WASSALAM ALEYKUM WARAHMATULLAHI WABARAKATUH. WASSALATU WA SSALAM ALAA RASUULIHI KHAATAMI NNABIYYIYA MUHAMMAD , WA ALAA AALIHI WASAHBIHI AJMIYN
NAFASI YA MWANAMKE KATIKA TAMADUNI TAFAUTI
UTANGULIZI:
Kuna hatua mbili muhimu za kuelewa nafasi ya mwanamke katika Uislamu. Hatua ya kwanza ni kuangalia nafasi ya mwanamke katika tamaduni zisizo za kiislamu. Hatua ya pili ni kufanya somo linganishi baina yao. Tutapofanya hivyo tutagunduwa kuwa:
Uislamu umeipa familia nafasi na umuhimu wa pekee. Mfumo wa kifamilia katika Uislamu unatowa haki kwa mume, mke, watoto, ndugu na jamaa kwa uwiano ulio wazi. Ni mfumo unaopinga tabia za uchoyo, umimi na wivu. Mapenzi ndiyo kiini cha mjengeko wa familia katika mafunzo ya Kiislamu.
Nafasi na haki za mwanamke katika jamii akiwa ameolewa au hana mume imewekwa wazi ikiwa ni pamoja na kumiliki na kutumia mali yake bila ya kuingiliwa au kusimamiwa na yoyote. Bali kwa lengo la kuondosha dhulma, udhalilishaji, unyanyasaji na ukandamizaji kwa mwanamke unaofanywa na tamaduni zisizo za Kiislamu, au waislamu wasiofuata mafunzo ya Uislamu ndiyo mana Mtume SAW akawasisitizia waislamu ubora wa kufanya usawa na uadilifu kwa wanajamii wote kwa kusema katika Hadithi kuwa: ((waliobora miongoni mwenu ni wale walio wema kwa wake zao)) Ibn Majah na Tirmidhi.
MWANAMKE KATIKA TAMADUNI NYENGINE:
Katika Encyclopedia Britannica, 11th ed., vol. 28 pamesemwa: “Katika India, mwanamke kuwa mtegemezi ni jambo la msingi kabisa. Ni lazima mwanamke awe chini ya kinga ya mwanamume. Haki ya kurithi ni ya mwanamume pekee ambaye anahaki ya kumrithi hata mwanamke” Aidha, katika maandiko ya Kihindu, pametajwa kuwa sifa za mke mzuri ni pamoja na hizi zifuatazo: “….akili yake, mwili wake na maneno yake ameyaweka chini ya utegemezi wa mumewe” sifa hizi zimetajwa na Vera katika “Marriage East and West”
Katika Athens, E.A Allen “History of Civilization” pameelezwa kuwa: “Mara zote wanawake wa Athena walikuwa ni wategemezi kwa baba zao, ndugu zao wa kiume au wanaume wengine,… haki yake ya kuolewa haikutiwa maanani, alitakiwa afuate tu matakwa ya wazee wake ikiwa ni pamoja na kupokea mume hata kama hakumjuwa au hakumpenda.
Katika Encyclopedia Britannica pameelezwa tena kwamba “Katika sheria za Roma, mwanamke alikuwa kwa ujumla wake ni tegemezi. Anapoolewa, yeye na mali zake zote zinakuwa za mumewe, ….mwanamke alikuwa ni bidhaa kwa mumewe. Mwanamke hakuwa na haki yoyote ya kiraia”.
Mwanahistoria mkubwa wa Kigiriki, Herodolt ametowa taarifa isemayo kwamba Ashtar alikuwa ni Mungu wa Waforsi wa mapenzi na uzuri. Moja kati ya matambiko kwa dini yao ilikuwa ni kutowa muhanga mwanamke mzuri aliye bikra. Mwanamume yeyote anayetaka kuoa ilikuwa anatakiwa kupeleka kipande cha shaba katika hekalu la mungu huyu na kumchukuwa mwanamke huyo kwenda naye atakako.
Katika ustaarabu wa Kaldonia, mwanamke aliyekuwa hajapata ujauzito muda mfupi baada ya ndoa yake huonekana kuwa amelaaniwa na miungu, Hupelekwa kufanyiwa dawa na asipopata uja uzito anaweza kuuliwa ili roho yake ikastarehe pahala pema.
