Askofu amshambulia Sophia Simba
2009-04-30 14:37:56
Na Restuta James
Askofu wa Kanisa la Pentecostal Evangelistic lenye Makao Makuu mkoani Mbeya, Zebadiah Mwakatage, amemshambulia Waziri wa Nchi, Ofsi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba, kuwa kauli yake ya kutetea mafisadi ni udhalilishaji serikali.
Alisema hali hiyo itafanya Watanzania kuamini kuwa waziri huyo na seikali yake wameajiriwa kuwa mawakili wa mafisadi.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Askofu Mwakatage, alisema anashangaza na kukatisha tamaa kwa tamko la serikali kupitia Waziri Simba, kutetea mafisadi na huku akijua umaskini unaokabiliwa Watanzania umetokana na kuchotwa kwa mabilioni ya fedha.
Alisema hata baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanaosema Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, anajipendekeza kwa Rais Jakaya Kikwete ni heri kuliko kujipendekeza kwa mafisadi kama alivyofanya Simba.
``Hivi Waziri Simba ameajiriwa uwakili na mafisadi kuyatetea, maana wao wana fedha tena wana midomo yao ambayo wao ndio wangelalamika, kwanini aibuke na kuwatetea eti ni wafanyabishara safi, hapa kuna mashaka,`` inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Alisema kutokana na maandiko matakatifu, Mengi asione ajabu kuchukiwa na mafisadi na baadhi ya viongozi wa serikali bila shaka wana maslahi wanayopata kutoka kwa mafisadi.
Askofu Mwakatage alisema kwa kuzingatia kuwa msema kweli ni mpenzi wa Mungu, Watanzania wataendelea kuwaombea waadilifu, wanaouchukia ufisadi kama Mbunge wa Karatu, Dk Wilbroud Slaa, Dk Harrison Mwakyembe, Mbunge wa Same, Anne Kilango, Spika wa Bunge, Samuel Sitta na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka.
``Nchi yetu tajiri kwa kila kitu, imebatizwa jila la dharau na aibu la umaskini, Mungu tuokoe. Wachonganishe ndimi zao mafisadi na waongo wote wasielewane,`` alisema Askofu Mwakaatage.
Juzi, Simba alijitokeza hadharani na kutetea wanaotuhumiwa kuwa mafisadi mapapa watano waliotajwa na Mengi na kwamba, kitendo cha kuwataja ni sawa na lugha ya kijiweni.
Simba alisema mapapa hao waliotajwa na Mengi ni watu safi na waadilifu kwa sababu, hawajahukumiwa na mahakama.
Alisema Mengi ameingilia kazi za serikali na kumtaka aiache ifanye kazi.
SOURCE: NIPASHE