Safari bado ndefu
Ikulu yamuonya Reginald Mengi
*Yamtaka aheshimu vyombo vya dola
*Yasema athibitishe tuhuma alizotoa
*Yakanusha taasisi zake kumuandama
*Jeshi la Polisi latamka kumchunguza
Na Waandishi Wetu
SIKU moja baada ya mfanyabiashara maarufu hapa nchini, Reginald Mengi, kutoa madai mazito ya kuandamwa na baadhi ya viongozi wa serikali na taasisi za dola, Ofisi ya Rais Ikulu, imetoa tamko la kumuonya, ikimtaka aviheshimu vyombo vya dola.
Imesema Mengi anapaswa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili viweze kufanyia kazi tuhuma za ufisadi alizozitoa katika vyombo vya habari dhidi ya wafanyabiashara watano kati ya kumi aliodai kuwa ni mapapa wa ufisadi hapa nchini.
Aidha, Ikulu imekanusha madai ya Mengi kuandamwa na baadhi ya viongozi wa kiserikali pamoja na taasisi zake, na kueleza kuwa, anapaswa kutoa ushahidi na vielelezo vya tuhuma alizozitoa dhidi ya wenzake, ili ziweze kufanyiwa kazi.
Msimamo huo wa Ikulu dhidi ya kauli za Mengi, ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, ulitolewa jana na Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi, Premi Kibanga, katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima Jumatano kupitia simu yake ya kiganjani.
Mengi anavyosema ameandamwa sasa, ameandamwa vipi? Alitoa sijui tuseme ndiyo kashfa au tuhuma za ufisadi, kwa hiyo ulikuwa ni wajibu wa vyombo vinavyohusika kumwita ili atoe ushahidi na vielelezo vyake ili viweze kufanyiwa kazi.
Hakuitwa yeye tu, ameitwa pia Rostam Aziz, katika idara zote hizo. Hawa wote walitoleana kashfa za ufisadi na wote waliitwa ili watoe ushahidi wao. Sasa kwanini Mengi anasema ameandamwa? alihoji Kibanga.
Akizungumzia kauli ya Mengi kuwa anamtegemea Rais Kikwete kumnusuru, Kibanga alisema kama anadai hivyo basi anao wajibu wa kumsaidia katika vita ya ufisadi.
Alisema anapaswa kutumia nafasi hiyo si tu kwa kuwataja mafisadi, bali pia kwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vyote vya dola vilivyo chini ya Rais Kikwete, ili viweze kuufanyia kazi ushahidi wake na kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya wahusika, ikiwa watathibitika kufanya ufisadi.
Vyombo vya dola havimwandami mtu. Na anaposema rais atamlinda, ni vema akaelewa kuwa Rais Kikwete ni rais wa wananchi wote. Rais Kikwete halindi mtu mmoja mmoja, analinda Watanzania wote.
Kama yeye ni rafiki wa Kikwete, basi autumie urafiki huo vizuri kama anavyofanya katika vita ya ufisadi. Lakini sasa asiishie tu katika kuwataja mafisadi, maana sasa kila mtu tu akitaja fulani fisadi kutakuwa na utulivu kweli? Yeye aviheshimu vyombo vya dola na amsaidie rafiki yake (Kikwete), kwa kuvipa ushirikiano vyombo hivyo, alisisitiza Kibanga.
Naye Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, alipohojiwa na gazeti hili kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu madai ya Mengi kuandamwa na taasisi za dola, likiwamo Jeshi la Polisi, alisema anachojua ni kwamba, polisi wanamchunguza Mengi, lakini hawamuandami.
Manumba alikataa kuzungumzia suala hilo kwa undani, kwa maelezo kuwa msemaji wa jeshi hilo kuhusu suala hilo ni mkuu wa jeshi hilo, Inspekta Jenerali Said Mwema.
Gazeti hili lilipomtafuta Mwema kupitia simu yake ya kiganjani, ilipokelewa na msadizi wake ambaye alikataa kutaja jina lake na kueleza kuwa yupo katika kikao.
Hata hivyo, alipoulizwa kama anaweza kuzungumza lolote kuhusu madai yaliyoelekezwa kwa jeshi hilo na Mengi, alisema si madai ya kweli, kwa sababu jeshi hilo halina kawaida ya kufanya kazi zake kwa kumwandama mtu.
Hakuna chombo cha dola kinachomwandama mtu. Jeshi la Polisi linafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria, kanuni na maadili yanayoliongoza, lakini kama unataka kupata taarifa zaidi kuhusu kinachofanyika kwa sasa, wasiliana na Kamishina wa Utawala na Rasilimali Watu, CP Clodwig Mtweve.
Kamishina huyo alipotafutwa, hakuweza kupatikana na simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani.
