Follow along with the video below to see how to install our site as a web app on your home screen.
Note: This feature may not be available in some browsers.
Dah ulikuw una jambo la kuweka sawa na mshua sio bure[emoji38][emoji38][emoji38]... Nilipata mzuka wa kuingia kwenye kilimo baada ya kufanya kazi kwenye shamba la matikiti la mzee mmoja hivi. Mavuno aliyoyapata ndio yalinishawishi na mimi kujikita huko.
Kutokana na ka akiba ambako nilikuwa nimekusanya mpaka muda huo, nikatafuta shamba kule kule Songea. Nilibahatika kupata eneo la kukodi sehemu fulani inaitwa Mpitimbi, heka 1. Kuna dogo nilikuwa nimezoeana nae kutokana na mishe za vibarua, huyo ndio nikawa napiga nae. Niliandaa shamba vizuri (robo 3 heka),weka samadi ya kuku, mwagilia kwa muda wa wiki kama mbili alafu ndio nikapanda mbegu zangu. Siku chache baadae zikaanza kuchipua. Ila walitokea wadudu wakaanza kushambulia yale majani mawili ya mwanzo kabisa. Nikajitahidi kupiga sana dawa, hatimaye nikafanikiwa kudhibiti. Hapo ile robo heka iliyobaki wazi,nikaweka maharage ya njano,lengo ni kujaribu kuona mwelekeo wake pia.
Miezi ikakata, tikiti zikatoka vizuri japo sio kwa wingi na ukubwa niliotarajia. Utata ukaja kwenye soko. Nakumbuka mnunuzi alikuja hadi shambani kwangu. Wakati mm gharama toka mwanzo mpaka yanakomaa nilitumia kwenye kama laki 7 mpaka 8, ila hesabu za kuyauza yote hela iliyokuja ni kama laki 3 na 40. Tulizozana sana na yule mnunuzi, ila mwisho wa siku ikawa ndio hivyo. Mpaka leo ile karatasi ya mahesabu na yule mnunuzi ninayo (Badae naweza nikaiweka hapa).
Kule ikabidi nitoke baada ya kuvuna na yale maharage pia ambapo nilipata kilo kama 60 (mimi nilipanda kilo 15), nikatafuta eneo jingine la kulima. Kuna sehemu inaitwa mshangano, kuna bonde la umwagiliaji, nikapata nusu heka. Nikaamua kulima tena tikiti, maana kila nikifikiria yule mzee wa kwanza alivuna fresh tu kwanini mm ishindikane?
Mwanzo mambo yalienda vizuri tu. Dawa nilikuwa napiga kila baada ya wiki au wiki mbili kutegemeana na aina ya dawa. Nakumbuka yalikuwa yamebakiza kama wiki 3 yatimize miezi mitatu, nilienda kwa ajili ya ukaguzi wa kawaida tu na kupiga dawa. Kama sikuzimia siku ile basi sizimii tena. Nafika shambani, kila tikiti unaloshika linabonyea, kugeuza chini limeanza kuoza. Nilisizi kwa dakika kadhaa, nikakaa na chini kabisa.
Badala ya kuuzia watu, niliishia kumuuzia mfuga nguruwe, kiufupi yakageuka chakula cha mifugo.
Ile kilo 60 ya maharage ambayo nilikuwa nafikiria pengine nije kuyafanya kama mbegu upya maana mwelekeo wa kilimo chake niliuona kidogo mzuri,nilikuwa nayatunza gheto. Nilipoyavuna na kuweka kwenye kiroba,sikuyapiga dawa,siku nakuja kuyacheki nakuta matobo matobo tu,wadudu washapita.
Kutokea hapo nikafulia upya. Nikaanza tena kufanya vibarua. Kuna jamaa akanishawishi sana tulime mahindi maana yanalipa ila sikumuelewa, nikaendelea na vibarua. Kuna siku nikapata tenda ya kuvuna na kupakia tangawizi kwenye lori, maana kuna mteja alinunua sasa anahitaji huo msaada. Nikaenda kupiga kazi, hiyo sehemu inaitwa Madaba. Tunalima na kujaza kwenye maroba, kila ukijaza kiroba kimoja unapewa 5000. Baada ya kama siku 5 kazi ikaisha tukarudi na lori hadi town Magingo kwa mbele kidogo kuna soko la tangawizi . Kufika pale baada ya ukaguzi, nikapata kibarua cha kupakia kwenye lori la mteja. Kazi imeisha, naenda kupokea ujila wangu, nakuta bosi ni faza, yani baba angu kabisa. Kumbuka hapo tokea nilipoondokaga home sikiwahi kurudi wala kuwa na mawasiliano nao. Na toka tunazaliwa,baba alikuwa anajishughulisha na biashara za kununua na kuuza mazao,japo kipindi naondoka nyumbani alikuwa shughuli zake zilikuwa ndani ya mkoa wetu tu,kati ya vijijini na mijini. Na ndio biashara iliyotukuza,kumuona pale maana yake biashara zake zimepanuka.
