Asante,
Kwanza kabisa tujue misamiati haramu na dhambi, pili tujue pombe, kisha tatu tujue Mtume Muhammad (hadithi) na Quran halafu mwishoni kabisa tumalize kwa kujibu swali lako. Nitatumia tafsiri zisizo rasmi ili niweze kueleweka kirahisi kwa baadhi ya vipengele ila maana ni ileile sitatoka nje ya Sheria ya dini ya kiislam
Haramu
Haramu ni jambo ambalo limekuwa prohibited kwa muumini, yaani amepigwa marufuku kulitenda na akikengeuka basi anakuwa amemkosea Muumba na itamletea madhara yeye (wakati mwingine na jamii yake) duniani na baada ya kufa. Haramu ni mambo mabaya na maovu
Dhambi
Dhambi ni chumo analopata mtu kwa kumkosea Mola wake, yaani ukitenda haramu malipo yake ni dhambi kama ilivyo kwa anayetenda halali (mambo mema na mazuri) malipo yake yakawa ni thawabu. Ikumbukwe uislamu una hukumu kuu Tano na katika hizo, mbili maarufu ni HALALI na HARAMU ambapo ukifanya halali utapata thawabu na ukifanya haramu utapata dhambi
Pombe au ulevi kwenye uislamu ni Kila chenye kuharibu akili na hapa naomba ieleweke kwamba kuharibu siyo kusambaratisha maana wapo wanaojisifu kwamba wanakunywa lakini wanajitambua hivyo pombe Haina shida kwa upande wao, sub'hanaallah! Kuharibu akili ni kufanya mtu awe tofauti na kawaida yake mfano kutembea, kuongea, utendaji, nk
Mtume Muhammad ni mtu ambae alipewa ujumbe wa kuwafikishia binadamu kama ilivyo kwa binadamu waliotangulia kabla ya kizazi chake ambapo walikuwa wakichaguliwa watu miongoni mwao na kupewa maelekezo maalumu ya namna ya kuishi
Kama ilivyokuwa kwa watu (mitume) wengine, Mtume Muhammad nae alipewa muongozo maalumu wa maisha kwajili ya kuufuata yeye na watu wa kizazi chake. Mwongozo huo ndio unaofahamika kama QURAN
Swala likaja sasa kwenye kuuelewa na kuutekeleza huo mwongozo ambapo Mtume Muhammad akawa akilazimika kutafsiri na kuchambua kinaganaga maneno yaliyotumika kwenye huo mwongozo ili kuwarahisishia watu katika utekelezaji wake (hii ilitokana na kwamba kuna mambo mengine yaliyohitaji vitendo zaidi pia mengine yalikuwa ni misamiati mipya katika lughat waliyozoea kuitumia)
Uchambuzi huo na utekelezaji wake aliokuwa akiudemonstrate Mtume Muhammad ndo unajulikana kama mwenendo wa Mtume yaani Sunnah na hadithi. Kwahiyo mtu hawezi kutenganisha suna ya Mtume na maneno ya MwenyeziMungu (Quran na hadithi) kwani hadithi ni mwenendo au utekelezaji wa Quran yenyewe
Majibu ya swali lako
Pombe imekatazwa katika mwongozo wa Quran soma sura ya Tano Aya ya 90 hadi 91. Mwongozo huu haukuacha kitu pia ukatoa na sababu za kuharamisha/kuzuia pombe>>> rejea surah Al baqara Aya ya 219 na surah Al Maida Aya ya 93. Ikumbukwe kwamba haramu au halali zipo ambazo unapewa direct madhara au faida zake, zingine hupati bali unadokezwa tu ili kwa mwenye kuweza kutafiti akatafiti kupata majibu na zingine zipo kwa mkato tu kwamba ni haramu au halali ila utafiti au ukweli wake utauona ukishakufa huko
MwenyeziMungu ndiye mjuzi zaidi