Jumapili iliyopita, wakati Mengi akizungumza katika ibada iliyofanyika kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Kisereny wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, alisema baada ya kutaja majina ya mafisadi papa, alianza kuandamwa na baadhi ya mawaziri, vyombo vya dola na taasisi za serikali.
Huku akishangiliwa na umati wa waumini wa kanisa hilo lililopo katika eneo la kijiji alichozaliwa, Mengi alimtaja waziri wa kwanza kumwandama kuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba.Mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Dk. Norman Sigalla na Mbunge wa Hai, Fuya Kimbita (CCM).
Mengi alimtaja waziri mwingine aliyemwandama baada ya kutaja mafisadi papa kuwa ni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika, aliyesema alimwita mbaguzi wa rangi.
Alisema mbali ya mawaziri hao kutoa kauli hizo, pia wahariri wa magazeti yake anayoyamiliki, walihojiwa na Msajili wa Magazeti wa Idara ya Habari.
Huku waumini wa kanisa hilo wakiwa kimya, Mengi alisema yeye mwenyewe pia aliitwa na kuhojiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ikidai alivunja sheria ya utangazaji kwa kutaja majina ya watu kuwa ni mafisadi papa, na kwamba hatua hiyo iliashiria ubaguzi wa rangi.
Mengi ambaye alikuwa mgeni mwalikwa kwenye hafla hiyo, alivitaja vyombo vingine vya dola vilivyomwandama kuwa ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ikimtaka apeleke vielelezo.
Pia alisema aliitwa na maofisa wa Jeshi la Polisi, linaloongozwa na IGP, Said Mwema, chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, inayoongozwa na Laurence Masha, wakimtaka apeleke vielelezo vya tuhuma zake.
Nimeitwa na Kamati Ndogo ya Ulinzi na Usalama wa Taifa ili kuhojiwa juu ya tamko langu kuhusu ufisadi. Yote haya yamefanyika pamoja na kwamba kuna kesi mahakamani juu ya jambo hili.
Tukumbuke kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alikwishatoa tamko bungeni kuwa wote waliotajwa, kama wanaona hawakutendewa haki, waende mahakamani. Sasa ni nani ana tamko la mwisho katika hili? Ni mawaziri, taasisi za serikali, vyombo vya dola ama Waziri Mkuu?
Kama raia wa Tanzania, vyombo vya dola ni moja ya mategemeo yangu ya kunilinda mimi na mali zangu, kama raia wengine, lakini pamoja na kusakamwa na vyombo hivyo, nasema siogopi. Ulinzi wangu unatoka kwa Mwenyezi Mungu, pili utatoka kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye naamini hatakubali kuona sitendewi haki, na tatu ulinzi wangu utatoka kwa Watanzania wanaochukia ufisadi, hasa masikini na wanyonge.
Hawa hawana fedha nyingi, ama madaraka, lakini wana nguvu ya sala na umoja bila kujali dini zao, alisema Mengi na kushangiliwa na waamini wa kanisa hilo.
Alisisitiza kuwa, hatarudi nyuma katika msimamo wake wa kupiga vita ufisadi, kwani anaamini rushwa ikiachwa bila kukemewa, wananchi watagawanyika katika makundi mawili; la watu wenye kipato na madaraka na la watu masikini.
Watanzania wenzangu wanaochukia umaskini, wanaochukia ufisadi, ndugu zangu waumini, nawaomba mniombee na tuimbe wimbo namba 59 katika kitabu cha Mwimbieni Bwana, usemao Kazi ni yako Bwana, alisema.
Hatua ya Mengi kutoboa siri ya kusakamwa kwake mara baada ya kutaja majina ya aliowaita mafisadi papa, ilitokana na mahubiri ya Mhashamu Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shayo, aliyeunga mkono harakati zake katika vita dhidi ya ufisadi.
Askofu huyo alimtaka Mengi asikatishwe tamaa na wajanja wachache, ambao wamekusudia kurejesha nyuma juhudi za kujiletea maendeleo.
Taifa letu limegubikwa na mafisadi wachache, wapo Watanzania wenzetu kama Mengi, wamekuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya kifisadi, lakini wanakwamishwa na baadhi ya viongozi walioko madarakani, tukemee kwa pamoja.
Mwaka huu na mwaka ujao, ni vipindi vya uchaguzi mbalimbali, kuna watu wamejaa choyo, wivu, chuki na ubinafsi miongoni mwetu, hakika watu hao ni wabaya kwa maendeleo ya taifa, msiwachague, alisema.
Alisema, Mengi hataki urais wala hana nia ya kuwania kiti hicho, wala uongozi wa aina yoyote, lakini amejitoa kusaidia wanyonge, na rafiki zake ni masikini, walemavu, wajane, wanaoishi na virusi vya VVU pamoja na wenye matatizo mengine ya kijamii.
Source: Tanzania Daima