Tuliangaliana kwa dakika kadhaa, natamani kama nimkumbatie, maana kiukweli baharia nilikuwa nimeshapigika sana. Atleast hata ningekutana na mama katika mazingira yale walau ningepata faraja kidogo, mshua kauzu ananiangalia tu bila kusema chochote.
Nikamwamkia akaitikia vizuri. Ikabidi nimuombe msamaha. Badala ya kuitikia, ananiuliza hapa umekuja kuniomba msamaha au kufata ujira wako? Nikamwambia lengo ilikuwa ujira mzee, ila baada ya kukuona sina budi kuomba msamaha. Mshua ananiambia kama ungetaka kuniomba msamaha ilibidi urudi unifate nyumbani, yani tunakutana tu kwa bahati mbaya ndio unaomba msamaha, tusingekutana je?
Nikawa mpole kidogo. Ila nikamwambia natamani kurudi ila nauli ndio ilikuwa tatizo, lasivyo ningesharudi kitambo. Mshua akasema utarudi nyumbani kama ulivyoondoka, yani nikupe nauli ili tu uje kuniomba msamaha? Kama kweli unania basi tafuta nauli urudi, we si mwanaume? Nikamwambia lakini nauli ya kunitoa nyumbani ulinipa wewe, kwanini usinipe na ya kurudi, maana sina kitu kweli.
Nikimwangalia mshua naona kabisa kuwa ananionea huruma, ila kwa nje ameamua kuleta ule ukauzu wa kiume. Acheni mama aitwe mama tu, pale angekuwa yeye nadhani yale maongezi tungekuwa tunayafanya huku tumekaa sehemu tunakula. Faza alikuwa mkavu usoni hadi na mimi nikaanza kupata wasi wasi kama ule wa kwake wa kipindi kile, kuwa mimi ni mwanae kweli? Ila nilivyokumbuka ile kauli ya mama alafu nikaangalia pua ya baba, nikaona bila shaka huyu ni baba angu.
Baada ya kuniangalia sana, sasa sijui kama na yy alikuwa anawaza kama kweli me mwanae, au alikuwa anaangalia pua ili kuthibitisha kauli ya mama, sijui. Ila alimuita Mfanyabiashara mwenzie aliyekuja nae, wakazungumza pembeni alafu nikaona kapewa hela.
Alirudi kwangu akanikabidhi laki 3 na 50. Akaniambia "Ujue kama ungekubali kuendelea na shule, basi ile hela niliyokupa mara ya kwanza isingetosha, awamu ya pili ilibidi nikupe tena. Sasa hii hela ninayokupa kuna posho yako ya kazi ya leo pamoja na ya mahitaji yako ya shule kipindi kile kama ungesoma. Hata siku moja usijekusema hukusomeshwa.
Nikapokea ile hela, nikashukuru sana. Mshua yeye ananiangalia tu. Nikamuomba tena msamaha. Ila msimamo wake ukawa ule ule, ukitaka kuniomba msamaha rudi nyumbani,maana hujui hata mama yako yupo na hali gani miaka yote umeondoka na hakuna anayejua upo wapi. Kwa mara ya kwanza nikakumbuka kuulizia hali za ndugu zangu kule nyumbani, hasa mdogo wangu wa mwisho na Mama. "Ukitaka kujua hali zao, fanya matumizi mazuri ya hiyo hela, sina haja ya kukwambia hali zao, rudi nyumbani ujionee" ilo ndio jibu alilonipa.
Tukaachana, nikarudi zangu kwenye ghetto langu kule moonlinght. Pamoja na maongezi yote yale na Mzee, ila sikumuomba namba ya simu, sio kwamba sikukumbuka, ila nilikuwa nasubiria walau aniulize kama nina simu. Na yeye hakuniuliza wala kuomba namba yangu. Sio kwamba hakufikiria ilo, nilikuja kujua baadae kuwa nae ilo swala alilifikiria ila hakujishughulisha nalo.
