Philbert JM
New Member
- Aug 23, 2022
- 1
- 4
"Je nisomee kazi gani itakayonipa ajira kwa haraka?" Limekuwa ni swali ambalo linaleta changamoto sana kwa wanafunzi waliowengi kwani halina majibu ya moja kwa moja. Kutokana na hali ya maisha kubadilika na wasomi kuwa wengi siku hizi, basi ajira zimekuwa ngumu kuzipata. Hali hii imefanya wanafunzi wengi hasa wa vyuo vikuu kujenga dhana akilini mwao kwamba 'ajira hazipo'. Lengo la makala hii ni kupinga dhana hiyo kwa kutoa njia mbalimbali zinazoweza kumsaidia mwanachuo kupata ajira au fursa za ajira kwa wepesi mara tu amalizapo masomo yake.
Kwanza, ni kufanya udahili uliosahihi kwa maana ya kozi sahihi katika chuo sahihi. Baadhi ya wanafunzi hukosea sana katika kipindi cha udahili (application) kwa kuwaachia ndugu zao au marafiki wafanye zoezi hilo kwa niaba yao, hii ni kama kumkabidhi mtu aamue kesho yako. Kipindi cha udahili ni kipindi ambacho mwanafunzi anatakiwa asimamie kutimia kwa ndoto zake (alizoziishi tangu kidato cha nne au sita) kwa kuchagua kozi sahihi na chuo sahihi yeye mwenyewe na si mzazi wake. Tabia ya wazazi au ndugu kuwachagulia watoto wao kazi za kusomea siyo nzuri hata kidogo kwani huondoa morali ya kusoma kwa watoto hao. Mtoto akijichagulia kozi aipendayo atapambana nayo hata kama ni ngumu kiasi gani ili mradi afaulu vizuri, lakini akichaguliwa siyo rahisi kuweka juhudi nyingi wakati wa masomo kwa sababu atakuwa anasoma kwa kulazimishwa na wazazi. Hivyo basi, hatua ya kwanza kabisa ni kuchagua kazi (profession) uipendayo ambayo hata ukija kuipata utaitumikia kwa moyo wako wote na hautajutia kuisomea.
Pili, tafuta GPA iliyoshiba. Kuna dhana inatembea sana vyuoni kwamba "GPA haimati kinachomata ni konection", asikudanganye mtu nawe ukakubali kudanganyika eti ohh gpa haina umuhim katika maisha ya sasa. Chakufanya ni kwamba hakikisha unatumia vizuri muda wako uwapo chuoni kwa kusoma kwa bidii ili kutafuta ufaulu mzuri (GPA kubwa) utakuja kunishukuru baadae. Kuna wakati utafika umetuma maombi yako ya kazi katika taasisi fulani, kutokana na waombaji (applicants) kuwa wengi kuliko nafasi zinazohitajika kitatumika kigezo cha GPA ili kuwapunguza waombaji hao, hapo ndipo joto litakapokupanda wewe mwenye kiGPA chako cha mbili point kadhaa wakati huo wenye gpa zao kubwa watakuwa wakishushia Coca baridi huku wakimshukuru Mungu na kusubiri usahili yaani 'Interview', kwa mantiki hiyo wewe utakuwa umejiengua mwenyewe katika kinyang'anyiro cha kuimega 'national cake' na methali ya "majuto ni mjukuu" itakuwa ikijirudia kichwani mwako kama kanda mbovu kwenye redio kaseti. Nimalize kwa kukuasa usizarau kitu rafiki yangu, uwapo chuoni tafuta GPA kubwa kwani hata ukiipata kubwa kuna hasara gani?
