Pole sana kwa magumu unayoyapitia. Bila shaka wewe bado ni kijana. Nimeumia sana moyoni, nikifikiria kama labda ni mtoto wangu angeweza kufikia hatua hiyo!!
Ingekuwa inawezekana, ningependa kujua zaidi: Je, ni nini kimekufanya kufikia hatua hii? Je, ni kuhisi familia na ndugu hawakupendi na kukuthamini? Je, ni ugumu wa maisha? Je, labda umefanya jambo unaloona limekutia sana aibu mbele ya unaowafahamu? Au unalazimishwa kuishi maisha usiyoyataka?
Lakini vyovyote iwavyo, ufahamu kuwa wewe ni mtu mwenye thamani kubwa sana mbele za Muumba wako, na kuna wengi wanakupenda na kukuthamini, japo yawezekana wengine hata huwafahamu. Ufahamu kuwa hata katika magumu, kuna wakati humea mema. Unaweza kupitishwa katika magumu ili akili yako iamke, ufanye uamuzi fulani, na huo uamuzi utakuondoa katika masikitiko, mahangaiko na hali ya kukata tamaa.
Ninachokusifu sana hukukaa na uamuzi wako moyoni, badala yake ukaamua kutushirikisha.
Kiufupi, kama unaona hali uliyofikia ni muhimu kujitenga, basi huna haja ya kufikiria kwenda mbali sana, huna haja ya kwenda Gaza au Burundi, wala Zimbabwe. Nchi hii ni kubwa, waweza kwenda mkoa mwingine, lakini ufanye hivyo kwa umakini, maana usije ukaenda ugenini halafu majuto yakawa magumu zaidi, ukaishia kukata tamaa.
Naomba utusaidie zaidi: upo mkoa gani? Una umri gani? Wewe ni wa jinsia gani? Kazi gani una uwezo wa kuzifanya? Wazazi wako wote wapo hai? Wanafanya shughuli gani? Una ndugu wengine katika familia, kama vile wadogo zako na wakubwa zako? Ni muumini mzuri wa dini (ukristo au uislam)?