Huwa tunarithi vitu na tabia toka kwa wazazi wote wawili, ila nahisi wanaume tunarithi vingi sana toka kwa baba zetu kuliko toka kwa mama. Ukiona huna tabia unazofanana na mzee wako,muulize mama vizuri pengine huyo baba ni mlezi tu
* * * * * * ***
Kesho yake wakati naendelea kutafakari namna ya kurudi nyumbani, jioni nilienda kwenye kijiwe cha draft sehemu moja inaitwa Bombambili. Story za hapa na pale, kuna jamaa akaanza kuongea kuhusiana kilimo cha mbaazi jinsi kilivyo na hela na soko la uhakika. Baadae nikapiga stori kwa kirefu na yule mdau, tukabadilishana namba.
Niliporudi ghetto, baada ya kutafakari sana nikajiambia inabidi nisubirie msimu wa kilimo ufike nilime mbaazi hata msimu mmoja, nipige hela alafu ndio niende nyumbani.
Nikaghairi kurudi nyumbani kwa wakati ule, nikaanza ushanta ili nipate hela ya kujazia kwenye mtaji. Hutakiwi kujikita kwenye kilimo ikiwa unapresha. Kilichoenda kunikuta sitakaa nisahau kamwe. NILILIMA MBAAZI KIPINDI CHA MAGU.
Analyse #Baharia wa nchi kavu.
........
Aisee kumbe kweli ilipaswa uzungumze na mzee[emoji38][emoji38][emoji38].... Tofauti na wengi wanafikiria, leo hii ukiniuliza shujaa wangu ni nani katika dunia hii,au ni nani namkubali sana katika ulimwengu huu, kwa kujivunia kabisa nitasema "BABA YANGU" . Huko mbele nitakwambia kwanini au hata wewe utagundua sababu.
Msimu wa kilimo ulipofika, sikuwa na hela ya kutosha kusema iniwezeshe kulima eneo kubwa sana. Nilifanya ushirikiano na jamaa mwingine mmoja, kwa pamoja tukafanikisha kulima heka tano za mbaazi. Shamba tulipata eneo moja lipo manispaa ya Songea, linaitwa Mlilayoyo. Tuliweka juhudi zote na usimamizi wa hali ya juu. Zao lilistawi vizuri sana. Naweza sema kati ya watu wote tuliokuwa tumelima maeneo ya pale, mimi na jamaa ndio tulikuwa na matokeo mazuri. Nakumbuka wakati tunaanza kilimo, bei ya mbaazi ilikuwa juu na nzuri. Kilo moja kuna sehemu ilikuwa inafika hadi 2500.
Msimu wa mavuno wakati unakaribia, ndio zikaja zile tetesi za kushuka kwa mbaazi. Tetesi zikawa kweli, soko likapotea. Ikafika kipindi kisado kinauzwa shillingi 500. Tukashauriana na jamaa tusivune, tusubirie hadi soko likae vizuri kwanza. Siku zikaenda, soko halikai sawa, mpaka mbaazi zetu zikakutana na msimu mpya wa kilimo. Gharama ya kuzivuna ilikuwa kubwa kuliko hata hela ambayo ingepatikana baada ya kuuza, achilia mbali gharama za kuendesha shamba mpaka kufikia hapo.
Mwenye shamba lake anatuuliza, tunampango gani msimu ujao? Tunalikodi tena shamba lake au la? Kama hatukodi, basi tuvune mbaazi tumuachie ardhi yake. Mshirika wangu ananiuliza, tunafanyaje? Nikamwambia me sina cha kufanya , we amua chochote utakachoona nakuachia shamba lote, siwezi kuingia tena gharama za kuvuna. Jamaa nikatemana nae kwa mtindo huo. Nikarudi ghetto pale moonlight.
Kwavile hela niliingiza zote kwenye kilimo, nikawa nimefulia tena. Hapo nilipata somo kuwa kama bajeti ya unachotaka kufanya ni laki 3,alaf na wewe una laki 3 hiyo hiyo, acha. Tulia kwanza mpaka upate hela ya ziada walau mara mbili ya hiyo au hata nusu yake, vinginevyo utakuja kuona watu wanakuchawia huko mbeleni.
Nilianza upya vibarua, hapo nipo choka mbaya. Baada ya kudunduliza na kupata hela kadhaa, sikutaka kujiuliza mara mbili wala kuzurura sana mitaani maana naweza nikakutana na mtu mwingine akanipa fursa. Nikaamua kurudi nyumbani.
