeza mwaka 1965 wakati jambo jipya la Muungano lilipoongezwa katika orodha ya mambo ya Muungano; inaonyesha bila ya makubaliano baina ya Serikali hizi mbili. Mawasiliano yaliopo katika kumbukumbu baina ya Waziri wa Fedha wa Zanzibar na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Muungano yanaonyesha kuwa mawazo ya Serikali ya Zanzibar katika uundaji wa Benki Kuu hayakusikilizwa. Baada ya muelekeo wa kuwa na Shirikisho la Afrika Mashariki kufifia, nchi za Afrika Mashariki zikitanguliwa na Uganda zilichukua hatua za kuanzisha Benki Kuu zao hata kabla ya kuivunja rasmi Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki. Katika hali hiyo ndipo Serikali ya Muungano ilipochukua hatua za haraka za kuanzisha Benki Kuu ya Tanzania bila ya maafikiano rasmi na Zanzibar na hivyo kupelekea Zanzibar kukosa haki zake katika Bodi ya Sarafu na ndani ya Benki Kuu ya Tanzania.

Kutokana na hatua hiyo Rais wa Zanzibar Sheikh Abeid Amani Karumed aliunda Kamati ya watu 12 ikiongozwa na mtaalamu wa Masuala ya Benki Bw. E. Ebert ili kuishauri Serikali juu ya kuanzisha Benki ya Serikali ya Zanzibar. Kamati hiyo iliwasilisha ripoti yake mwishoni wa mwaka 1965. Ripoti hiyo pamoja na mambo mengine ilipendekeza kuwa Benki hiyo iwe ndio Benki ya Serikali na itumike kusimamia hesabu za (Accounts) Serikali. Kamati ilipendekeza hadi ifikapo July, 1966 ‘accounts’ zote za Serikali ziwe zimehamishiwa Benki hiyo. Hapo ndipo ilipoanzishwa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ambayo iliendelea kuwa ndio Benki ya SMZ hadi mwaka 2001 wakati Benki Kuu ya Tanzania ilipoanza rasmi kuwa Benki inayotumiwa na Serikali ya Zanzibar. Hivyo pamoja na kuwepo Benki Kuu kama chombo cha Muungano lakini kuanzia awamu ya kwanza hadi ya Tano za Serikali ya Zanzibar, haikutumia Benki hiyo. Serikali ya Muungano ilikuwa siku zote ikililalamikia jambo hilo.

2.2 Wakati wa Awamu ya Pili ya Serikali ya Zanzibar, matatizo ya Muungano yalijitokeza zaidi. Rais Aboud Jumbe alionekana dhahiri kutoridhishwa hata kidogo na mwenendo wa Muungano. Mbali ya kutafuta mtaalamu wa Sheria kutoka Ghana, Bw. Bashir Swanzi ili kujenga Hoja ya kukiukwa kwa Katiba ya Muungano na kupendekeza hatua za kisheria za kuondoa kasoro hizo, hatua iliyopelekea kuanguka kwake katika Uongozi, lakini yeye binafsi alichukizwa sana na mambo ya Muungano yanavyoendeshwa bila ya kufuata Katiba na ‘sprit’ ya Muungano. Katika moja ya mawasiliano yake ya kiserikali ya tarehe 23 Oktoba, 1983 aliwahi kuandika yafuatayo:
“Kosa moja ambalo linaendelea kufanywa ni lile la kudhani kwamba kuimarisha Muungano kuna maana moja na kuhaulisha shughuli zisizokuwa za Muungano ziwe za Muungano na kwamba Chama na Serikali ya Muungano wanaweza kufanya hivyo – bila ya kuzingatia Katiba wala hisia au matakwa ya Zanzibar.

Dhana hizo ni ama ni za kupotosha kusudi kwa sababu wanazozielewa wenyewe wafanyao hivyo, au ni kukataa kuelewa Katiba. Vyovyote vile ilivyo ni mashaka.
Kisheria shughuli yoyote isiyo ya Muungano haiwezi kufanywa iwe ya Muungano bila ya ridhaa ya Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika au na Serikali ya Muungano kwa niaba ya Tanzania Bara. Mpango wa Serikali ya Muungano kuwakilisha pia Tanzania Bara umeleta fadhaa na wasiwasi wa kutosha katika miaka kadhaa, hasa ya hivi karibuni.

Hata kingekuwa Chama au Serikali ya Muungano vingeweza Kikatiba kufanya hivyo, na haviwezi , basi lingelikuwa ni kosa la uadilifu na pia la kisiasa kufanya hivyo, bila ya ridhaa na makubaliano ya pande zote mbili za Muungano, wala hicho kisingekuwa kitendo cha kuimarisha, bali cha kudhoofisha na hata kupotosha dhamiri na maana ya Muungano.

Najua baadhi wana mashaka na kimya changu na wangependa kujua msimamo wangu juu ya suala hili la masahihisho ya Katiba. Msimamo haunihusu kwa sasa, jambo la msingi ni kwamba lazima Katiba ziheshimiwe, maadili yafatwe na dhamiri ya Muungano ihifadhiwe. Dhamiri lazima siku zote ibaki kuwa ni zao la nidhamu ya hali ya juu kabisa.