Katika Misri ya kale, mwanamke alikuwa na aina fulani ya uhuru wa kurithi na kumiliki nyumba wakati mumewe anapokuwa hayupo. Hata hivyo alikuwa hana thamani kubwa kwa vile baadhi ya wanawake walikuwa wakitolewa muhanga kwa miungu na kwa kutupwa katika mto Nile ili uendelee kutowa neema kwa watu wa Misri.
Katika Uyahudi, mwanamke yoyote asiye Muyahudi alionekana ni sawa na mnyama. Kwa hivyo kumuadhibu haikuwa kosa. Mwanamke hakuwa na uhuru wa kukataa tendo lolote analolitaka mume katika nyumba yao. Baba alikuwa na haki ya kumuuza mtoto wake wa kike.
Baadhi ya dini za Ulaya zinaamini kwamba mwanamke ndiye chanzo cha shari na matatizo yote yanayomkumba binaadamu. Hii ni kwa sababu Bi Hawa ndiye aliyekosea kwa kumlaghai Adam hata wakatolewa peponi.
Katika Ulaya kulifanyika mkutano wa kidini huko Ufaransa katika mwaka 586 CE na pakakubaliwa kwamba ukimtowa bikira Maria, wanawake wote si wakamilifu. Miongoni mwa masuali yaliyoulizwa katika mkutano huo ni pamoja na: Je mwanamke ni roho tupu au ana roho na kiwiliwili? Je mwanamke ni binaadamu au hapana? (M. Cisse, 2005, 4). Mwanamke wa Uingereza amepewa uhuru wa kumiliki mali yake mwenyewe Mnamo mwaka 1882 (ibid, 4), Mwanamke wa Ufaransa amepewa uhuru kamili mnamo karne ya 18.
Katika Waarabu wa zamani/Jahilia, mwanamke alikuwa ni alama ya unyonge. Hawakusherehekea anapozaliwa mtoto wa kike. Palikuwa na uhuru wa kumdhalilisha hadi kumuuwa wakati mwengine. Aidha mwanamke anayeachwa hai alikuwa ni sehemu ya rasilimali ya mwanamume, kwa hivyo wajane walikuwa wakirithiwa.
Mwanamume alikuwa na haki ya kuoa idadi yoyote ya wake bila ya kushauri na akitaliki atakavyo bila ya kizuwizi
MWANAMKE KATIKA UISLAMU
Miongoni mwa lengo la Uislamu ni kuwakombowa wale wote waliokuwa wakidhulumiwa. Hata hivyo kwa mnasaba wa mada hii, Uislamu ulikuja na sharia nyingi zilizolenga kumkombowa mwanamke. Kwa hivyo Aya na Hadithi nyingi zimeteremka kwa lengo la kumrejeshea mwanamke haki zake. Baadhi ya mafunzo hayo ya Uislamu ni pamoja na haya yafuatayo:
Usawa wa mwanamume na mwanamke katika malezi:
((ساوو بين أولادكم في العطية، فلو كنت مفضلا أحدا لفضلت النساء)) الطبراني
((Fanyeni usawa baina ya watoto wenu katika upaji/kuwapa, lau ningekuwa wa kumfanya bora mmoja (wao), ningemfanya bora mwanamke)) A-tabrani
((إنما النساء شقائق الرجال)) البراز
((Kwa hakika wanawake ni ndugu (pacha) na wanaume)) Al-buraz
((Yoyote mwenye mtoto wa kike akamlea vyema bila ya kumfadhilisha wa kiume, Mwenyezi Mungu atamuingiza peponi))
((Mwenye kulea watoto wawili wa kike (kwa vyema) mpaka wakakuwa, siku ya kiama nitakuwa mimi nye kama hivi)) Muslim.
