JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,780
- 6,607
Kufuatia Video iliyosambaa mitandaoni ikionyesha Mjasiriamali mdogo wa ndizi akichukuliwa bidhaa zake na mgambo wa Halmashauri ya Mwanza, kuna matamko kadhaa yametolewa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Innocent Bashungwa
WAZIRI AAGIZA MKUU WA MKOA AINGILIA
"Nimeona video inayosambaa mitandaoni ikionesha matunda aina ya ndizi ya mfanyabiashara mdogo yakipakiwa na mgambo kwenye gari aina ya Toyota Hilux.
"Inasemekana tukio hili limetokea Jijini Mwanza. Namuagiza Mkuu wa Mkoa, Mhe. Eng. Gabriel Luhumbi kufuatilia kubainisha wahusika na hatua kali zichukuliwe dhidi yao.
"Ninaendelea kuwaelekeza Wakuu wa Mikoa kote nchini kuhakikisha zoezi la kuwapanga wafanyabiashara wadogo wa machinga linafanyika kwa utulivu na amani na kujali utu.
"Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya mpaka haya yanatokea kwenye maeneo yenu mjitathimini kama mnatosha," - Waziri Bashungwa.
Tamko Halmashauri ya Jiji la Mwanza
Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kupitia barua kwa umma jana Jumamosi Aprili 16, 2022, umelaani vikali kitendo cha kinyama kama kinavyoonekana katika video inayosambaa mitandaoni kilichofanywa na baadhi ya Askari Mgambo wa Halmashauri, kuchukua bidhaa aina ya ndizi za Wajasiriamali wadogo yaani Machinga.
Bidhaa hizo zilizokuwa zinauzwa katika toroli na zinaonekana kutupiwa katika gari ya Halmashauri na Mgambo hao kinyume na taratibu za Oparesheni ya kuwaondoa Machinga katika maeneo yasiyo rasmi tukio ambalo ni la unyanyasaji na linahatarisha usalama wa mali za Wafanyabiashara ikiwemo kupoteza ubora na kuharibika kabisa.
Halmashauri ya Jiji la mwanza haihusiki kwa namna moja au nyingine kuagiza Askari kuendesha zoezi hili kwa namna linavyoonekana bali ni utashi na nía ovu ya Askari Mgambo hao jambo mbalo ni kinyume kabisa cha maelekezo ya oparesheni.
Kufuatia hili Uongozi wa Halmashauri umechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha Askari Mgambo waliohusika kutojihusisha katika Oparesheni ya kuwaondoa machinga katika maeneo yasiyo rasmi wakati taratibu nyingine za kisheria zikiendelea kufanyika dhidi ya wahusika wote.
Halmashauri inaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kwa umma hasa wafanyabishara waliopata kadhia hii na kusisitiza kuwa Halmashauri inaongozwa kwa miongozo, sheria na taratibu kwa kuzingatia utu na maadili na inatoa wito kwa Askari Mgambo kuwa waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia miongozo, sheria na taratibu.
Source: Global Publishers