2nd December 2010
B-pepe
Chapa
Maoni
Agusia pia Tume Huru ya Uchaguzi
Limo la madaraka makubwa ya Rais
Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani
Serikali imewataka wadau mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa kuwasilisha mapendekezo maalum kwake kama wanataka kuwepo Tume Huru ya Uchaguzi badala ya kulalamika mitaani.
Kadhalika, Serikali imesema suala la mgombea binafsi limekabidhiwa kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba ndiye atakayeamua kuitisha mjadala miongoni mwa wabunge na kisha kulitolea uamuzi.
Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, alitoa msimamo huo wa Serikali jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na NIPASHE katika mahojiano maalum ofisini kwake.
Kombani alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku yake ya tatu akiwa ofisini baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo na Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa wiki.
Hata hivyo, alisema hajui tume huru inayoombwa na wanasiasa inatakiwa iweje na watumishi wake wagharimiwe na nani, ingawa alisisitiza kwamba ikiwa atapokea mapendekezo hayo atayafanyia kazi.
"Mimi nasikia kwenye magazeti na kwa kuwa mimi ni mtawala, siwezi kuyafanyia kazi mambo ya mtaani, lazima hao wanaoitaka tume huru walete mapendekezo yao kwangu na mimi nitakaa na kuyachambua," alisema. Alisema wapinzani waandae na kuwasilisha mapendekezo hayo, lakini mwisho wa siku watumishi wa tume huru wanayoitaka watapaswa kuwajibika kwa serikali kwa kuwa ndio itakayowalipa na kuwagharimia kila kitu.
Kuhusu kuajiri watumishi walio nje ya serikali kwa ajili ya kusimamia uchaguzi badala ya kutumia wakurugenzi wa halmashauri na maofisa watendaji wa kata, Waziri Kombani alisema suala hilo halitawezekana.
Alitoa mfano kuwa mwaka 1995 Serikali iliajiri watu kutoka nje ya Serikali kwa ajili ya kusimamia Uchaguzi Mkuu, lakini badala ya kufanya kazi hiyo vizuri, waliishia kukimbia na masanduku ya kura.
Alifafanua kwamba watu hao waliamua kukimbia na masanduku ya kura kwa kuwa walikuwa hawawajibiki kwa Serikali kama ilivyo kwa wakurugenzi wake inaowatumia mara zote kufanya kazi hiyo.
Alidai kuwa vyama vya upinzani ndivyo vinavyotaka Tume Huru na sio Chama Cha Mapinduzi (CCM) wala wananchi, lakini akasema suala hilo linazungumzika ikiwa upande unaolalamika utawasilisha mapendekezo rasmi.
"Mara utamsikia Tundu Lissu anazungumza kwenye vyombo vya habari, lakini Serikali haijapokea mapendekezo yao ili kujua nini wanachokitaka kifanyike ama kirekebishwe," alisema.
Alisema watu wanaotaka Tume Huru wasikate tamaa na kuangalia historia ya huko nyuma katika utawala wa Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, na kipindi cha kwanza cha Rais Jakaya Kikwete ambapo labda waliwahi kuwasilisha mapendekezo yao, lakini hayakufanyiwa kazi.
"Atafutaye hachoki wala hakati tamaa," alisema. Alipoulizwa kuhusu madai yanayotolewa na makundi mbalimbali ya jamii kutaka kutungwa kwa katiba mpya, Waziri Kombani alisema kuwa suala hilo linazungumzika na kwamba wanaotaka katiba mpya wapeleke hoja bungeni ijadiliwe.
Kuhusu suala la mgombea binafsi, Kombani alisema Serikali imeshajivua na kuliachia Bunge liamue, hivyo wabunge wana nafasi nzuri ya kulijadili bungeni.
Hata hivyo, suala hilo lilishawahi kuamuliwa na Mahakama Kuu mara mbili na kutaka waruhusiwe kuwepo katika chaguzi za kisiasa, lakini baadaye serikali ilikata rufaa katika Mahakama ya Rufani ambayo ilisikilizwa na jopo la majaji saba wakiongozwa na Jaji Mkuu, Augostino Ramadhani mwaka huu na waliamua suala hilo lipelekwe bungeni kwa maelezo kuwa mahakama haina mamlaka ya kusikiliza kesi za katiba.
Akizungumzia malalamiko kwamba katiba inampa Rais madaraka makubwa na kutaka yapunguzwe, Kombani alisema suala hilo linapaswa kuwasilishwa bungeni na wabunge wanaoona kuna haja ya kufanya hivyo ili lijadiliwe na kutolewa maamuzi.
Alisema wabunge ndiyo wanaoweza kujadili suala la kumpunguzia Rais madaraka kama wanaona yamezidi, lakini akatahadharisha kuwa suala hilo linaweza kusababisha mkanganyiko na mwingiliano wa mihimili mitatu ya nchi ambayo ni Serikali, Mahakama na Bunge.
Kuhusu mikataba mibovu ambayo Serikali imekuwa ikiingia, Kombani alisema tatizo lililokuwa linachangia hali hiyo ni uelewa mdogo wa wanasheria wa Serikali katika kuandika na kuichambua mikataba.
Alisema baada ya serikali kubaini tatizo hilo, ilianzisha programu maalum ya kuwasomesha wanasheria wake ndani na nje ya nchi ili kuwawezesha kuwa na uwezo wa kumudu kufanya kazi hiyo kwa maslahi ya nchi.
Mambo mengine aliyosema atayapa kipaumbele katika uongozi wake kama Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria, alisema ni pamoja na kukomesha vitendo vya rushwa katika mahakama nchini na kupunguza mrundikano wa kesi.
Aidha, alisema ataziboresha mahakama kwa kuzipatia vitendea kazi, kutoa mafunzo kwa watumishi wa idara hiyo pamoja na kuchunguza sababu zinazochangia kuwepo kasi ndogo katika kushughulikia kesi mbalimbali. Aliahidi kukutana na watumsihi wa mahakama ili kujadiliana na kuzipatia ufumbuzi kero mbalimbali zinazowakabili ili kuzipatia ufumbuzi.
Baada ya Mahakama ya Rufani kujitoa kusikiliza kesi ya mgombea binafsi, aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta, alisema kuwa Serikali inaweza kuaandaa na kuwasilisha muswada bungeni ili Bunge lifanye maamuzi.
CHANZO: NIPASHE