Muungano au Umoja hauwezi kuimarishwa kwa upande mmoja kutwaa madaraka ambayo ni ya pande mbili za umoja huo. Ikiwa wote tutatekeleza wajibu wetu kwa dhati, haki haitakuwa mbali kuonekana na kila upande utakuwa na utaridhika na haki yake. Huko ndiko kuimarisha Muungano”.
Hii ni ushahidi wa wazi kuwa pamoja na viongozi wakuu wa Muungano kuupenda Muungano lakini waliona kasoro za wazi za utekelezaji wa Muungano zaidi ya miaka 20 iliyopita.

2.3 Katika Awamu ya Tatu na Nne mbali ya mambo ya Muungano kuongezeka, juhudi za kusawazisha kasoro za Muungano ziliendelea. Njia kubwa iliyotumika ilikuwa ile ya vikao vya pamoja baina ya Serikali ya Muungano na Zanzibar. Vikao hivyo vikiongozwa na Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi.

2.4 Katika Awamu ya Tano, kama tutavyoona hapo baadae, Serikali ilichukua hatua nyingi zaidi kuliko awamu yoyote kushughulikia kasoro za Muungano. Dr. Salmin Amour hakuwa akificha hisia zake za kutoridhishwa na utekelezaji wa Muungano. Miongoni mwa mambo aliyoyawekea msimamo wazi wa kutaka kuwe na uwazi na masawazisho ni masuala ya uchumi, kupunguzwa mambo ya Muungano yasiyo ya lazima na suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kuna taaarifa za kuaminika kuwa wiki chache kabla ya kutiwa saini Mkataba wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Rais Salmin Amour alimuandikia Waraka maalum Rais Benjamin Mkapa, kueleza msimamo na mtazamo wa Zanzibar juu ya uwakilishi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Jambo ambalo nina hakika ni kuwa Waraka huo wa kurasa 10 wenye maoni na mtazamo wa Zanzibar haukushughulikiwa hadi leo!!

2.5 Awamu ya Sita ya Serikali ya Zanzibar inajulikana wazi kwa msimamo wake juu ya suala la uchimbaji wa mafuta – msimamo ambao iliurithi kutoka Awamu ya Tano. Mbali ya suala hilo, iliunda Kamati ya Wataalamu katika siku za mwanzo za kuingia madarakani. Kamati ilichambua kasoro za Muungano na kupendekeza mambo ya kubaki katika Muungano, mambo ya kupunguzwa, mambo ya kuongezwa na utaratibu wa kuendesha masuala ya Muungano kisera, kiutawala na katika kutunga Sheria za Muungano. Miongoni mwa mapendekezo mahsusi ya Kamati ilikuwa ni pamoja na kuwa Bunge la Tanzanzia liwe na sehemu mbili – ‘Lower house’ itayoshughulikia mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara na ambapo Wabunge wa Zanzibar hawatoshiriki na “Upper House” ambayo itashughulikia mambo ya Muungano tu na itakuwa na uwakilishi sawa baina ya Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha Kamati ilirudia mapendekezo ya Bomani ya kuwa na Baraza la Taifa (Council of State) ingawa kwa muundo tofauti. Baraza hilo kazi yake ni kushughulikia mambo ya Muungano kisera na kiutawala. Kamati iliwasilisha Ripoti yake Serikalini mwezi March, 2001. Kwa kadri ya ninavyoelewa hakuna hata moja katika mapendekezo ya Kamati, na ambayo yalikubaliwa na Serikali lililofanyiwa kazi. Eneo jengine lilofanyiwa kazi na Awamu ya Sita ni masuala ya fedha – Benki Kuu na Tume ya Pamoja ya Fedha.

2.6 Maelezo hayo yanathibitisha mambo mawili:-
(a) Muungano una kasoro za msingi
(b) Juhudi za kuondoa kasoro hizo zinazofanywa na viongozi wa SMZ hazijawa na mafanikio ya maana

JUHUDI MAHSUSI ZA SMT NA ZA SMZ

2.7 SMZ peke yake ama kwa kushirikiana na Serikali ya Muungano, zimechukua hatua kadhaa za kutafuta ufumbuzi wa Kero za Muungano. Kwa upande wa SMZ, miongoni mwa hatua ilizochukua na ambazo zinajulikana ni pamoja na kuunda Kamati mbali mbali. Miongoni mwa Kamati zilizoundwa na SMZ kushughulikia Kero za Muungano kati ya mwaka 1990 na 2003 ni pamoja na ziufatazo:

(a) Kamati ya Baraza la Mapinduzi (Kamati ya Amina) ya 1992.
(b) Kamati ya Rais ya Kupambanua na Kasoro za Muungano (Kamati ya Shamhuna, 1997).
(c) Kamati ya Rais Kuchambua Ripoti ya Kisanga (Kamati ya Salim Juma).
(d) Kamati ya Rais ya Kuandaa Mapendekezo ya SMZ juu ya Kero za Muungano. (Kamati ya Ramia, 2000).
(e) Kamati ya BLM juu ya Sera ya Mambo ya Nje.
(f) Kamati ya Rais ya Wataalamu juu ya Kero za Muungano (2001).
(g) Kamati ya BLM ya Jamuiya ya Afrika Mashariki.
(h) Kamati ya Mafuta
(i) Kamati ya Madeni baina ya SMZ na SMT.
(j) Kamati ya Suala la Exchusive Economic Zone (EEZ)
(k) Kamati ya Masuala ya Fedha na Benki Kuu.
(l) Kamati ya Rais ya Masuala ya Simu – (1996 – 1999)
SMZ pia imewahi kuajiri mtaalamu wa mambo ya fedha
Dr. Courtrey Blackman na Mtaalam wa masuala ya mafuta.

