Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imesema kuwa inatarajia kutangaza viwango vipya vya nauli nchi nzima kuanzia Januari 31, mwaka huu. Hayo yalibainishwa wakati wa kikao cha pamoja baina ya Sumatra na wadau wa usafirishaji Mkoa wa Tanga mwishoni mwa wiki wakati wakitoa mapendekezo yao kuhusiana na viwango vipya vya nauli.
Meneja Ufundi na Usalama Barabarani wa Sumatra, Aaron Kisaka, alisema hatua hiyo inafuatia maelekezo ya sheria ya Sumatra namba 13 inayoruhusu mamlaka hiyo kutafuta maoni, habari na kufanya uchunguzi wa viwango vipya vya nauli vinavyoweza kutumika kwa maslahi ya wasafiri na wasafirishaji.
Alisema utaratibu wa Sumatra katika kubadili viwango vipya vya nauli unafanyika mara moja kwa mwaka au pale ambapo faida juu ya mtaji inakuwa chini ya asilimia tano au chini ya asilimia 25 na kwamba kufikia mwisho wa mwezi huu, mamlaka yake itakuwa imetangaza viwango vipya vya nauli, lakini akasema kuwa viwango hivi vinazingatia pia ubora wa miundo mbinu ya barabara husika.
Nao wadau wa usafirishaji wa Tanga waliohudhuria kikao hicho ambao ni Muungano wa Wasafirishaji Abiria Tanga (Muwata) na Umoja wa Wenye Mabasi Mkoa wa Tanga (Taboa), walisema kuwa ombi la kutaka kubadili viwango vya nauli ni kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji katika utoaji huduma.
Wasafirishaji hao walisema wamekuwa katika wakati mgumu kumudu mfumo wa utoaji huduma kutokana na kupanda maradufu kwa bei ya mafuta siku hadi siku, kuongezeka kwa bei ya vipuri, soko huria la vyombo vya usafirishaji sambamba na upandaji holela wa kodi mbalimbali nchini.
Tunakubaliana na maelezo yaliyotolewa na wadau wa usafirishaji kwa Sumatra kwa lengo la kuishawishi mamlaka hiyo kuridhia upandishaji wa viwango vya nauli.
Hata hivyo, jambo muhimu linalopaswa kuzingatiwa wakati wa mchakato wa kutafuta maoni ya wadau, ni ukweli wa hali halisi ya usafirishaji nchini.
Ni kweli kwamba gharama za usafirishaji zinapanda mara kwa mara, lakini wapo baadhi ya wasafirishaji ambao hawaelezi ukweli halisi kuhusiana na hali ilivyo katika sekta ya usafirishaji.
Baadhi yao wamekuwa wakieleza kuelemewa na gharama hasa kupanda mara kwa mara kwa bei ya mafuta, ingawa wakati mwingine wanachokizungumza hakiendani na hali halisi.
Tatizo lililoko ni kwamba wasafirishaji wengi wanataka kupata faida kubwa kuliko hali halisi ilivyo.
Wasafirishaji kadhaa wa mabasi hasa yanayotoa huduma katika miji kwa mfano katika jiji la Dar es Salaam, wamekuwa wakikaidi kutoza viwango vya nauli vilivyopangwa na Sumatra kwa madai kuwa wanaingia gharama kubwa za uendeshaji.
Hali hiyo inashangaza kwa kuwa Sumatra kabla ya kupanga viwango vya nauli, hufanya utafiti pamoja na kukusanya maoni ya wadau hivyo, viwango vya nauli inavyopanga vinaenda sambamba na hali halisi.
Kwa kuwa Sumatra imesema kuwa itaendelea kukusanya maoni ya wadau katika mikoa mbalimbali nchini, itakuwa vizuri ikiwa mamlaka hiyo itashauriana na wadau hao kuhusiana na namna ya kila upande kutekeleza makubaliano yatakayofikiwa kwa lengo la kuwawezesha wasafirishaji kutoa huduma bora kwa wateja.
Inabidi ufike wakati wasafirishaji watoe huduma kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu bila kusubiri kubanwa na mamlaka husika.
Itakumbukwa jinsi wenye daladala na mabasi walivyokuwa wakilalamika kutokana na kubanwa na kampuni ya uwakala ya Majembe Auction Mart kuhusiana na kukiuka sheria za barabarani.
Tunaamini kuwa mashauriano yanayoendelea baina ya wadau wa usafirishaji na Sumatra yataleta mwafaka kabla viwango vipya vya nauli kutangazwa.
Ni matarajio yetu kuwa viwango vipya vitapangwa kulingana na hali halisi iliyopo na bila kuwaumiza wananchi ambao kila wakati wanaendelea kubeba mzigo kutokana na kupanda mara kwa mara kwa gharama za huduma na bidhaa.
CHANZO: NIPASHE