* ** ** ** ****
Nilifika nyumbani majira ya usiku. Kabla sijaingia kwenye himaya ya nyumbani kabisa, nilipaangalia kwa muda mrefu sana. Kwa muonekano palikuwa panavutia na maisha hayakuwa mabaya. Nikagonga mlango baada ya kuvuka fensi ya maua na geti kubwa la mbao. Baba ndio alifungua mlango, alivyoniona akaniambia karibu. Yani hakuonesha kama ameshangaa, amefurahi au kushtuka, kiufupi alichukulia kama nilienda dukani sasa ndio narudi.
Asubuhi ya siku hiyo, naskia mama alijichoma na msumali wakati anapalilia maua pale nyumbani, toka hapo hakuweza kukanyaga vizuri chini, alikuwa anachechemea, ila aliponiona nahisi alipata ganzi ya mguu, maana sio kunikumbatia tu, bali pamoja na ndevu zangu alinibeba. Nikapata faraja niliyoitaka, faza nikampotezea. Pale mezani alikuwa ndio anamtengea mzee chai na maandazi (siku zote baba hupenda kunywa chai usiku hata awe ameshiba vipi). Basi ile chai akanipa mimi, Mzee anauliza vipi mbona unagawa chai yangu? Mama hana hata habari nae. Mara kaniletea hiki, mara kile, ilimradi ukarimu. Nilipoenda kulala, kila mara anakuja kunichungulia. Sina uhakika kama yeye alilala usiku ule.
Asubuhi ndio tuliweza kuongea vizuri kama familia. Hapo mama ameshawaambia ndugu zangu wote kuwa nimerudi. Baada ya chai ndio niliweza kukaa na kuongea na mzee. Kitu cha kwanza kuniuliza "Umefata ada?". Nikamwangalia kwa mshangao, ila kilichonishangaza zaidi nilipogundua kuwa hakuwahi kuwaambia nyumbani kuwa tulikutana Madaba, Songea. Ilo lilinishangaza.
Ila aliniambia, "Ulitaka nimwambie mama yako kuwa baada ya kupotea miaka mingi tulikutana ukiwa kibarua ambae maisha bado yamekupiga? Au baada ya miaka mingi kutoonekana, tumeonana ila bado ukaniomba hela? . Nilijua hutorudi ndio maana sikumwambia chochote mama yako kwa kipindi kile, na pia sitoshangaa kama utaondoka tena. Najua tulipoachana maisha yako yaliendelea kuwa magumu na ndio maana hata hela niliyokutumia wala hukunirudishia. Nikajiuliza hela gani alinitumia huyu mzee? Nahisi alijua ninachowaza, akaniambia siku tuliyoachana alichukua namba yangu toka kwa wale vibarua niliokuwa nafanya nao, na alipoona imepita zaidi ya miezi 6 sijaonekana nyumbani alinitumia laki 3 kwenye simu. Nikakumbuka kuna siku iliingia hela, nikajua mtu kakosea kutuma, nikaitoa kwa wakala alaf nikakausha. Mtumaji nae hakunicheki tena. Niliona aibu kichizi.
Baba akaniambia "Ikitokea leo hii Mama yako aseme nyie wote 7 sio wanangu, nitakubaliana nae kwa hao 6 wengine lakini wewe nina uhakika wa asilimia zote ni mwanangu. Mimi na wewe ni mapacha tuliozaliwa katika miaka tofauti, kwa kifupi ww ni mimi". Maneno ya mzee yalinigusa sana kwa mbali machozi yakawa yananilenga hivi. Faza akaniambia "Kama unalia nenda jikoni kwa mama yako" . Mzee wangu kauzu kichizi yani,kwanza toka nakua sijawahi kumuona anasikitika. Nikabaki nashangaa tu maneno yake. Akazidi kuniambia " Tofauti ya ww na mimi, ni kwamba mimi nilirudi baada ya safari yangu kuelekea mwishoni,nilirudi nikiwa shujaa. Wewe ni shujaa lakini safari yako haijaisha,umerudi ikiwa kati"
Kuna mengi sana hatuyajui kuhusu wazazi wetu ambayo yangetufunza na kutujenga, hii inatokana na kwamba tuko bize sana kiasi tunakosa muda wa kuzungumza nao. Misukosuko tunayokutana nayo leo hii, majibu yote yapo kwenye maisha waliyopitia wazazi wetu. Tunatafutaga majibu, lakini majibu sahihi yapo tulipotoka. Baba yangu ni Shujaa wangu,Mimi ni Baba yangu,na Baba yangu ni Mimi, unajua kwanini? Ni kutokana na stori fupi ya safari ya maisha yake aliyonisimulia.