2.8 Mbali ya baadhi ya Kamati hizo za SMZ peke yake, SMT na SMZ zimeunda Tume, Kamati na Kuajiri Wataalamu mbali mbali ili kutafuta suluhisho la Kero mbali mbali za Muungano. Miongoni mwa Tume na Kamati hizo ni kama zifuatazo:

(a) Kamati ya Mtei
(b) Tume ya Nyalali
(c) Kamati ya Shellukindo
(d) Kamati ya Bomani
(e) Kamati ya Shellukindo 2, ya kuandaa Muafaka juu ya Mambo ya Muungano baina ya SMZ na SMT.
(f) Kamati ya Harmonisation.
(g) Kamati ya Masuala ya Simu (Kamati ya Kusila)

Aidha SMZ na SMT zimefanya vikao vya pamoja visivyopungua 80 katika ngazi mbali mbali ili kuzungumzia Kero za Muungano. Aidha Serikali hizi mbili mwaka 1994 ziliomba msaada wa IMF ili kuzishauri kuhusiana na Benki Kuu, mgawano wa Misaada na uhusiano wa kifedha (intergovernmental fiscal relationship).

2.9 Mbali ya juhudi zote hizo, tarehe 14 Novemba, 2000 wakati Rais Benjamin Mkapa alipokuwa akizundua Bunge aliahidi kuzipatia ufumbuzi Kero za Muungano ndani ya siku 60!! Tokea ahadi ilipotolewa hadi leo ni siku 1620 – yaani siku 60 zimepita mara 27.

2.10 Pamoja na hatua zote hizo zilizoambatana na masikitiko ya Viongozi wa juu, manung’uniko ya wananchi wa pande zote mbili juu ya uendeshaji wa Muungano na ahadi nzito za viongozi wa juu wa Serikali za kuondoa kasoro za Muungano – lakini bado Kero au Kasoro hizo zipo pale pale au zimezidi zaidi. Cha kusikitisha zaidi kuwa baadhi ya Kero zilizozungumzwa mwaka 1984 katika vikao vya pamoja ndizo Kero hizo hizo zilizozungumzwa katika Ripoti ya Shellukindo ya 1992 na katika Muafaka baina ya SMZ na SMT wa mwaka 1994 na ndizo hizo hizo zilizozungumzwa katika Ripoti ya Kamati ya Wataalamu ya SMZ ya 2001.

Suala muhimu ni kuwa ni kwa nini juhudi zote hizo zimeshindwa? Jibu langu ni kuwa Muungano una Kasoro za maumbile, za kuzaliwa nazo!!

2.11 Suala muhimu ni kuwa ni vipi tutaweza kuzibaini Kasoro hizo za Maumbile katika Muungano? Jibu ni kuwa baadhi ya kasoro hizo hazitaki utaalamu kuziona. Hata hivyo kwa sababu kasoro nyingi za Muungano ziko wazi na zimeshazungumzwa mara nyingi, wengi wamezizoea na kuona kwamba kasoro ni sehemu ya Muungano. Lakini tunaposogea mbele zaidi na kujiuliza ni kwa nini Kero za Msingi Muungano zimeshindwa kupatiwa ufumbuzi pamoja na juhudi na ahadi nzito za viongozi, nadhani jibu si kuwa Kero hizo zimezoeleka au kuwa ni sehemu ya Muungano. Tunapaswa tujiulize zaidi nini kiini cha tatizo. Wengi wana maoni kuwa kiini cha tatizo ni mfumo wa Serikali mbili. Ingawa mfumo huo kweli umechangia, lakini hilo bado ni jibu rahisi kwa suala zito (gumu) – “it is an oversimplified answer to a very complicated question”.

2.12 Kwa maoni yangu, tatizo la msingi ni kuwa kila uhusiano baina ya watu una Kanuni za msingi zinazoongoza uhusiano huo (“basic principles” au “grundnorm” za uhusiano). Aidha kuna mipaka ya uhusiano (parameters). Nyenzo za uhusiano kama vile nyaraka na sera lazima ziwe na uwezo wa kujibu maswali ya msingi kuhusiana na uhusiano huo.

2.13 Katika Muungano wa Tanzania, Zanzibar na Tanganyika ziliungana kwa baadhi ya mambo tu na sio mambo yote na ndio maana kuna orodha ya mambo ya Muungano. Aidha ibara ya 64 ya Katiba ya Muungano inaeleza wazi kuwa Bunge halina mamlaka ya Kutunga Sheria kwa mambo ya Zanzibar yasiyokuwa ya Muungano. Hivyo ilitarajiwa kwamba, kwa vile pande hizi zimeungana kwa baadhi ya mambo tu Kanuni ya msingi ni kuwa pande hizo lazima ziwe na kauli sawa kuhusiana na Mambo ya Muungano katika Sera, Utawala na katika kuyatungia Sheria. Aidha ziwe na kauli sawa katika kuongeza na kupunguza mambo ya Muungano na Katiba iweke bayana jambo hilo.

