Mwanza: Wapangaji Nyamanoro waomba serikali iingilie kati baada ya kufukuzwa katika nyumba walizopanga

Mwanza: Wapangaji Nyamanoro waomba serikali iingilie kati baada ya kufukuzwa katika nyumba walizopanga

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
5,352
Reaction score
15,876
Wapangaji waliokuwa wakiishi katika nyumba namba 59, kwenye viwanja namba 169, 171 na 173, Kitalu “F”, mtaa wa Mnyampala, Kata ya Nyamanoro, Wilaya ya Ilemela, wameiomba serikali iingilie kati na kuwasaidia kupata haki zao baada ya kufukuzwa na kutolewa nje ya nyumba walizokuwa wakiishi.

Wapangaji hao wamedai kukumbwa na sintofahamu hiyo baada ya nyumba hiyo kuuzwa kwa mmiliki mwingine, hali iliyosababisha baadhi yao kukuta samani zao zikiwa zimetolewa nje huku wengine wakiwa bado ndani ya vyumba vyao. Tukio hilo lilitokea kabla ya nyumba hiyo kuanza kubomolewa na dalali wa mahakama, Nsombo & Company Limited.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wapangaji hao wameiomba serikali pamoja na mamlaka husika kufuatilia kwa karibu suala hilo ili waweze kupata stahiki zao za kisheria.

Miongoni mwa wapangaji hao ni Veronica Ngaya, ambaye ndiye aliyekuwa mpangaji mkuu wa nyumba hiyo yenye vyumba 16, aliyepangishwa na Bw. Dawson Salewa, kisha yeye kuwapangisha wapangaji wengine. Ngaya anadai kuwa baada ya kuliboresha eneo hilo, mmiliki huyo alipata tamaa na kumtuma mwakilishi wake, anayefahamika kwa jina la Aboubakar Kapela, kubadili mikataba ya wapangaji waliokuwa wameingia kupitia kwake.

Aidha, Veronica Ngaya ameeleza kuwa wakati zoezi hilo linafanyika, mwakilishi huyo hakuwa na mamlaka ya kisheria katika baadhi ya maeneo, kwani aliruhusiwa kusimamia kiwanja namba 171 pekee, lakini walivunja pia majengo yaliyopo kwenye viwanja namba 169 na 173, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Bw. Moses Msholange, akizungumza kwa njia ya simu na waandishi wa habari, amekiri kuwepo kwa mgogoro huo na kusema kuwa unahitaji kufuatiliwa ili haki itendeke.

Kwa upande mwingine, Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Mwanza, kupitia maombi madogo namba 82 ya mwaka 2026 yanayotokana na maombi namba 96 ya mwaka huo, Mei 25, chini ya mwenyekiti wake Paulos Lekamoi, lilitoa notisi ya zuio kwa wadaiwa, mawakala wao au mtu yeyote anayefanya kazi kwa maelekezo yao, kutomwondoa wala kumbughudhi kwa namna yoyote Veronica Paul Ngaya katika eneo lenye mgogoro hadi shauri litakaposikilizwa na kuamuliwa.
 
Back
Top Bottom