* * * * * *
Kwa ufupi tu ilikuwa hivi. Anasema "Sikuwa na uwezo mkubwa wa kuelewa darasani, shule niliishia elimu ya msingi hata mtihani wa mwisho sikufanya, nilifukuzwa kwa kosa la kuchoma ofisi ya walimu. Tokea hapo nilikuwa naonekana kama mtoto mtukutu nyumbani, babu yako aliniwekea zamu ya kuchunga kila siku, alaf nyumbani sikuwa napewa upendeleo wowote. Kuna siku nilienda kuchunga,jioni nikarudisha ng'ombe ila nikasepa na mbuzi wote. Nikauza na kufanya mtaji. Heri yako unaondoka nyumbani umepewa hela, tena tukijua kuwa utaondoka. Sijui msoto uliopitia ww, lakini msoto niliopitia mimi baba yako ndani ya miaka minne ya mwanzo nadhani ww ungekufa. Ndani ya hiyo miaka minne ya mwanzo kuna siku niliamua kabisa kurudi kwa babu yako nikaombe msamaha, nilifika mpaka pale, nikaiangalia sana nyumba ila nikaona siwezi kurudi nikiwa hivi, nikageuza na kuondoka. Ndio maana sikuile tuliyokutana Songea, nilijisemea kimoyo moyo, kama huyu ni mwanangu hatorudi nyumbani.
Tokea ile siku niliyogeuza, nilijituma sana kiasi kwamba siku niliyorudi nyumbani, nilirudi na idadi ile ile ya mifugo niliyoondoka nayo ila badala ya mbuzi nilirudi na ng'ombe. Ila pamoja na hayo babu yako aligoma kunisamehe hadi kikafanyika kikao na wazee wa kijiji, ndio nikasamehewa,tena baada ya kuchapwa bakora pamoja utu uzima wangu.
Aliendelea kunisimulia vitu vingi sana, hapo ndio nikajua nilidhani nimesota na kupitia tabu nyingi sana, kumbe ningezifananisha na za mzee, basi zangu zingekuwa ni utangulizi tu. Mgodini niliposhindwa kwenda, yeye alishaenda na alishawahi kufukiwa hadi na kifusi. Baba yangu akitembea huwa anachehemea,mguu mmoja ni kama mfupi. Ananiambia ule ulishavunjika mara mbili kutokana na mbilinge za migodini.
Tokea siku hiyo, kila nnapopitia ugumu wowote, lazima nijiangalie kwenye kioo. Baba yangu ni kioo changu.
* ** * * ****
Kurudi kwangu kulirudisha furaha sana nyumbani. Usiku kabla ya kulala, mshua aliniuliza "Una watoto wa ngapi mpaka sasa? Nikamjibu mmoja wa kiume. Akasema namuhitaji, fanya mpango aje hapa nyumbani.
Najua kuna wadau watashangaa kuona nimesema nina mtoto mmoja wa kiume, wakati katika stori yote sijawahi kuongelea ili swala. Katika hii stori ya safari yangu, nimegusa baadhi ya matukio ya kwenye maisha yangu ila sio yote. Na sijagusia mapenzi kwasababu yamenitesa kichizi, nadhani mwanaume akiwa hana hela mwenendo wake wa mapenzi unajilikana tu,mapenzi yanatesa sana Me kuliko Ke. Kuna msemo mmoja nimeuona juzi kuwa "Mwanaume kama huna hela, kazi ya kulinda mahusiano yako muachie Mungu" hii ni kweli kwa asilimia zote. Kwa ufupi kwenye hii safari yangu, mtoto ninae tena wa kiume.
Nikafanya mpango na taratibu zote, nikapewa yule mtoto. Sasa hivi anaishi na babu yake.
Siku ambayo mtoto alifika pale nyumbani, kesho yake mzee aliniita tukawa na mazungumzo ya hapa na pale. Kisha akatoa bahasha na kunikabidhi, kuhesabu ni milioni mbili. Nikamuuliza za nini. Akasema "Babu yako alinipokea baada ya kufanya kikao na wazee kisha nikachapwa bakora,nimekupokea nyumbani ila sitokuchapa...Safari yako bado haijaisha, nenda kapambane". Nilimwangalia yule mzee sikummaliza.
Wiki moja badae nilikuwa ndani ya bus naelekea Songea. Nikarudi rasmi kwenye kilimo. Safari hii nikalima tangawizi..