Katika Muungano wa Kikatiba au wa kisiasa, Katiba au Mkataba wa Muungano, Sheria na Sera za Muungano ndio nyenzo kuu. Iwapo nyenzo hizo zinashindwa kutoa majibu kwa masuala ya msingi kuhusiana na Muungano ni kielelezo tosha kuwa Muungano huo una kasoro za maumbile. Kasoro hizo ni pamoja na kutokuwa na Kanuni za Msingi na kutokuwepo Mipaka katika Waraka huu tutaeleza Masuali ya Msingi ambayo hayana Majibu katika Katiba, Sheria na Sera za Muungano.

3.0 MASUALA YASIYO NA MAJIBU

3.1 SUALI LA KWANZA: JE WASHIRIKI WA MUUNGANO BADO WAPO AU HAWAPO?

3.1.1 Suala hili ni la msingi kwa vile nchi ambazo zimeungana kwa baadhi ya mambo tu, inategemewa kwamba waliounganisha mambo hayo wapo, wana vikao rasmi vinavyotambuliwa na Katiba na Sheria za Nchi. Ilitegemea kuwa Washirika hao wanaamua kuongeza kupunguza mambo ya Muungano wakiwa na nguvu sawa ya uamuzi. Ilitegemea kuwa Washirika hao wana kauli sawa za maamuzi juu sera, uendeshaji na Sheria za Muungano. Suala ni kuwa hivi ndivyo hali ilivyo?

3.1.2 Suala hili kila mtu anaweza kuwa na maoni na fikra zake, lakini sio jibu na wala huwezi kupata jibu ndani ya Katiba, Sheria na Sera za Muungano. Sababu zinazoonyesha kuwa hakuna jibu la suali hili ni zifuatazo:

(a) Wengi wanadhani kuwa Zanzibar ipo na ni Tanganyika tu ndio haipo – lakini ukweli Zanzibar haipo katika Muungano. Wengine wanahisi Tanganyika ipo ndani ya Muungano ikivaa koti la Muungano lakini hata hilo haliko wazi kama iliomo ndani ya Muungano ni Tanganyika au nalo ni koti tu la Tanganyika.

(b) Hakuna Kikao kinachotambulika kisheria kinachozikutanisha pande mbili za Muungano.

(c) Mambo ya Muungano kiutawala na kisera yanaamuliwa na Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano. Zanzibar haiwakilishwi ndani ya Baraza hilo. Rais wa Zanzibar anaingia kama Mjumbe wa Baraza la Mawaziri na sio kama upande mmoja wa chombo hicho ambao unaruhusiwa kutetea msimamo wa Zanzibar. Hivyo ndani ya Baraza Rais wa Zanzibar haiwakilishi Zanzibar kwa vile akiwa ndani ya Baraza hilo anawajibika kwa Rais wa Muungano na sio kwa mamlaka yoyote ya Zanzibar. Mawaziri ambao ni Wazanzibari nao hawawakilishi Zanzibar bali ni Mawaziri sawa na wengine ambao wanafungwa na Kanuni ya kuwajibika kwa pamoja (Collective responsibility). Hivyo lazima wakubaliane na maamuzi ya wengi na kwa vyovyote vile hawamo ndani ya Baraza kuiwakilisha Zanzibar.

(d) Inapotokea Rais wa Muungano au Makamo wa Rais anatoka Zanzibar – jee anaiwakilisha Zanzibar. Ameteuliwa na Zanzibar kama mshirika wa Muungano kuiwakilisha? Anayo haki na uwezo wa kisheria wa kutetea maslahi ya mmoja wa Washiriki ndani ya Muungano ambayo ni Zanzibar. Jibu ni kuwa Makamo wa Rais wala Rais anapotokea kutoka Zanzibar haiwakilishi Zanzibar ndani ya Muungano bali anatumia fursa yake kama Mtanzania kushika nafasi hiyo. Hapaswi na hana uwezo wala wajibu wa kutetea Zanzibar ndani ya Muungano.

(e) Katika kutunga Sheria za Muungano Zanzibar kama mshirika inawakilishwa? Takribani Sheria zote za mambo ya Muungano zinapitishwa kwa wingi wa Kura. Kwa vile idadi ya wabunge kutoka Zanzibar takriban ni robo tu ya Wabunge wa Bunge la Muungano ni wazi kuwa Zanzibar kupitia Wabunge hao haina kauli katika kutunga Sheria za Muungano. Ni mambo yale tu yaliyoainishwa katika Orodha ya Pili ya Jadweli ya Pili ya Katiba ya Muungano ndio yanayoamuliwa kwa kauli sawa. Kichekesho ni kuwa kati ya mambo hayo 8 yaliyoorodheshwa baadhi sio mambo ya Muungano.