Usawa wa mwanamume na mwanamke katika haki mbalimbali:
Haki hizo ni pamoja na hizi zifuatazo:
i) Haki za kijamii
Sharia ya Kiislamu imemtandikia haki muwafaka mwanamke wa Kiislamu akiwa ni miongoni mwa wanajamii. Katika hili Sharia inamuangalia mwanamke kama inavyomuangalia mwanamume, hasa katika upande wa haki, majukumu na wajibu. Haya yanabainishwa na Aya ya 134 ya Suratu Nnisaa inayosema: ((Na watakaofanya vitendo vizuri, wakiwa wanaume au wanawake hali wao ni wenye kuamini, basi hao wataingia peponi wala hawatadhulumiwa hata ugamba wa kokwa ya tende)) Wote ni sawa katika majukumu na haki. Aya nyengine zinazotilia nguvu kuwepo kwa haki hizo ni pamoja na Surat Nnahli aya 97, – Al-Imran aya 195 na Al-Ahzab aya35.
Zifuatazo ni baadhi ya nyanja za kijamii ambazo bila ya ubaguzi, Sharia ya Kiislamu imeweka usawa wa haki kati ya mwanamke na mwanamme.
ii) Haki ya uchumi na kumiliki Mali.
Mwenyezi Mungu anasema:
((Wala msitamani vile ambavyo Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu (kwa vitu hivyo) kuliko wengine. Wanaume wanayo sehemu (kamili) ya vile walivyovichuma na wanawake nao wanayo sehemu (kamili) ya vile walivyovichuma. Na mwombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu)). An-nisaa aya 32
Uislamu umempa mwanamke haki ya kumiliki mali na ukamruhusu kuindeleza mali hiyo kwa njia za halali kama kufanya biashara. Kadhalika ukamuwekea njia za kumiliki mali hiyo kwa kumpa fungu maalumu katika mirathi, kujuzisha kupewa mwanamke zaka, sadaka, hiba na mengine yaliyo halali, (mfano mahari).
Aidha Uislam umeharamisha mwanamke kuchukuliwa mali aliyonayo pasina ridhaa yake kama ilivyokuja katika Suratun Nisaa aya ya 20 na 29, Suratul Baqaraa aya 188.
Pamoja na mwanamke kupewa haki hiyo ya kumiliki mali, Uislamu haujamkalifisha wala kumuwajibisha kutumia mali hiyo kwa kumpa mtu mwengine isipokuwa katika mambo yaliyo ya faradhi, lakini mwenye kuitoa kwa ikhlasi katika njia za kheri kwa khiyari na ridhaa yake ameandaliwa ujira ulio mkubwa kabisa.
Mwanamke wa Kiislamu ana uhuru kamili na haki ya kutafuta, kumiliki na kutumia mali yake apendavyo kulingana na sharia kama ilivyokuja katika Aya ya 32 ya Nnisaa ((…Na wanawake wanayo sehemu (kamili) ya vile walivyovichuma)). Usawa wa Sharia unajidhihirisha zaidi ulipompa mwanamke uhuru wa kutiliana mikataba na makubaliano ya kibiashara bila ya kuingiliwa na mumewe, baba yake au walii wake. Zaidi ya haki hizo pia ana uhuru wa kumuwakilisha amtakaye kushughulikia mali yake, kuusia, kugaia na kufanya mengineyo ya halali yanayohusiana na mali kama ilivyo kwa mwanamme.
Kwa upande huu wa kumiliki mali, kuna suala moja linalojitokeza ambalo inabidi pia tuliweke wazi kwa mtazamo wa Sharia ili haki itendeke. Suala hilo ni haki ya mwanamke katika mali, vifaa au vitu vilivyopatikana wakati wa ndoa.
Ikiwa palikuwa na makubaliano ya tangu awali (ni vizuri yawe ya maandishi) kwamba wanaingia katika asasi ya ndoa na watakachokichuma ni cha ushirika, hapa mwanamke atakuwa na haki ya mali hiyo kwa kiwango waliochokubaliana.
Ikiwa hapakuwa na makubaliano yoyote baina yao, Sharia inampa haki kila mmoja kumiliki kile alichokichuma tu na kuainishwa kwa jina lake.
