Wanafunzi vijana kutoka kote Cape Town, nchini Afrika Kusini, walileta nguvu na shauku kubwa katika sherehe ya utamaduni wa Kichina siku ya Jumamosi, wakati Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Cape Town (CIUCT) ilipoandaa Shindano lake la tano la Kuimba kwa Kichina, ikiangazia wazo kwamba muziki unaweza kutumika kama daraja kati ya tamaduni.
Kama tukio maalum la kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kichina mwaka huu, shindano hilo lilifanyika katika Shule ya Sekondari ya Groote Schuur, chini ya mada "iSing" na liliandaliwa kwa ushirikiano na shule na Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Stellenbosch. Washiriki kutoka vyuo vikuu, shule za sekondari, na shule za msingi walishindana katika vitengo viwili: kundi la chuo kikuu na kundi la pamoja la shule za msingi na sekondari.
Naibu Balozi wa China huko Cape Town, Wang Xiao, katika hotuba yake ya ufunguzi wa tukio hilo, alibainisha mizizi ya kitamaduni iliyo ndani ya lugha ya Kichina. "Kama moja ya lugha kongwe zaidi duniani, Kichina kina umri wa maelfu ya miaka na kinazungumzwa kote duniani," alisema.
"Nyimbo za Kichina, kama njia ya kitamaduni inayovutia sana, sio tu kwamba zinawasaidia wanafunzi kuboresha ustadi wao wa Kichina, lakini pia zinawawezesha kupata uzoefu wa kina wa utamaduni wa Kichina kupitia melodi na mashairi," alisema Wang.
"Tunatarajia kuona marafiki wengi zaidi wa Afrika Kusini wakijifunza Kichina, jambo ambalo litawafungulia mlango wa kuingia kwenye China ya kisasa na ustaarabu wa China," aliongeza.
Katika shindano lote, washindani wenye viwango tofauti vya ustadi wa Kichina na uzoefu wa kujifunza walifanya maonesho wakijiamini na kuwa na shauku kubwa, huku wakipigiwa makofi na kushangiliwa na watazamaji. Maonesho yao yalianzia nyimbo za kitamaduni kama vile "Mti wa Mzeituni" na "Kengele ya Jioni Inapolia kwenye Vilima vya Nanping" hadi nyimbo za kisasa zaidi kama vile "Kauri ya Bluu kwa Weupe" na "Shujaa Mpweke."
Onesho la wimbo wa watoto "Little Bugs Flying" wa kundi la wanafunzi wa shule ya msingi ya huko uliwika kama moja ya wimbo mzuri kwenye tukio hilo, ukiwafanya watazamaji wengi kuwapigia makofi na kuimba pamoja.
Mwishowe, waimbaji wawili walioimba pamoja kutoka Chuo Kikuu cha Cape Town, Arielle Denis na Hannah Engel, walipata tuzo ya mshindi kwanza katika kitengo cha chuo kikuu kwa utumbuizaji wao murua wa wimbo wa "Free," huku Chazz Hendricks kutoka Shule ya Msingi ya Floreat akishinda tuzo ya juu katika kitengo cha shule za msingi na sekondari kwa wimbo wake "The Snail and the Oriole."
Denis na Engel waliiambia Xinhua kwamba wote walianza kujifunza Kichina wakiwa Darasa la 8 na wamepata marafiki wengi wapya njiani.
Waliongeza kuwa katika siku zijazo wanatumai kutafuta kazi ya kutafsiri ya kimataifa au sheria, wakibainisha kuwa kujifunza Kichina na kuimba nyimbo za Kichina sio tu kwamba kunaongeza uelewa wao wa utamaduni wa Kichina bali pia kunanufaisha matarajio yao ya baadaye ya kazi.
"Kujifunza Kichina ili kuwasaidia watu, kujifunza lugha wanayozungumza -- nadhani hiyo itakuwa na manufaa sana kunisaidia katika siku zangu zijazo," Engel alisema.
Baada ya tukio hilo, Danie Visser, mkurugenzi wa Ofisi ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Cape Town na mkurugenzi wa mambo ya nje wa CIUCT, aliiambia Xinhua kwamba muziki hutumika kama daraja kati ya tamaduni tofauti, na kwamba katika muktadha wa Mwaka wa Mawasiliano ya Watu na Watu kati ya China na Afrika wa 2026, shughuli za kitamaduni kama vile mashindano ya kuimba ya Kichina zina jukumu muhimu katika kujenga uhusiano kama huo.
"Bila shaka mtu hawezi kujenga daraja kwa kulifikiria tu. Lazima uchukue hatua ndio ulijenge, kwa hivyo matukio kama haya, kila moja ni tofali kwenye daraja," Visser alisema.
Pia alibainisha kuwa kwa nguvu inayoongezeka ya China na uhusiano unaoongezeka kati ya China na Afrika, ushawishi wa lugha ya Kichina unapanuka. Alisema anatarajia kuwa shule nyingi zaidi za Afrika Kusini zitajumuisha Kichina katika mitaala yao, na kuwasaidia wanafunzi kukuza ujuzi wa lugha tangu wakiwa na umri mdogo.
"Sasa, Kichina ni lugha inayokua, nan i lugha ya kimataifa," alisema. "Nadhani wakati mzuri wa kujifunza Kichina, ni sasa."