(f) Inapotokea Zanzibar kushirikishwa kama Zanzibar katika masuala ya Muungano ni kwa njia ya SMZ kutakiwa kutoa maoni. Hata hivyo, maoni hayo ya SMZ ambayo baadhi ya wakati huandaliwa na Baraza la Mapinduzi, mara nyingi hukataliwa na hata Mkurugenzi tu wa Serikali ya Muungano au Katibu Mkuu au Waziri. Baadhi ya mifano mashuhuri ambapo maoni ya Zanzibar hayakuzingatiwa katika masuala muhimu ya Muungano ni:

(i) Katika uanzishaji wa Benki Kuu, mwaka 1965 na marekebisho ya Benki Kuu, 1995.
(ii) Uanzinshwaji wa Mamlaka ya Mapato TRA.
(iii) Katika suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
(iv) Sera ya Mambo ya Nje
(v) Uraia na Uhamiaji na
(vi) Sheria ya Deep Sea Fishing Authority.
(g) Kwa upande wa pili, ingawa tunasema kuwa Tanganyika imevaa koti la Muungano lakini suala bado linabaki, kuwa Tanganyika (T/Bara) kama mshirika wa Muungano ipo. Jee Serikali ya Muungano kweli inawakilishwa na kutetea maslahi ya Tanganyika ndani ya Muungano na kwa utaratibu gani?

3.2 NINI MAANA YA JAMBO LA MUUNGANO

3.2.1 Suala hili lina sehemu mbili zifuatazo:

(a) Mambo ya Muungano ni mangapi; na
(b) Jambo linapoitwa ni la Muungano maana yake ni nini.
Mambo ya Muungano ni Mangapi:

3.2.2 Jibu rahisi kwa watu wengi kuhusiana na suala hili ni kuwa mambo ya Muungano ni 22 kama yalivyoainishwa na Katiba ya Muungano katika Jadweli la Kwanza. Lakini hata Jadweli hilo limeorodhesha zaidi ya mambo 22 kama ifuatavyo:

(i) Katiba ya Muungano
(ii) Mambo ya nje
(iii) Ulinzi
(iv) Usalama
(v) Polisi
(vi) Hali ya Hatari
(vii) Uraia
(viii) Uhamiaji
(ix) Mikopo ya Nje
(x) Biashara
(xi) Utumishi katika Serikali ya Muungano
(xii) Kodi ya Mapato
(xiii) Forodha (Ushuru)
(xiv) Kodi ya Bidhaa (exercise)
(xv) Bandari
(xvi) Usafirishaji wa Anga
(xvii) Posta
(xviii) Simu
(xix) Sarafu
(xx) Mabenki
(xxi) Fedha za Kigeni
(xxii) Leseni za Viwanda
(xxiii) Takwimu
(xxiv) Elimu ya Juu
(xxv) Mafuta yasiyosafishwa
(xxvi) Gesi asilia
(xxvii) Baraza la Mitihani
(xxviii) Usafiri wa Anga
(xxix) Utafiti
(xxx) Mahkama ya Rufaa
(xxxi) Usajili na Shughuli za Vyama vya Siasa

3.2.3 Pamoja na Orodha hiyo jadweli ya Pili, Orodha ya Pili inaeleza kwamba, Bunge lilipotaka kubadili masuala yanayohusiana na Mamlaka ya Serikali ya Zanzibar na suala la Mahkama Kuu ya Zanzibar – lazima yakubaliwe na theluthi mbili ya Wabunge wa Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wabunge wa Zanzibar. Suala hapa ni kuwa kwani hayo ni mambo ya Muungano?

3.2.4 Dalili ya pili inaonyesha kwamba Mambo ya Muungano hayajulikani ni mangapi ni kuwa yapo mambo yanayofanywa kimuungano pamoja na kwamba si ya Muungano (kama vile Bima – inayosimamiwa na Kamishna ya Bima). Aidha yapo mambo ya Muungano ambayo hayasimamiwi kimuungano kama vile Takwimu (isipokuwa sensa ya Idadi Watu), Bandari na Leseni za Viwanda.

3.2.5 Dalili ya tatu ni kuwa Bunge limekuwa likitunga Sheria na kuzifanya za Muungano hata kwa mambo ambayo hayamo katika orodha ya Muungano. Mfano ni Sheria ya Proceeds of Crimes Act ya 1991.

3.2.6 Dalili ya nne ni kuwa kuna baadhi ya maeneo ambayo Serikali zenyewe (pamoja na Wanasheria Wakuu) hazikubaliani kama ni ya Muungano au si ya Muungano. Maeneo hayo ni kama vile “Deep Sea Fishing Authority”, na Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora. Aidha suala la Ushirikiano wa Kimataifa.

3.2.7 Dalili ya Tano ni kuwa hata kwa yale mambo ambayo yamo katika Orodha ya Mambo ya Muungano, mengi hayana tafsiri na hivyo hayajulikani mipaka yake. Mifano ni kama vile Elimu ya Juu (inaanzia wapi inaishia wapi?), Usalama (Jee ni ule wa hata kuweka “watchman”) jee Serikali ya Zanzibar haina siri zake peke yake ambazo hazipaswi kujulikana na Serikali ya Muungano na hivyo kuwa na taratibu zake za usalama? Mikopo ya Nje, Biashara za Nje. Posta na Simu jee ni miundo mbinu au udhibiti (regulatory aspect).