Ikiwa mwanamke kwa mfano alikuwa akisaidia kuwapikia mafundi wakati nyumba iliyosajiliwa kwa jina la mumewe inajengwa, au akisaidia kwa mengine kama kukubali kujinyima chakula au kulala pazuri lakini hapakuwa na makubaliano yoyote kuwa alipwe au ana haki katika nyumba hiyo, Sharia hailazimishi mwanamke huyo kudai fidia au haki ya hayo aliyoyafanya. Kufanya hivyo kisharia huitwa hisani ambayo ni vyema pia malipo yake yawe ya hisani. Vivyo hivyo ikiwa aliyesaidia au aliyetumika ni mwanamme katika nyumba au kazi ya mke. Tunachosisitiza hapa ni umuhimu wa mwanamke kujua haki zake mapema ili kuepusha lawama. Si vibaya kisharia pakawa na mkataba wa ndoa ambao unaingiza madai na masharti kama hayo.
iii) Haki ya kupata Elimu na Maarifa, na kuyatumia:
Mwanamke wa Kiislamu ana haki na uhuru kamili wa kutafuta elimu na maarifa na kutumia kwa mujibu wa njia za kihalali. Zipo aya na Hadithi nyingi zinazobainisha hayo. Moja kati ya hizo ni Hadithi ifuatayo ambapo Mtume (SAW), amesema: ((Kutafuta elimu ni faradhi (lazima) kwa Muislamu mwanamume na mwanamke))Bayhaky na Tabaraniy. Pia Mtume (SAW), amesema: ((Anayeulizwa kuhusu taaluma akaificha, atafungwa kamba za moto siku ya kiama)). Ahmad, Abu Daud, Nasai, Tirmidhy na Ibnu Majah. Jambo la msingi hapa ni kusoma elimu kwa nia ya ibada. Nako ni kukusudia kujisaidia mwenyewe, jamii na taifa kimaendeleo katika nyanja zote.
Sharia ya Kiislamu inapomlazimisha mwanamke kusoma na kuifanyia kazi elimu inalenga kwenye elimu za aina zote. Lakini elimu iliyo bora zaidi kwao ni ile itakayowakomboa kimaarifa na kimaisha. Hii ni elimu ya kutambua haki na wajibu wao wakiwa kama mama au wake au ndugu wa kike au wanajamii.
Elimu ya pili ni kuleta maendeleo ya jumla. Sharia haijamkataza mwanamke kufuata elimu popote ilipo. Hadithi ya Mtume (SAW), inasema((Tafuteni elimu japo Uchina (maeneo ya mbali)).Ibnu Abdulbari, Bayhaqiy n.k. wengine wamesema dhaifu. Jambo la msingi hapa ni kufuata taratibu za kisharia zinazolinda heshima. Kama kutakuwa na udhamini unaoaminika kisharia mwanamke anaweza kwenda masomoni popote. Kinachosisitizwa na Sharia ni kwa mwanamke kujua haki na wajibu wake na kufuata taratibu kama hizo za walii.
iv) Haki ya kufanya kazi:
Sharia ya Kiislamu inamhimiza mwanamke kujitahidi kufanya kazi za halali ili apate chumo la halali hasa pale anapokuwa hana mtu anayelazimishwa na Sharia kumhudumia kwa kumtimizia mahitaji yake (kama baba, mume, ndugu wa kiume au walii mwingine n.k). Hata pale wanapokuwapo hao, pia hakatazwi kufanya kazi lakini mhimizo wa hapa si kama ule wa mwanzo. Mana kule mwanzo unafikia kuwa ni wajibu.
Faida ya elimu tuliyoizungumza hapo juu na ule uhalisia wa kumiliki mali unapatikana na kudhihirika matunda yake kwa kufanya kazi. vipi utamiliki bila kufanya kazi? Na vipi utafanya kazi kwa mafanikio bila ya maarifa ya kazi hiyo na taaluma yake? Mtume (SAW), amesema((Hakika Mwenyezi Mungu anapenda mmoja wenu akifanyakazi aifanye vyema/ kwa ustadi)) Bayhaqiy. Mifano ya Waislamu wanawake wa mwanzo waliofanya kazi ni wengi. Kazi walizofanya ni pamoja na udaktari, ualimu, ulinzi ukusanyaji kodi n.k. kwa hivyo Sharia inamruhusu mwanamke kufanya kazi yoyote ambayo ni ya halali inayoendana na maumbile yake, huku akichunga mipaka mingine ya ibada za maadili, mavazi, heshima na utu unaokubalika katika Sharia.
