Katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya wanasiasa na wanauchumi wa nchi za Magharibi ikiwemo Marekani wamekuwa wakichochea makampuni ya Magharibi “kutengana na China”. Kuna baadhi kauli kama “kuporomoka kwa uchumi wa China”, na “tishio la China”, ambazo hazina msingi wowote, na bila ya kujali ukweli wa ushirikiano kati ya uchumi wa China na dunia.
Kuchochea “kutengana na China” kunatokana na fikra ya baadhi ya watu wa Magharibi, kuwa mafanikio ya upande mmoja ni hasara kwa upande mwingine. Watu hao hawawezi kuvumilia mafanikio ya China ambayo ina mfumo tofauti wa kisiasa na kijamii na nchi za Magharibi, wakichukulia China kama mshindani badala ya mshirika, na kutumia “kutengana na China" kama silaha mpya dhidi ya maendeleo ya China. Mtafiti mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Marekani na China Surabh Gupta amesema, nchi chache za Magharibi zinahimiza “kutengana na China” ili kuzuia maendeleo ya China, kitendo ambacho kinafanana sana na jinsi zilivyofanya wakati wa Vita Baridi.
Wakati huohuo, uhusiano wa uchumi na biashara kati ya China na nchi za Magharibi unazidi kuimarika. Kulingana na takwimu za Idara Kuu ya Forodha ya China, thamani ya biashara kati ya China na Marekani ilifikia karibu dola bilioni 700 za Kimarekani mwaka 2021, ambalo ni ongezeko la asilimia 20.2 ikilinganishwa na mwaka 2020, huku biashara kati ya China na nchi za Ulaya ikifikia dola bilioni 738 za Kimarekani mwaka 2021, na kuifanya China kuendelea kuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Umoja wa Ulaya.
Kauli ya “kutengana na China” imepingwa na wataalam wa nchi mbalimbali zikiwemo nchi za Magharibi. Mwanauchumi mashuhuri wa Marekani Jeffrey Sachs amebainisha kuwa, kauli hiyo inatoa wazo lisilo sahihi, na inakwenda kinyume na mahitaji halisi ya dunia. Amesema kwa muda mrefu, maendeleo ya China ni “chanya sana”, na nchi za Magharibi hazipaswi kuweka shinikizo kwa China katika nyanja za teknolojia na biashara, au hata kupiga kelele za “kutengana na China”, badala yake, zinapaswa kushirikiana kikamilifu na China ili kupata mafanikio ya pamoja.
Mkurugenzi wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Abuja, Nigeria Sherif Ghali, anaamini kwamba ushawishi wa China unaendelea kuongezeka, na nafasi yake katika mnyororo wa ugavi wa kimataifa haiwezi kubadilishwa, hivyo “kutengana na China” ni ndoto isiyoweza kutimia. Amesema maendeleo ya China yameendelea kuongeza sauti ya nchi zinazoendelea, na kuufanya utandawazi wa dunia kuwa wa haki na shirikishi zaidi. Amesisitiza kuwa “kutengana na China” kunamaanisha kujitenga na fursa na kujitenga na siku za baadaye.
Binadamu wana hatma ya pamoja. Badala ya kupingana na kutengana, nchi mbalimbali duniani zinapaswa kushirikiana zaidi ili kupata maendeleo ya pamoja.