3.2.8 Dalili au hoja ya Sita ni kuwa jee mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara pekee nayo ni ya Muungano au si ya Muungano. Hili linaonekana kama suali la kijinga mno, lakini ndio suali gumu hata kwa wanaojiona werevu mno. Hakuna ubishi kuwa jambo lisipokuwa la Muungano Zanzibar inaweza kulisimamia wenyewe, lakini kuna matatizo kwa upande wa Tanzania Bara.

3.2.9 Baadhi ni kama yafuatayo:

(i) Bajeti: Zipo baadhi ya Taasisi za Muungano ambazo zinafanya kazi za Muungano na sizizo za Muungano – kwa mfano Bunge linatunga Sheria na kusimamia mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano. Vivyo hivyo kwa ‘Executive’ na Judiciary ya Muungano. Hivi gharama zake zitoke wapi. Kwa sasa Bunge na Executive inajulikana kuwa ni za Muungano, hivyo igharamiwe na Mfuko wa Muungano?

(ii) Taasisi zisizo za Muungano ndizo zinazoiwakilisha Zanzibar nje kwa jina la Tanzania mfano Kilimo, Kazi, Utalii na hata Tanzania Football Federation. Hivyo suala linakuja ni wakati gani taasisi ya Tanzania Bara isiyokuwa ya Muungano inakuwa sio ya Muungano?

3.2.10 Majibu ya maswali yote hayo hayamo katika Katiba wala Sheria zetu wakati ni mambo ya msingi na ndio uti wa mgongo wa Muungano.
Jambo linapoitwa la Muungano Maana yake Nini.

3.2.11 Jibu la rahisi ni kuwa jambo linapoitwa la Muungano ni kuwa Zanzibar haina uwezo wa kulisimamia kisera, kiutawala na kisheria. Hata hivyo suala hili ni gumu kuliko linavyoonekana. Kabla ya kuja sera za biashara Huria mashirika kama vile Air Tanzania, Shirika la Posta na Simu na Benki ya Taifa ya Biashara n.k yakijulikana kama mashirika ya Muungano. Katika vikao kadhaa ilikubaliwa kuwa Zanzibar ishirikishwe katika uendeshaji wa mashirika hayo ya Muungano. Mashirika hayo mengi yamebinafsishwa.

3.2.12 Hisa za mashirika ama zinamilikiwa na HAZINA ya Serikali ya Muungano ama zimeuzwa kwa ‘Strategic Investors” au hata kwa wananchi. Zanzibar haikupewa hisa. Kuna hoja kwamba zile hisa za Serikali ya Muungano ndio pia za Zanzibar. Hoja hii haina uzito kwani katika Muafaka baina SMT na SMZ ilikubaliwa kuwa suala hilo lizungumzwe upya baina ya Serikali mbili (Uk. 46, dondoo la 18.4.3 la Muafaka). Kwa kadri ya ninavyofahamu suala hilo halijazungumzwa tena na Zanzibar imekosa haki zote katika mashirika hayo yaliyokuwa ya Muungano. Tatizo kama hilo lilijitokeza katika Benki Kuu. SMZ ilipodai kuwa na hisa ambazo ilizilipia kupitia Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, Zanzibar ilielezwa na SMT kuwa haiwezi kuwa na hisa katika Benki Kuu lakini inaweza kupewa mafao kwa kima cha asilimia 4.5.
3.2.13 Kwa upande wa pili, taasisi ambazo ni za Muungano kama vile TRA, TPDC, TCRA, TCAA, n.k zinaonekena ni za Muungano katika ngazi ya Bodi ya Wakurugenzi. Hata hivyo katika ajira vigezo vinavyotumika ni vya Tanzania Bara. Kwa mfano anayeomba kuajiriwa katika Taasisi hizo kama Mwanasheria, lazima awe ni Wakili wa Mahkama Kuu ya Tanzania (Bara) ingawa Mahkama Kuu ya Zanzibar na Tanzania (Bara) zina mamlaka sawa, lakini kuwa wakili wa Mahkama Kuu, Zanzibar hakutambuliwi. Aidha Makao Makuu ya taasisi zote hizo yapo upande mmoja wa Muungano. Mashirika haya sio tu kuwa yanatoa fursa za ajira lakini yanatumia fedha nyingi sana kufundisha wafanyakazi wake kuliko fedha zinazotumiwa na bajeti ya SMZ kufundisha watumishi wake. Hivyo kama taasisi hizo ni za Muungano kwa nini Mshirika mmoja asifaidike na fursa hizo?
Maelezo haya yanaweka bayana suala ambalo
halijapatiwa jibu la nini maana ya jambo la
Muungano?

3.3 NINI MAANA YA MTU ANAYETOKA ZANZIBAR/TANZANIA BARA.

3.3.1 Moja kati ya zilizokuwa nguzo kuu za Muungano ni ile ya uwakilishi wa Zanzibar ndani ya Muungano kupitia Rais wa Zanzibar ambaye alikuwa Makamo wa Rais wa Muungano kwa kupitia wadhifa wake wa Urais wa Zanzibar. Baada ya Marekebisho ya 11 ya Katiba Rais wa Zanzibar aliondolewa katika nafasi ya Makamo wa Rais kwa kupitia wadhifa wake. Badala yake Makamo wa Rais anapatikana na utaratibu wa Mgombea Mwenza. Chini ya ibara ya 47(3) ya Katiba ya Muungano, Mgombea Mwenza anateuliwa kwa Kanuni kuwa iwapo Rais ni mtu anayetoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, Makamo wa Rais awe ni mtu anayetoka upande wa pili wa Muungano.