v) Haki ya kuheshimiwa:
Lengo la Sharia ya Kiislamu ni kuchunga heshima za binaadamu wote pamoja na kulinda haki za viumbe wote. Sharia inatambua vyema na inapigania heshima na utu wa mwanamke katika jamii, hasa kwa kuzingatia jukumu kubwa alilokabidhiwa la kubeba mafanikio ya jamii nzima. Mwanamke ni nusu ya jamii. Sharia imempa aula ya juu kabisa. Ndiyo mana mama amempita baba mara tatu kwa kustahiki heshima ya mtoto. Zaidi ya hayo Sharia inapozungumzia haki ya kuheshimiwa mwanamke inamaanisha utekelezaji wa hatua maalumuu zinazofikisha kwenye heshima hiyo. Miongoni mwa hatua hizo inabidi zichukuliwe na zifuatwe na mwanamke mwenyewe, nyengine zitekelezwe na wanaume na nyengine na jamii. Kwa mnasaba wa kazi hii, tunajaribu kuangalia mambo yafuatayo yatayopelekea heshima na haki ya mwanamke ya kuheshimiwa.
Kujistiri kwa mavazi yanayokubalika na Sharia (Hijabu) Mwenyezi Mungu ameumba kila kitu mbeya mbili mume na mke. Kila mmoja anavutiwa mno na mwenzake. Mwenyezi Mungu amewatia jazba ya mapenzi kati yao. Jazba hiyo ingeachiwa tu bila ya kuwekewa mipaka ingeondosha uwiano wa kibinaadamu na unyama ungetawala. Hali hiyo ingepelekea kwenye kosa jengine la kukaribia zina au kuzini kabisa, hasa pengine na watoto au na wake za watu. Heshima ingekuwa imekufa kabisa.
Kwa mantiki hiyo, Sharia ya Kiislamu imefaradhisha sitara ya hijabu kwa mwanamke ili apate heshima zaidi. Sharia hiyo ilitanguliwa na kukatazwa kuangalia yasiyo halali yanayoamsha mori wa hisia za zina, imeamrisha kustiri tupu na pia kutoregeza sauti au kujiregeza katika mwendo au kufanya jambo lolote litalopekelea kuibua hisia za jinsi na hatimaye kuondosha heshima ya mwanamke na ya jamii. Katika kuchunga heshima hizo Sharia imeangalia na kuweka mipaka ya namna ya kuchanganyika baina ya wanawake na wanaume. Katika kuchunga heshima na stara ya mwanamke, Mwenyezi Mungu amewaamrisha wote kila mmoja achukue hadhari. Aya ya 30 na 31 An-nur ((Waambie Waislamu wanaume wasitizame yaliyokatazwa na wazilinde tupu zao, hili ni takaso (heshima) kwao………)) (( Na waambie Waislamu wanawake wasitizame yaliyokatazwa, na wazilinde tupu zao, wala wasidhihirishe viungo vyao isipokuwa vinavyodhihirika (uso , vitanga vya mikono – nyayo!) na waangushe shungi zao mpaka vifuani mwao, na wasionyeshe mapambo yao ila kwa waume zao………………)) Ahzab aya 59.
vi) Kuhifadhiwa Siri.
Sharia ya Kiislamu inasema kuwa “Ukamilifu ni wa Mwenyezi Mungu, Mitume wameepushwa na ufanyaji makosa, watu wa kawaida wanaweza kutahiniwa kwa makosa (au na aibu). Kuna kauli nyengine ya kisharia isemayo “Binaadamu (wote) wanafanya makosa, na wabora wa wafanayao makosa ni wanaokubali makosa na kutubia”.
Hali ya kumstiri aliyefanya makosa, hasa aliyetubia inapendezeshwa katika Sharia. Kwa upande mwengine Sharia inaamrisha tuwasiri waliofanya makosa wakatubia, bali pia tuwastiri kuwatolea aibu zao za kimaumbile Mtume (SAW), anasema ((Anayemstiri Muislamu mwenzake atasitiriwa na Mwenyezi Mungu siku ya Kiama)).Bukharina Muslim, Ahmad, Abu Daud, tirmidhiy, Ibnu Majah.
