- Source #1
- View Source #1
Nimeona huko walimwengu wakijadili kuhusu vile vipele vinavyozunguka kichwa cha uume, sasa baadhi wanadai kuwa mwanaume mwenye hivyo vipele ana asilimia ndogo sana ya kuambukizwa UKIMWI hasa akiwa na damu group O-, lakini pia mwanaume mwenye navyo hawezi kupata magonjwa ya zinaa.
Haya mambo yanachanganya, tusije jikuta tunalombana bila tahadhari tukapata majanga.
Naamini humu tutapata uhalisia wa hili.
- Tunachokijua
- Vipele vidogo vitokeavyo kwenye kichwa cha uume kitaalamu hujulikana kama Pearly penile papules ambavyo mara nyingi hutokea baada ya mwanaume kubalehe. Vipele hivi hutokea kwa kuzunguka kichwa cha uume vikiwa vimepangana kwa kufuatana kuzunguka kichwa cha uume. Vipele hivi sio vya kuambukiza na wala huwezi kumuambukiza mtu.
Magonjwa ya zinaa (ngono) huambukizwa kwa njia ya ngono mfano Kaswende na Kisonono, wakati mwingine huweza kuambukizwa kwa njia isiyo ya kufanya ngono moja kwa moja mathalani mama anaweza kumuambukiza mtoto wakati wa kujifungua. Kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani (WHO) takribani watu milioni moja kila siku wanapata magonjwa ya zinaa yanayotibika huku wengi wakiwa kati ya miaka 15-49, na wengi wao wakiwa hawaoneshi dalili.
Tovuti ya MedicalNewsToday wanabainisha kuwa bado haijabainika haswa vipele hivi (Pearly penile papules) vinasababishwa na nini, na badala yake inaaminika kuwa vinatokea katika hali ya kawaida tu. Haviambukizwi kwa njia ya ngono, na wala havisababishwi na viambukizi (infections) au magonjwa, havina hatari kwa mtu mwenye navyo. Huwezi kujikinga na vipele hivi na wala havina matibabu maalum ingawa kuna baadhi ya njia ya kuvitoa zinazotolewa na wataalamu wa afya ikiwa mtu hatokuwa na amani kuwa navyo.
Makala ya Health.com inaeleza kuwa vipele hivi vya (PPP) ni hali ya kawaida ya utofauti wa ngozi, na havina madhara ama hatari yoyote, pia kuwa navyo haina maana kuwa vinakuweka kwenye hatari ya kupata magonjwa mengine.
Hakuna uthibitisho unaoonesha kuwa mtu mwenye vipele hivyo hayupo katika hatari ya kupata UKIMWI ama magonjwa ya zinaa. WebMd wameandika kuwa kama una vipele hivi na umekuwa ukishiriki ngono ukijihisi una magonjwa ya ngono nenda ukamuone daktari na ukamueleze unavyojihisi.
Tovuti ya NIH inaeleza kuwa ni vyema kuchukua hatua mbalimbali ili kuweza kujilinda na UKIMWI ikiwemo kutoshiriki ngono zembe, kutokuchangia vitu vyenye ncha kali pia unaweza kutumia kondomu.