Nitarudi kukwambia jambo zuri lililotokea. Katika maisha,Baraka za wazazi ni kila kitu.
....
Analyse #Baharia wa nchi kavu.
[emoji12][emoji12][emoji28][emoji28][emoji28] mke yupi mkuu?
Wangu huwa tunaongea naye akilewa....😅😅😅Sehemu ya 9:
.. Katika ile Million mbili aliyonipa Mzee, miliona 1.7 yote niliweka kwenye kilimo. Kuanzia kukodi mashamba, kuyaandaa, mbegu n.k. Hiyo laki 3 iliyobaki ndio ilikuwa inanisogeza. Tangawizi nilipanda sehemu moja kule Madaba, Songea inaitwa Balali (ni milimani huko ndani ndani) . Nilipovuna na kuuza, nilipata faida ya milioni 1.5 (baada ya kutoa ile 1.7 niliyowekeza). Toka nianze kufanya biashara, hiyo ndio ilikuwa mara ya kwanza napata faida toka nianze hustling.
Nikaamua kurudi tena nyumbani kwa Wazee. Nilipokelewa vizuri tu. Kesho yake nikaongea sana na Mzee akitaka kujua maendeleo yangu, nikamuelezea hali halisi. Akatikisa kichwa kukuonesha amependezwa na matokeo. Ile siku ambayo alinikabidhi milioni mbili, ilikuwa makubaliano kwamba mambo yakikaa sawa nimrudishie. Kwahiyo baada ya mazungumzo ya hapa na pale nikamkabidhi bahasha ila hakuangaika kuigusa, aliuliza tu kuna nini. Nikamuelezea. Akatabasam tu, alaf akaniambia "Niliposema unirudishie mambo yakikaa sawa, lengo langu ilikuwa ni kukufanya usisahau ulipozitoa ili ikupe motisha ya kuzitumia vizuri, na uzee huu ukinipa milioni mbili napeleka wapi?
Nilimwangalia sana yule mzee ila sikummaliza. Mazungumzo yaliisha.
Baada ya wiki mbili nikaondoka nyumbani nikiwa na ile milioni mbili, pamoja na ile ambayo ilikuwa faida, nikajisemea moyoni "Safari yangu bado haijafika mwisho, ntarudi nyumbani nikiwa mshindi"
Pamoja na kupata faida kwenye tangawizi, ila sikutaka kuendelea nayo maana ilinisumbua pia mpaka kuja kufikia mavuno. Niliamua kuwekeza ile hela kwenye kitu tofauti kabisa na kilimo. Mungu ni mwema mambo yameenda vizuri sana. Badala ya kurudi nyumbani kishujaa, nikaamua kuwa natuma nyumbani msg za kishujaa. Kila mwisho wa mwezi huwa nawatumia Baba na Mama laki mbili kila mmoja kwenye account zao za simu. December 2018 niliwatumia mapema sana,Baba alinipigia simu "Christmas jitahidi huwe hapa nyumbani" .
Nikaenda.
Mazungumzo ya hapa na pale,Mzee akaniambia " Nashkuru kwa unavyotuhudumia mimi na Mama yako,yawezekana hujui uzito wa unachokifanya ila ni kikubwa sana. Ila ningependa kukwambia kitu kimoja,mwangalie sana Mama yako. Vitu vyote ambavyo nimefanya mimi kama baba yako,au magumu niliyopitiaga,yote ilikuwa ni kumtengenezea mazingira mazuri mama yako na wanae ambao ni nyinyi,kama unataka kunipa furaha Baba yako,basi mwangalie sana Mama yako. Furaha yake ni yangu. Nina uwezo wa kuvumilia matatizo 100 yanayonisumbua mimi,ila sitoweza kuvumilia tatizo moja linalomsumbua Mama yako. Kwa hali ya uchumi niliyonayo ningeweza kuwa na wanawake wengine,ila siku zote nilimuahidi sitofanya kitu cha kumuumiza,na kamwe sitoweza".