Tatu, tafuta konection za kutosha. Hapa naomba kukwambia ewe mwanachuo kwamba vyeti pekee havitoshi kukupa fursa za ajira, kwa hiyo konection nazo zina nafasi yake. Mtu anaweza kujiuliza hizo connection zinatafutwaje? Ni kwamba, miaka yako mitatu ya kuitafuta "bachelor degree" au shahada ya kwanza ni mingi sana kukukutanisha na watu aina mbalimbali na kutoka sehemu tofauti tofauti. Kumbuka konection zinazotajwa hapa ni watu, hivyo siri ya mafanikio katika konection ni kuishi vizuri na watu. Hautakiwi kuwa na maadui wengi kuliko marafiki badala yake unatakiwa kuwa na marafiki wengi kuliko maadui. Nikupe mfano mmoja halisi, kijana mmoja alikuwa akisoma shahada ya usimamizi wa raslimali watu yaani ''Bachelor of Human Resources Management", alipomaliza masomo alisaidiwa kupata kazi na mwanafunzi mwenzake ambaye baba yake ni mmiliki wa kampuni moja mashuhuri sana hapa Tanzania, kwa maana hiyo mwanafunzi huyo alimkonekt mwenzake kwa baba yake akapata kazi kutokana na kada aliyokuwa amesomea (HR). Naamini endapo watu hawa wangekuwa maadui kipindi wanasoma sizani kama wangepeana huu mchongo wa faida. Basi nawe mwanafunzi wa chuo inatosha kukwambia 'ishi vizuri na watu' maana haujui wanaokuzunguka ni kina nani. Kuna msemo tulikuwa tunapenda sana kuutumia kipindi tunasoma kwamba 'Salimia watu maisha sio magumu kiasi hicho'.
Nne, jifunze kuwa mwaminifu na mwenye juhudi nyingi. Uaminifu ni kitu kizuri sana hata kwenye maisha yetu ya kawaida. Uaminifu shuleni au chuoni humfanya mtu kupata nyazifa mbali mbali ambazo huweza kumwongezea sifa (CV) nzuri. Watu wanaosema hakuna ajira huenda wamekosa sifa ya uaminifu au mojawapo kati ya nilizozitaja na kuwafanya wakose kazi. Kama hakuna ajira mtaani iweje wengine wapate kazi mara tu baada ya kumaliza degree zao? Tazama jinsi uaminifu unavoweza kukupatia ajira; kuna rafiki yangu mmoja alikuwa 'field' (mafunzo kwa vitendo) katika tawi fulani la benki. Katika kipindi chote cha field yake alikuwa mchapakazi sana na mwaminifu kwa boss wake na wafanyakazi wote wa benki hiyo.
Alivomaliza field aliondoka kurudi chuoni kumalizia masomo yake, na mara tu alipomaliza masomo kisha kutunukiwa cheti chake, aliitwa na ile benki na sasa ni mfanyakazi wa benki hiyo. Wito wangu kwa wanachuo, tujiangalie sana tuwapo field kwani huwa tunachunguzwa bila ya sisi kujua. Kwa mfano kuchati au kuongea na simu kwa muda mrefu wakati wa kazi ni miongoni mwa tabia ambazo haziwapendezi maboss wetu. Tujichunge.
Tano, tuwe na imani na tumshirikishe Mungu. Kumwamini Mungu ni jambo la muhimu sana kwa sababu unaweza ukawa umekidhi kila sifa na bado usipate kazi, hii ipo kwa ajili ya kutekeleza usemi usemao "mgawa riziki ni Mungu pekee" yeye ndiye mpangaji na mpanguaji wa maisha yetu. Japo kutegemea muujiza wa Mungu pekee bila kufanya kazi hakuwezi kukupatia mafanikio kwani hata Mungu mwenyewe anatusisitiza tufanye kazi na anatusisitiza kumshika sana elimu.
Shida ambayo watu wanakosea ni kujifungia kila siku chumbani kwa kusali na kuomba wapate kazi nzuri na mafanikio bila ya kujishughulisha kufanya kazi wala kutafuta fursa, nikwambie tu rafiki yangu Mungu hayuko hivyo kwani aliyenacho ataongezewa na wewe unayekaa kusubiri muujiza wa roho mtakatifu utasubiri sana mwisho utaishia kulaumu kwamba mtaani hakuna ajira kumbe wewe ndio haupo mtaani.
Hitimisho, napenda kutoa ushauri kwa wanafunzi wote kuanza kujenga ndoto hivi sasa na kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto hizo. Niwasihi pia wazazi kutowalazimisha watoto wao kufanya vitu ambavyo haviko katika mapenzi yao na badala yake watoto wasikilizwe na wazazi wawe wasimamizi na washauri wa kwanza katika kuhakikisha ndoto za wanao zinatimilika.
Mtaani kuna fursa, suala muhimu ni jinsi gani umejiandaa kukabiliana na uchache huu wa ajira huku ukimshirikisha muumba wako. Kwa kufanya hivyo tutaweza kutimiza ndoto zetu na kuwa msaada kwa familia zetu, jamii zetu na hatimaye taifa letu kwa ujumla. NANI KASEMA KAZI HAKUNA? AHSANTE.
Upvote
3