HUENDA safari za kwenda mikoani kwa mabasi zikapungua endapo Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra) itaridhia maombi ya Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo Mikoani (Taboa).
Taboa inapendekeza nauli ya mabasi hayo ipande kwa asilimia 100 kwa kile inachodai ni ongezeko la gharama za uendeshaji, lakini inapingwa na Baraza la Watumiaji wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra CCC).
Katika maombi yake, Taboa imeambatanisha mchanganuo wa ongezeko la gharama za usafirishaji na mapendekezo ya nauli yaliyoainishwa katika madaraja matatu yakionesha
ongezeko hilo kwa kila daraja.
Sumatra CCC kwa upande wake inashikilia nauli hizo zibaki kama zilivyo kwa maelezo kuwa hakuna gharama zilizoongezeka.
Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa Sumatra, Ahamad Kilima, alisema jana kwenye mkutano wa wadau, mapendekezo yao yanataka nauli ipande kwa Sh 69.86 kwa kilometa kwa kila abiria kutoka Sh 26.60 kwa kilometa ya sasa kwa mabasi ya kawaida, ongezeko ambalo ni sawa na asilimia 163.
Alisema kwa mabasi ya Semi Luxury, walipendekeza Sh 97.59 kwa kilometa kutoka Sh 40.70
ambalo ni ongezeko la asilimia 140.
Kwa mabasi ya anasa walipendekeza Sh 113.71 kwa kilometa kwa kila abiria kutoka Sh 46.40 ya sasa ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 142.
Alitoa mfano wa mabasi ya Dar es Salaam-Arusha ambayo nauli ya sasa ni Sh 16,400 mabasi ya kawaida na kutaka iwe Sh 43,000.
Pia kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya Sh 22,000 iwe Sh 58,000.
Akisoma mchanganuo huo mbele ya wadau wa usafirishaji, Katibu wa Taboa, Wilbard Mtenga, alielezea baadhi ya gharama hizo kuwa ni mishahara ya wafanyakazi wanne ambayo ni Sh milioni moja, riba kwa mikopo kwa ununuzi wa mabasi ambayo ni asilimia 19, ununuzi wa matairi na mengineyo ambayo gharama zake zilioneshwa kwa mwezi na mwaka.
Mwenyekiti wa Sumatra CCC, Gilliard Ngewe, alisema wamefanya utafiti makini kwa kupitia mikoa kadhaa kwa mabasi aina ya Scania na ya kichina ya Yutong na kugundua kuwa nauli inapaswa kuongezeka na kuwa Sh 29.75 kwa kilometa kwa mabasi ya kawaida.
Alitoa mfano wa nauli ya Dar es Salaam-Mbeya kwa basi aina ya Scania ambayo nauli ni Sh
22,200, akapendekeza iwe Sh 24,778 ambapo ongezeko ni Sh 2,500.
Alisema kwa Yutong, nauli ya Dar es Salaam - Mbeya inapaswa kupungua kwani ilitakiwa kuwa Sh 28.51 kwa kilometa ambayo ni Sh 23,749 badala ya nauli ya sasa ya Sh 33,900.
Kutokana na takwimu hizi thabiti kutoka kwa watoa huduma wenyewe, sisi tunaona nauli zibaki kama zilivyo, ili kupata muda wa kuangalia mwenendo wa upatikanaji wa mabasi nafuu yenye ubora katika barabara zetu, alisema Ngewe.
Mwenyekiti wa Taboa, Mohammed Abdulla, alisema mapendekezo hayo waliyatoa mara ya mwisho mwaka 2008 wakati gharama zilipopanda kwa asilimia 20 tofauti na walivyokuwa wakiomba.
Mshauri wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Wilson Mashaka, alipinga ongezeko la nauli kwa kiasi hicho kwa kuwa miaka ya nyuma walikuwa wakidai ongezeko la nauli kutokana na mfumuko wa bei ambao sasa hadi asilimia 5.5.
Katibu wa Umoja wa Madereva Waendao Mikoani (UWAMADA), Salum Abdalla, alisema wamiliki hawana umoja wa kudai kupanda nauli, kwani kila mmoja anajiamulia yake kutokana
na gharama.
Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Israel Sekirasa, alisema wamepokea mapendekezo hayo na watayafanyia kazi na kutoa uamuzi mwezi huu baada ya kupokea maoni ya wadau Januari 15.