Donnie Charlie
JF-Expert Member
- Sep 16, 2009
- 19,009
- 22,509
Muktasari:
- Suala hilo la mwisho ndio linalozungumzwa sana katika kipindi hiki ambacho mchakato wa Katiba umekwama na hakuna dalili za kuendelea huku wanasiasa wakilalamika kuwa kuna uendeshaji nchi usiozingatia maridhiano hayo ya wanajamii.
Kuna wakati alitumia hafla kuzungumzia Muungano pekee; au kutenganisha siasa na dini; ubinafsishaji, kilimo, au umuhimu wa Katiba.
Suala hilo la mwisho ndio
linalozungumzwa sana katika kipindi hiki ambacho mchakato wa Katiba umekwama na hakuna dalili za kuendelea huku wanasiasa wakilalamika kuwa kuna uendeshaji nchi usiozingatia maridhiano hayo ya wanajamii.
Hotuba zake kuhusu umuhimu wa kuandika Katiba bora, ndiyo hoja ya Watanzania kwa sasa, hasa ile anayozungumzia kupunguza madaraka ya Rais ambayo alitumia kuonya kuwa kwa Katiba ya sasa nchi inaweza kwenda pabaya iwapo itapata mtu atakayetumia vibaya madaraka aliyopewa na nyaraka hiyo.
Nyerere, kiongozi aliyeongoza harakati za kudai uhuru na hatimaye kuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika na baadaye Tanzania, alifariki dunia Oktoba 14, 1999 jijini London, Uingereza
alikoenda kutibiwa.
Miongoni mwa kauli zake alizotoa baada ya kung'atuka madarakani ni kukemea utawala wa kutofuata Katiba na sheria na kusisitiza viongozi kufuata Katiba na sheria za nchi.
"Tujenge utamaduni wa kudhibiti
viongozi wetu kama wanavunja sheria ya nchi, tusiogope. Mkianza kuwa na woga, nawaambia mtatawaliwa na dikteta. Mkiogopa namna hii ninyi wabunge na nani wote mkisema mzee wanakuwa wakali then you are making absolutely like that, You will live under dictatorship. (hapo ndipo mnatengeneza madikteta na mtaishi chini yao).
Alisisitiza nchi huongozwa kwa kufuata Katiba na sheria na kuwadhibiti watu wanaovunja Katiba. "Kama haifanyiki wanadhibitiwa, wale ambao wanavunja Katiba wanadhibitiwa na kusema kweli kabisa lazima tuwe serious katika jambo hilo," anasema.
Katika moja ya nukuu zake Julai 19, 1967 Mwalimu Nyerere alionya dhidi ya uendeshaji nchi usiofuata Katiba. "Katiba haiwezi kupuuzwa.
Akishachaguliwa mtu ataapishwa kuilinda Katiba ili tuweze kumshtaki aliyeikiuka. Mtu yeyote ambaye hawezi kuilinda wala kuisimamia Katiba baada ya kuchaguliwa, hatufai," anasema.
Udikteta ni Serikali ya mtu mmoja au kikundi cha watu wachache na wao ndiyo huwa sheria. Anayepinga watakayo, basi huonyeshwa cha mtema kuni," anasema katika hotuba hiyo.
Alisema wanaopuuza Katiba akisema hawafai. "Kama hawezi kuilinda wala kuisimamia Katiba, aende kuendesha shamba lake, lakini si nchi yetu. Huyo hatufai. Nchi haiendeshwi kwa matamko wala kwa akili za mtu bali kwa Katiba itakayowapa wananchi haki ya kufahamu nini kitatokea kesho kwa kuwa hiyo ni haki yao," alisema Mwalimu.
Akizungumzia utawala wake alisema: "Wale viongozi wanapokiuka wanakemewa na Taifa bila woga. Mimi sidhani kama jitihada zangu zote hizo zilikuwa ni kujenga Taifa la watu waoga, hapana. Haikuwa nia yangu, kama matokeo yake ndiyo hayo, Mwenyezi Mungu nisamehe, mimi sikuiona hiyo.
Akitoa mfano wa jinsi alivyoshirikishwa katika vikao ya Bunge baada ya kung'atuka madarakani, Mwalimu Nyerere aliwaonya viongozi kutotumia mwanya huo kuwaziba midomo wabunge.
"Tuzungumze. Mambo ya nchi yazungumzwe waziwazi katika vikao rasmi vilivyowekwa. Nchi yetu inaendeshwa kwa mujibu wa Katiba na maamuzi makubwa ya nchi yanatokana na vikao na bungeni walivyotaka janja janja ya kuyatoa, hizi ndizo dalili za dictatorship. Lazima zikemewe pamoja na janja janja.
Aliongeza: "Nchi haiongozwi kwa janja janja hata kidogo. Nchi inaongozwa kwa msimamo, na msimamo wake ni thabiti. Watu wanakutana kwenye 'central committee' wanaelewanaaa. Mkihitilafiana sana katika jambo la msingi, wengine wana 'resign' wazi wazi na wanaeleza kwa nini na unajua mambo yanayozungumzwa katika 'cabinet openly' kabisa, wanaelewana vizuri.
Wamzungumzia Mwalimu Mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Profesa Mwesiga Baregu anasema kama Mwalimu Nyerere angekuwepo leo angeanzisha operesheni ya kuwadhibiti viongozi wasiofuata sheria na Katiba.