Sharia inahimiza kuhifadhiana siri za ndani ya nyumba (umbo, sura, harufu n.k.).
vii) Haki ya kushirikishwa:
((…Na saidianeni/shirikianeni katika wema na ucha Mungu, wala msishirikiane katika dhambi na uadui …)) Al-Maidah Aya 2
Haki hii ya kusaidiana kimawazo na kifikra na kushauriana kwa kuwashirikisha wanajamii wote wakiwemo wanawake ni katika mahimizo ya Sharia ya Kiislamu. Jambo la msingi hapa ni kumshirikisha kila mwenye uwezo katika jambo alilo na uwezo nalo.
Katika siku za mwanzo za Sharia ya Kiislamu, wanawake walikuwa wakishirikishwa katika nyanja zote za maisha ikiwemo kazi za ulinzi wa dola, kazi za kuelimisha umma kazi za biashara na nyenginezo.
Uislamu unakataza kabisa kuwatenga watu kwa misingi ya rangi, kabila au jinsi zao. Mtume (SAW), anasema ((Nyote nyinyi asili yenu inatokana na Adam ambaye anatokana na udongo…..)) Bazar. Kwa maana hiyo hakuna kumbagua yoyote au kumtenga Muislamu yoyote kwa sababu yeyote.
Haki hii ya kushirikishwa inajumuisha haki nyengine muhimu zikiwemo.
viii) Haki ya kutoa rai na maoni na kusikilizwa
Wanawake wa mwanzo katika uislamu walikuwa wakishiriki katika mikutano ya kuchangia maendeleo ya dola na maendeleo yanayohusu sekta ya wanawake hususan. Katika mkutano mmoja (wa siku ya ijumaa) uliofanyika Msikitini Madina, mwanamke mmoja alisimama na kutoa rai yake ambayo ilikuwa inapingana na rai ya Sayyidna Omar bin Khatab ya kuweka kiwango maalumu cha mahari kwa kila mwanamke. Kwa maana hiyo Uislamu unathamini rai za kila Muislamu, hasa aliebobea katika fani anayoitolea rai bila ya kuangalia ikiwa ni mwanamke au ni mwanaume.
ix) Haki ya kuthaminiwa na kushauriwa.
Hii ni amri iliyokuja katika. Mwenyezi Mungu anasema ((…Na wanashauriana katika mambo yao…)) Ash-Shuura aya 38. Kwa mantiki hii, mwanamke ana haki ya kushauriwa na kuthaminiwa maoni yake katika mambo yote yanayomhusu binafsi, jamii na taifa zima. Ni lazima ashauriwe katika mambo yote yanayohusu uendeshaji wa nyumba zao, watoto wao na waume wao. pia wana haki ya kushauriwa katika mambo yanyohusu mustakbali wa nchi yao. Mwenyezi Mungu anasema ((…Na ushauriane nao katika mambo)). Al -Imran Aya 159
x) Haki ya kuishi na kuwa hai:
Sharia ya Kiislamu inautaja uhai kuwa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni haki ya mtu itokayo kwa muumbaji. Kwa hivyo hakuna yoyote mwenye ruhusa ya kuondosha uhai wa mwengine kimwili au kiakili. Amri hii imekuwa inalindwa zaidi kwa wanawake ambao kihistoria walikuwa wakinyimwa uhai wao kabla ya Uislamu.
Ni haramu kujitoa roho, kujinyonga na kudhulumiwa uhai kwa sababu yoyote iwayo isipokuwa ya kisharia. Mwenyezi Mungu anasema ((…Wala msijiue wala msiue wenzenu…)). Annisaa aya 29. Kwa hivyo haifai kumtesa mwanamke, kumpiga, kumjeruhi, kumpoozesha au kumtia maradhi.
xi) Haki ya kufurahia maisha/uhai:
Sharia ya Kiislamu imefungamanisha haki ya kuishi na haki ya kufurahia maisha. Mwenyezi Mungu anasema. ((…Sema: Ni nani aliyeharamisha (aliyekataza) mapambo ya Mwenyezi Mungu ambayo amewatolea waja wake. Na nani aliyeharamisha vitu vizuri katika vyakula? Sema: “Vitu hivyo vimewahalalikia Waislamu hapa katika maisha ya dunia na vitakuwa vyao peke yao siku ya Kiama)). Al-Aaraf aya 32
Mwanamke kama mwanamme anatakiwa aifanyie kazi dunia kama ataishi milele. Pia Mwenyezi Mungu anapenda amuone mwanamke anatumia riziki alizompa vizuri na kwa manufaa ya dunia yake na akhera. Kwa hivyo hapana sharia inayoruhusu kumzuilia mwanamke starehe za halali zisizopingana na mwenendo wa uislamu.