3.3.2 Suala ni kuwa mtu anayetoka upande mmoja wa Muungano ni sifa ya uzawa, ukaazi au ya mahusiano? Mtu anaweza, kwa mfano kutoka Zanzibar kwa sababu ya kuzaliwa ama kwa sababu ameishi Zanzibar au kwa sababu wazazi au mmoja wa wazazi wake ametoka Zanzibar lakini yeye mwenyewe hajazaliwa wala hajawahi kuishi Zanzibar.

3.3.3 Nafasi ya Urais (iwe Rais au Makamo) ni muhimu katika Muungano, Ni moja ya nguzo zake kuu. Aidha Katiba ndio muongozo wa uteuzi wake. Hivi sasa kuna madai kuwa hakuna utaratibu wa kubadilishana zamu za Urais baina ya Bara na Zanzibar kwa vile haijaelezwa ndani ya Katiba wala Sheria yoyote. Kutokana na utaratibu uliopo (angalau ndani ya CCM) ya uteuzi wa mgombea Urais, tunaanza kuandika Kanuni kuwa Zanzibar itaendelea kutoa Makamo wa Rais. Lakini kwa vile maana ya mtu anyetoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano hajafafanuliwa ndani ya Katiba, kesho itakuja Hoja kuwa neno hilo halikutafsiriwa ndani ya Katiba wala Sheria, hivyo sifa moja yoyote ya uzawa, ukaazi au uhusiano inafaa. Sijui kama kuanzia hapo patakuwa tena na Muungano huu tunaoujua leo. Njia rahisi ilikuwa ni kusema kwamba mtu anayetoka Zanzibar ni yule ambaye ana sifa ya kuwa Mzanzibari chini ya Sheria za Zanzibar.

3.3.4 Serikali ya Muungano ilikataa wazo hilo kata kata wakati wa kujadili Muafaka baina ya SMZ na SMT hapo mwaka 1994. Kamati ya Shellukindo iliwahi hata kupendekeza Sheria ya Mzanzibar ifutwe kwa vile inatoa dhana ya uraia wa aina mbili (Angalia uk. 10 – Dondoo 2.6 la Ripoti ya Shellukindo). Serikali ya Muungano hata hivyo katika muafaka wa 1994 ilikubali kuwa kuifuta Sheria hiyo ni makosa, na hivyo iendelee kuwepo kwa vile ndiyo inayofafanua nani ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika uchaguzi wa Zanzibar. (Angalia uk. 10 – Dondoo 2.2.2.1 ya Taarifa ya Muafaka).
Hivyo suala hili muhimu halina majibu ndani ya Katiba na Sheria zetu na ni wazi kuwa ni mbegu ya mzozo wa baadae.

3.4 JEE TANZANIA INA UCHUMI MMOJA AU CHUMI MBILI

3.4.1 Ingawa katika Kitabu cha Muafaka baina ya SMT na SMZ inaeleza kuwa “Tanzania ni nchi moja yenye uchumi mmoja wenye mazingira tofauti” lakini katika utekelezaji Serikali zote mbili zinaonyesha kuwa na jibu tofauti – kwamba uchumi wa Tanzania Bara na Zanzibar ni tofauti. Hata katika hali halisi ndivyo ilivyo. Mtafaruku uliopo unatokana na ukweli kwamba ingawa chumi ni mbili lakini nyenzo zote kuu za uchumi zinadhibitiwa na Serikali ya Muungano. Nyenzo kama vile udhibiti wa sera za fedha, kodi na mahusiano na nchi za nje hazimo mikononi mwa Zanzibar ingawa Zanzibar inategemea ijiendeshe kiuchumi.
Dalili au sababu zinazoonyesha wazi kuwa Tanzania ina chumi mbili ni pamoja na zifuatazo:

(i) Masuala ya Maendeleo ya Uchumi sio ya Muungano; hivyo kila upande una Wizara yake inayoshughulikia uchumi, mipango na sera zake za uchumi na bajeti yake.
(ii) Kila upande una Mfuko wake Mkuu wa Serikali na hivyo mapato yake.
(iii) Kila upande una jukumu la kushughulikia huduma za jamii, miundo mbinu n.k.
(iv) Kila upande una Sera na Sheria zake za biashara na uwekezaji na hata Sheria za ajira.

Pamoja na ukweli huo Katiba ya Muungano haiweki bayana na ndio inayofanya kusiwe na majibu ya wazi ya suala hili kwa sababu zifuatazo:

(i) Kodi ya Mapato, Mikopo ya nje na Biashara za Nje bado yamefanywa ni mambo ya Muungano. Kodi ya Mapato ambayo ni nyenzo kuu ya uchumi wa visiwa ambao ni “Service oriented” badala ya kuwa “resource based” kama ilivyo kwa Bara, bado ni jambo la Muungano kisera, ingawa mapato halisi yanatumika Zanzibar.
(ii) Sera za fedha na mahusiano ya kikanda yapo chini ya Serikali ya Muungano bila ya kuwa na uwazi wala Sheria inayoilazimisha kushughulikia maslahi ya kiuchumi ya Zanzibar.