Nilimwangalia sana Mzee wangu,nikaona kumbe nina mzee jembe kiasi hiki? Ikabidi kama kijana nianze kuongea maneno ya kiustaarabu na mimi. Nikamwambia "Nashkuru Mzee kwa maneno yako uliyoongea,yamenigusa sana. Nitawaangalia siku zote wewe na Mama kwa kadiri niwezavyo. Maana hata ningesema nijaribu kuwarudishia fadhila zenu inagenichukua miaka mingi sana" Kabla hata sijamaliza Mzee akacheka. Ikabidi nimwangalie kwa mshangao. Akasema "Sio tu ungejaribu,ukitaka jaribu alafu hiyo miaka mingi unayosema ungetumia,ongezea na mingine 100 ila hutoweza kulipa fadhila yoyote aliyokufanyia mtu,achilia mbali sisi Wazazi wako. Maana hujui walipoteza nini katika kukufanyia wewe fadhila.Kitu pekee unachoweza kufanya ni kulipa wema kwa wema."....akaendelea " Nenda jikoni kwa Mama ako naona ushaanza kutia simanzi hapa,yeye ndio anaweza kuvumilia mazungumzo ya aina hiyo".
Kwa siku hiyo mazungumzo yaliishia hapo,tuliendelea kesho yake. Mzee wangu siku zote hapendi mtu anayeongea kinyonge nyonge au kutia huruma.
Turudi nyuma kidogo:
MWISHONI MWA MWAKA 2017
Hii ni siku ambayo mambo yangu yalienda ovyo sana. Ni siku ambayo niliamua rasmi kumsusia yule partner wangu shamba la Mbaazi. Hapo nilikuwa nimeshasota sana kwenye kilimo na ujasiliamali. Nishasota kitaa bila kazi baada ya kumaliza chuo. Dunia yote naona ipo kinyume na mimi. Nishasikiliza sana wale motivational speakers wote unaowajua ili kutafuta tumaini ila naambualia patupu. Ndipo nilipoamua kumpigia simu Baba. Naongea nae huku nikiwa na hasira inayotokana na ugumu wa mambo plus huzuni pia. Mzee akaniambia "Kama huwezi kuongea bila kulia, basi mpigie simu Mama ako, au la, kata simu, lia kwanza, ukimaliza nipigie tuongee" Mzee wangu ni shujaa wangu aisee. Nikajikaza tukaongea kidogo, akaniambia fanya mpango usafiri uje tuongee vizuri.
Nikawatembelea. Siku moja baada ya kufika mida ya jioni akaniita tuongee. Mama akatutengea chai, mshua akamimina kwenye kikombe kimoja alafu akamuita Mama. "Huyu mpe juice" Nikawahi kusema, na baridi hii ningependa chai zaidi kuliko juice. Baba akaniambia "Dogo ukishaoa utakuwa huru kutoa mapendekezo ya chakula unachotaka, kabla ya hapo chukua kilichopo". Alaf akamgeukia Mama " Mletee juice". Nikawa mpole. Najua alifanya vile kwasababu siku ambayo tuliongelea habari za mwanangu aliniuliza naoa lini, nikamwambia bado sana.
Anyway, nikakubali juice na kikao kikaendelea. Akaniambia najua una maswaibu yamekukuta, ila kabla hujaniambia na kuanza kutia huruma, ngoja nikuelezee ya kwangu. Akaanza kunipa story ya harakati alizopitia na ndizo ambazo nilikuwa nawasimulia tangia story inaanza Asilimia kubwa ya niliyowasimulia ni mambo aliyopitia Mzee wangu. Kati ya yote, yangu ni asilimia kama 5 tu, na hasa yanayohusu kilimo na Shule.
Alipomaliza kunisimulia, nilibaki namshangao. Nikamuuliza "Mbona hujawahi kunisimulia mimi au ndugu zangu wengine?" Akanijibu "Ningekusimulia sa ngapi na ww muda huna,pia naskia role model wako ni Ben Carson? Ambae unajua historia yake tokea anazaliwa hadi anakuwa Neuro Surgeon? " Nikakausha. Akaniuliza unajua leo tarehe ngapi? Nikajbu 8. Hapo ndio nikakumbuka kuwa ni siku ya kuzaliwa ya Mama. Nikajishangaa imekuwaje nikaisahau wakati miaka yote huwa naikumbuka? Sikuongea kitu. Akaniambia kuna maswahibu yamekukuta mpaka yamepelekeaa ww kuwa hapa, unaweza kuniambia?
Nikamwambia hapana, nipo sawa sasa. Nitamwambia nini wakati aliyopitia yeye ni kama bahari nzima, na yangu ni tone tu? Alafu pia nilijaribu kuielewa psychology ya Mzee kwann alianza kunisimulia story yake kabla hata hajasikiliza yangu.
Alivyoona sina cha kuongea akaniruhusu niondoke. Wakati natoka nikajigonga kwenye ncha ya kiti. Sikutaka kugeuka nyuma,ila nikamsikia anasema "Utapewa pole jikoni,ila najua ukifika mjini utapost kuwa umejigonga kwenye kiti" Alaf akaangua kicheko.
