Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amewataka waganga wakuu wa hospitali zote nchini kuanzia ngazi ya taifa, kanda, mkoa, wilaya hadi vituo vya afya vinavyomilikiwa na halmashauri kuhakikisha wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanapatiwa huduma za matibabu bila kutozwa gharama yoyote.
Dkt. Samizi ametoa maelekezo hayo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Morogoro Mjini, Mohamed Abood aliyeeleza kuwa licha miongozo hiyo lakini bado kumekuwa na usumbufu kwa wakinamama wanaoenda kujifungua hospitalini.
Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hutenga zaidi ya shilingi bilioni saba kila mwaka kugharamia huduma za afya kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, hivyo hakuna sababu ya kundi hilo kukataliwa au kutozwa fedha wanapohitaji matibabu katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma.
Soma Pia mijadala ya kero ya malipo kwa wajawazito