xii) Haki ya Uhuru wa Kuamini:
Binaadamu wote akiwemo mwanamke wameumbwa na Mwenyezi Mungu na akapewa akili na uwezo wa kupambanua mema na mabaya. Ameoneshwa njia na kaachiwa uteuzi. Mwenyezi Mungu anasema ((Kwa hakika tumemuumba mtu kutokana na mbegu za uhai, zilizochanganyika ili tumfanyie mitihani. Kwa hivyo tukamfanya ni mwenye kusikia na mwenye kuona. Hakika sisi tumemuongoa/tumembainishia njia mbili ya kheri na ya shari. Basi yeye mwenyewe tena atakuwa mwenye shukurani au mwenye kukanush)) Addahar aya 2-3.
Kwa hivyo mwanamke asilazimishwe kuwa lazima afuate kundi fulani ikiwa la mumewe la baba yake au la viongozi. Mwenyezi Mungu anasema🙁(Hakuna kulazimishwa mtu kuingia katika dini (imani)) Albaqarah aya 256. Mwenyezi Mungu angetaka dunia nzima ingekuwa katika Uislamu.
xiii) Haki ya kuwa na maoni tofauti:
Sharia ya Kiislamu inabainisha kwamba kuwapo kwa tofauti ya mambo duniani ni katika kufanikisha raha na maslahi ya dunia. Kwa hivyo rangi, kabila, mawazo na tafauti ya maoni ni mambo yaliyoletwa na Mungu ili kuthibitisha kuwapo kwake na kwa lengo la kunufaisha wanadamu. Mwanamke anaruhusiwa kwa hivyo, na ni haki yake atowe maoni yake japo yanatafautiana na walio na mamlaka kwake. Mwenyezi Mungu anasema: ((Na kila (umma) kati yenu binaadamu tumejaalia sharia yake na njia yake)) Almaida aya 48. Siyo dhambi kwa mwanamke kuwa na maoni yake juu ya maendeleo. La msingi ni kuwa na dhamira iliyo ndani ya misingi ya Uislamu.
xiv) Haki ya Usawa (wa Kijamii)
Mwenyezi Mungu anasema: ((Enyi watu! Kwa hakika tumekuumbeni nyote kwa yule yule mwanamume mmoja na yule yule mwanamke mmoja………… Hakika ahishimiwaye sana miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchaye Mungu zaidi)). Al-hujraat aya 13
Kwa mantiki ya aya hiyo, watu wote kiasili ni sawa katika ubinaadamu wao, tafauti yao itakuwa mbele ya Mungu katika uchaji. Hakuna mbora kwa kabila, jimbo, nasaba au jinsi. Hata hivyo katika upande wa kibaiolojia zipo tofauti za kimaumbile ambazo zikiheshimiwa na kuthaminiwa ndipo ule usawa wa asili wa kijamii hufanyakazi, Sharia inakataza kumdhalilisha mwanamke kutokana na misingi yoyote ikiwemo ile ya kijinsi.
xv) Haki ya kufanyiwa Uadilifu:
Mwenyezi Mungu anasema: ((Kwa hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha uadilifu na kufanya hisani……)) Annahl aya 90
Sharia ya Kiislamu hapa inawataka wanajamii wafanyiane uadilifu wakati wote. Wanapotoa ushahidi au hata wanapohukumu. Kwa hivyo kuwasingizia baadhi ya wanawake kuwa wazinzi au kuwatupia sifa mbaya si uadilifu. Pia kuwa na mke zaidi ya mmoja na akafadhilishwa na kupendelewa mmoja si uadilifu. Vile vile kuwa na watoto wa kike na wa kiume wakafadhilishwa na kupendelewa wa kiume inavunja uadilifu.
Hiyo ni mifano tu ya haki mbali mbali ambazo mwanamke wa Kiislamu amepewa na Uislamu ambapo katika tamaduni nyengine zinakosekana