* *
Siku moja kabla ya kurudi mjini, Baba ndio alinipatia zile milioni mbili ambazo niliwekeza kwenye tangawizi. Japo sikumuelezea matatizo yangu, ila najua aliyahisi.
Aliniambia yafuataya "Dunia ya leo kila unayemuona anamatatizo yake kiasi kwamba anakosa hata muda wa kukuonea huruma ww. Hivyo unapoongea na watu tegemea sana msaada wao,ila usitegmee huruma yao.
Akaendelea "Huwezi kurudisha fadhila alizokutendea mtu,ila unachaweza kufanya ni kulipiza wema kwa wema.
Akamalizia "Najua utakuwa bize sana,lakini mimi na Mama yako kwa umri tulio nao hatuwezi tena kuongea na simu zaidi hata ya nusu saa,dakika 10 zako kwa siku ukitupigia simu zinatutosha".
Maneno ya mzee yalinigusa sana.
Tukaishia hapo.
Kesho yake niliongea na Mama kiasi,nikawa nagusia kuwa Baba kauzu sana. Mama akaniambia "Toka ujana wake yupo hivyo na ndio njia iliyosababisha akanipata mimi,ni mchekeshaji aliye serious"
Nikajikuta natamani kuijua story ya jinsi Baba na Mama walivyokutana. Kabla sijaondoka nikajaribu kumgusia Mzee ilo swala ,akajibu " Unataka darasa la kutongoza? We ukimpata nipe namba yake,nitamaliza kila kitu" baada ya kuongea hivyo akacheka saaana.
Aisee nilikuwa namiss vitu vingi sana toka kwa Wazazi.
My father,my hero
* *
Nimejaribu kushare na nyie story ya Baba yangu kwavile najua leo hii kuna mtu anapitia msoto,kuna mtu hana muda wa kuzungumza na wazee wake,anakaribia kukata tamaa,anasubiria miaka 3 ijayo ndio aweze kuongea na wazazi wake n.k
Ili niweze kuwagusa hao wote,imebidi niilete kwa mtindo wa story,kinyume na hapo kuna wengine wasingepata huu ujumbe japokuwa wanauhitaji.
Wazee wetu wanavitu vingi sana ambavyo vingekuwa funzo na mwangaza mkubwa kwetu, ila hatuvijui maana hatupati muda nao. Pata muda na wazee wako. Ongea nao kadri unavyopata muda, usisubiri mambo yawe tight kama ilivyokuwa kwangu ndio ukaongee nao.
Tunayopitia sasa, walishapitia. THE BEST MOTIVATION SPEAKERS ARE OUR PARENTS. THEIR LIFE IS OUR DICTIONARY TRUST ME GUYS.
Najuwa kuna madini mzee hajaniambia yote. Kwa jinsi nilivyokaribu nae siku hizi, ntajua kila kitu.
Mimi ni Baba yangu, na Baba yangu ni Mimi.
Naitwa Analyse ,na hiyo ndio ilikuwa safari yangu na Baba yangu.
See You.
#Baharia wa Nchi Kavu.
Nimetingwa kidogo kwasasa. Ila panapo majaaliwa, anytime mwezi ujao nitaweka kisa kingine. Maana ili kutengeneza peace na Mshua, nililazimika kurudi shule, tukapoteza hela nyingi kunirudisha kwenye mfumo, na hata baada ya kumaliza, mambo hayakwenda kama tulivyotarajiaOy bro Analyse Hebu lete another hustling experience kuhusu maisha yakoo
Bro Analyse umepitia safari ndefu. Though na Mimi yangu ni ngumu na ndefu ila maybe nikifanikisha Jambo fulani. Basi nitaweka wazi.Nimetingwa kidogo kwasasa. Ila panapo majaaliwa, anytime mwezi ujao nitaweka kisa kingine. Maana ili kutengeneza peace na Mshua, nililazimika kurudi shule, tukapoteza hela nyingi kunirudisha kwenye mfumo, na hata baada ya kumaliza, mambo hayakwenda kama tulivyotarajia
Sio inshu za kutoboa, ila Kuna mstari sitakiwi kuuvuka kwa Sasa. Ili kulinda maslahi na harakati za Mimi intelli. Bro AnalyseWw tuandikie tu, sio mpaka utoboe. Mimi na hustle zote hizo, still sijatoboa mpaka leo. Share nasi tu 😅😅
[emoji28][emoji28][emoji28] mke yupi mkuu?