Alisema kwa hali ya sasa Watanzania wametiwa hofu kwa kila jambo kiasi cha kushindwa kutekeleza utawala wa demokrasia.
"Tuko kwenye kipindi ambacho kila kitu kimepigwa marufuku, hata kumjadili Tundu Lissu haturuhusiwi. Nadhani Mwalimu aliyaona haya na angekuwepo leo angeyasema tena," alisema Profesa Baregu.
Mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana anasema japo kuna taasisi zinazowakilisha wananchi katika kuwadhibiti viongozi, zimelala.
Alisema uongozi wa sasa umechukua sura ya ukali kwa sababu ya kulala kwa taasisi hizo. "Mwalimu aliposema wananchi wawadhibiti viongozi alimaanisha taasisi zinazowawakilisha kama vyama vya siasa, Bunge nyinginezo. Sasa Bunge linashindwa nini kuwadhibiti viongozi? Limeshindwa kwa sababu limekuwa kimbilio la wahalifu wanaotaka kuwa karibu na watoa uamuzi.
Mtu akishavuruga huko anakimbilia bungeni, hapo litamdhibiti nani?" alihoji na kuongeza: "Taasisi zimelala, sasa Rais atafanyaje? Uongozi wa sasa unafuata nyayo za Nyerere katika kutekeleza mambo muhimu ya Taifa."
Waziri mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili, Njelu Kasaka anasema kuwa Watanzania wamepata bahati kuwa kiongozi kama Nyerere kwani alikuwa na maoni ambayo mpaka sasa yanaonyesha hali halisi.
"Mwalimu aliweka misingi iliyosaidia umoja, mshikamano lakini pia alikuwa na maono ambayo yalisaidia nchi kusonga mbele," anasisitiza.
Kasaka anaongeza Mwalimu aliona maendeleo siyo vitu na badala yake watu wanapaswa kubadilika kifikra na kimtazamo ili kuweza kujitegemea na kuamua masuala yao wenyewe ili kupiga hatua
Kuhusu Mwalimu kuwa na maoni ya kutahadharisha Watazania makini na Katiba ambayo alisema inatoa mamlaka makubwa kwa kiongozi kama Rais.
"Unajua kuna nchi zina histori mbaya hivyo viongozi wake wanafaya mambo ya kidikteta hivyo Mwalimu aliliona hilo na kusisitiza elimu kwa wananchi ili waweze kujiamulia mambo yao wenyewe, lakini pia waone umuhimu wa kuchagua kiongozi wanaomtaka na kumwajibisha wakati wowote pindi anapoamua kufanya mambo anayotaka yeye na si aliyotumwa na wananchi."
Anasema kuwa kwa kutambua hilo mwaka 1965 Mwalimu Nyerere alifuta vyeo kadhaa vilivyoonekana kwamba havina masilahi kwa wananchi ikiwamo cha Kamisha wa wilaya na kuweka cha mkuu wa wilaya ambaye anawajibika moja kwa moja kwa wananchi.
Naye Katibu wa wabunge wa CCM, Jason Rweikiza anasema kuwa Nyerere anapaswa kuenziwa kwa kuwa alikuwa kiongozi aliyeweka misingi imara ambayo mpaka sasa imelinufaisha Taifa.
Rweikiza ambaye ni mbunge wa Bukoba Vijijini anasema kuwa ili kumuezi Mwalimu Nyerere, Watanzania hawana budi kuendeleza demokrasia, viongozi kufuata Katiba iliyowekwa na wananchi lakini pia kuachana na mambo yote
yanayorudisha nyuma maendeleo. "Nyerere alikuwa mpenda maendeleo na kuchukia vitendo vya rushwa kwa kuamini ni adui namba moja wa haki hivyo hatuna budi kufuata nyayo zake ili kuhakikisha tunajipatia maendeleo."
Anasema hata sera ya viwanda iliasisiwa na Mwalimu Nyerere ndiyo maana kipindi chake kulikuwa na viwanda vingi vilivyokuwa vikichangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa nchi hivyo kwa kuendeleza viwanda na kuanzisha vipya tutakuwa tukimuenzi yeye.
Anasema Mwalimu Nyerere aliwekeza nguvu katika kuimarisha viwanda vilivyopo nchini kwasababu aliamini ndiyo njia pekee ambayo nchi inaweza kujinasua kiuchumi na kuepukana na kutegemea uingizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Wakizungumza katika kongamano la kumbukizi ya Mwalimu Nyerere aliyewahi kuwa msaidizi wake wa karibu Joseph Butiku, ameutaja utawala bora kuwa ndiyo unaoweza kuisaidia nchi katika uchumi wa viwanda.
"Ukiona nchi ina viwanda vingi na vijana wapo ujue hiyo nchi ina watu walioendelea," anasema Butiku.
Butiku aliwahi kufanya kazi kwa karibu na Mwalimu akiwa ni msaidizi wake katika masuala mbalimbali.
Naye spika mstaafu wa Tanzania, Anne Makinda anasema wakati wa utawala wa Mwalimu mojawapo kati ya sera alizotaka ni asilimia 60 ya pamba iliyolimwa nchini, iwe inafanyiwa usindikaji nchini na kutokana na hilo viwanda mbalimbali vilianzishwa ikiwa ni sehemu ya maono yake.