3.4.2 Kutokana na kutokuwepo majibu ya wazi na pia kuwepo mtafaruku ya lipi hasa ndio sahihi, ndio maana Kero za Muungano zinaonekana kuzidi badala ya kupungua kwani maisha ya watu hasa wa Zanzibar yamedidimia kutokana na uchumi wa Zanzibar kuanguka kutokana na zao la karafuu kushuka bei. Mategemeo pekee ya kiuchumi au uwekezaji katika nyanja zote hasa za huduma. Hata hivyo Zanzibar haiwezi kuweka sera huru na za kuvutia za kiuchumi kuliko Tanzania Bara kwa vile haina mamlaka katika eneo hilo. Mfano mzuri ni kushindwa kwa miradi ya EP2, Bandari Huru na Off-Share Companies.

4.0 HITIMISHO

4.1 Muungano wetu hautalindwa kwa siasa na kuusifu pekee na kuwaita wale wanaoukosoa kuwa ni maadui wa Muungano ingawa wapenzi wa Muungano wenyewe wanazikubali kasoro hizo hizo na hata wameziandika na kuzifanyia vikao. Muungano utalindwa kwa kuwekewa misingi madhubuti iliyo wazi na ambayo italindwa kwa misingi ya Katiba na Sheria inayokubalika na ambayo itatokana na ridhaa za washirika wa Muungano.

4.2 Mifano ipo mingi. Muungano wa Uingereza (England) na Scotland ingawa ulianzia mwaka 1603 lakini ulijadiliwa rasmi mwaka 1705 na kuanzishwa rasmi kisheria mwaka 1707. Hata hivyo miaka ya 1990 imeshuhudia ukizungumzwa tena na kuafikiwa kurejeshwa kwa Bunge la ndani la Scotland. Aidha, kwa upande mwengine, ingawa Uingereza iliungana rasmi na Ireland mwaka 1800 kwa Sheria ya “Union of Great Britan and Ireland” lakini kwa kukosekana misingi madhubuti mwaka 1922 majimbo 26 yalijitoa katika Muungano na kuanzisha Irish Free State ambayo sasa ni Ireland. Mfano mwengine, ambao pengine si mzuri ni ule wa Canada na Uingereza. Ingawa Canada ilipewa hadhi ya kuwa Dominion kupitia Sheria ya British North America Act ya 1867 lakini bado kulikuwa na matatizo mengi ambayo yalifanyiwa kazi ambako kulipelekea kutungwa Sheria ya kuweka bayana masuala yenye mzozo kwa Sheria ya Statute ya Westminster ya 1931.

4.3 Hali ni tofauti katika Muungano wa Tanzania ambapo marekebisho mengi ya kikatiba, kishera na kisera yanafanya Muungano kuwa na matatizo zaidi kwa vile kiini cha Kero za Muungano hakijashughulikiwa. Masuala ambayo hayana majibu ni mengi ndani ya Muungano.

4.4 Niliyoyaeleza ni mifano tu ya masuala hayo mengi. Kinachojidhihirisha ni kuwa tatizo sio la idadi ya Serikali tu lakini ni zaidi ya hapo. Tatizo la msingi ni lile la Kanuni za msingi za Muungano kutozingatiwa na kutopatiwa majibu. Kutokana na Kasoro hizo ndio maana Muungano wetu kama ulivyo hivi sasa hauwezi kuhimili mabadiliko ya kisiasa.

4.5 Hakuna Muungano madhubuti ambao unategemea kulindwa na sera za chama. Muungano madhubuti ni ule unaolindwa na misingi madhubuti, uwazi na wenye majibu kwa masuali yanayohusu nguzo kuu za Muungano huo.
 
Lwaitama anajadili juu ya muungano kwa kuwarushia makombora viongozi wa serikali na chama tawala kuwa ni wabinafsi hawataki kusema ukweli juu ya muungano
 
Dk.Lwaitama,Mtatiro,mzee Mbawala na masako wanajadili kama muungano umeenziwa kwa miaka 47 na upande gani umenufaika sana..
 
asante kwa taarifa, sasa huyu bi mkubwa sijui atamaliza saa ngapi kuangalia hii movie yake, jamani ndo kazi!
 
Nice debate. Dk Lwaitama katoa mfano wa United Kingdom, kwamba Scotland, Wales na Ireland zina serikali zake lakini hakuna serikali tofauti ya
England. Kwa mfano huu anasema hakuna sababu ya kuwa na serikali ya Tanganyika na kuwamwagia maji wale wanaoitisha serikali tatu. Serikali ya Tanganyika imo ndani ya serikali ya mwungano kwani rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni rais wa Tanganyika. Nice debate.
 
Hawa jamaa wa leo wote wanasema muungano ni muhimu, na kelele za kuvunja muungano sinasababishwa na ubinafsi wa viongozi
 
Back
Top Bottom