Nimevutiwa sana kujua Historia ya mwanamke shupavu ambaye alikuwa ni mtawala wa kutoka katika kabila la waha wa Jamii ya kitutsi, ukanda wa Kasulu sehemu za Heru Juu.
Heru Juu
Heru ni eneo linalopatikana Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma.Heru imegawanyika katika sehemu mbili nazo ni Heru juu na Heru chini. Heru juu inaundwa na vijiji vya Munyegera,Heru na Buha pamoja na vijiji vya ukanda wote wa juu kuelekea Buhigwe. Heru Chini inaundwa na vijiji vya Nyansha, Mgandazi, Ntare, Bugaga, Nyumbigwa, Nkundutsi, Zeze na vijiji vyote vya maeneo ya Kasulu ya chini.
Asili ya kabila la Waha ni kijiji cha Buha kinachopatikana eneo la Heru Juu. Waha kutoka Buha walisambaa na kuja eneo la chini la Kasulu (Heru Chini). Muingiliano huu wa Wanyaheru kutoka Buha (Heru juu) na kushuka chini ya vilima vya Bugaga, Nkundutsi hadi kuelekea Zeze kulileta muingiliano wa Lugha na kuzaa tofauti za matamshi baina ya Waha wa Buha(Wanyaheru) na Waha wa Maeneo ya Chini. Lakini kihistoria Wanyaheru (Buha) ndiyo Waha asilia na Kiha cha Heru (Buha) kina tofauti ya kimatamshi na jamii zingine za Waha. Na kiha cha Buha/Heru ndicho kiha asilia. Usisahau pia pale ndipo kuna Ngoma za asili za waha zinazojulikana kama NGOMA ZA BWAMI.
Mwami Theresa Ntare
Mwami Theresa Ntare alifunga ndoa na George Shinganya ambao kwa pamoja walijaliwa kupata watoto kadhaa. Kwa mila za Kiha, Mwami haolewi. Akiolewa inabidi ahame milki yake ya Uchifu ili akawe mke wa huyo muoaji. Hivyo basi, Mwami Ntare hakuolewa na
Bw. George Shinganya. Familia ya Mwami ndiyo iliyolipa mahari kwa familia ya
Bw. George Shinganya. Jina la Shinganya likaondolewa na akaitwa George Ntare. George Ntare alikuwa akiishi maeneo ya karibu na barabara inayoelekea Munyegera - Kati ya ilipo shule ya msingi na Kahaga Dispensary (kulikuwa na soko hapo kati miaka ya 1985). Baadaye ndoa ya Mwami Theresa Ntare na George iliingia tafrani na Mwami Theresa Ntare akaoana na Mwami Louis Dantes Ngua wa Ufipa. Kama kumbukumbu zangu ziko sawa, nyumba ya Mwami Ntare haikuwa umbali mrefu na lilipo kanisa la Roman Catholic, Heru Juu kama unatokea Mapanda Njia au zilipo ofisi za kijiji.
Zamani zile jamii nyingi za Kiafrika zilitajwa kuwaweka nyuma wanawake, Mwanamama Mwami Theresa Ntare aliweza kuwa Kiongozi wa Jamii ya Heru huko Kasulu. Hakuishia hapo, mama huyu aliweza kushika wadhifa mkubwa ambapo alikuwa ni mkuu wa machifu akipokea kijiti kutoka kwa Chifu Petro Itosi Marealle mwaka 1958. Makabidhiano yalifanyikia shule ya Mzumbe, na mpaka sasa Mzumbe kuna bweni linaitwa Ntare. Mwami Theresa Ntare alikuwa ni mmoja ya Wabunge wachache wa Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika kabla hata ya Uhuru wa Tanganyika.
Tulashashe numbu, nzembagiza nu mukubhi!
Tuendeleze historia kutoka hapa sasa kwa wanaoifahamu kwa undani Zaidi.
Credit to JF particularly
Chachu Ombara,
fundimchundo, and
Vyamavingi