KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amewataka Watanzania kuwaombea wanaofanya ubadhirifu na wezi ili roho hizo za kuhujumu nchi ziwatoke.
Amesema haiwezekani Rais Samia anahangaika kutafuta fedha ndani na nje ya nchi usiku na mchana na kuzishusha chini halafu hazitumiki kama ilivyokusudiwa, akatolea mfano wa mtu kuongeza idaidi ya manunuzi kuliko kinachohitajika bila aibu.
========
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amewataka Watanzania kuwaombea wenye roho za wizi, ubadhirifu ili ziwatoke.
Amesema haiwezekani Rais Samia Suluhu Hassan anahangaika kutafuta fedha ndani na nje ya nchi usiku na mchana na kuzishusha chini halafu hazitumiki kama ilivyokusudiwa.
Akizungumza jana na wananchi Korogwe, mkoani Tanga, Balozi Nchimbi alisema sehemu inayohitaji mifuko 10 ya saruji mtu anaweka miwili bila hata aibu.
Balozi Nchimbi ambaye yuko ziarani kutembelea mikoa mitano, aliwaomba Watanzania wamwombee Rais Samia kwa kuwa anaipenda nchi na kuitumikia kwa upendo na kujitolea kutafuta fedha, kuzisimamia zikusanywe sawasawa ili kujenga taifa.
Alisema Rais Samia anasimamia kutafuta fedha za mikopo na misaada kutoka nje na inashuka chini.
“Kuna baadhi ya viongozi Afrika ambao wakienda kuomba misaada au mikopo au kukusanya fedha, anagawana yeye na familia yake. Ziko nchi ambazo fedha za serikali kuu hazijawahi kufika chini miaka 20 imepita.
“Lakini Rais wetu anasimamia anasukuma zinakwenda kufanya kazi za maendeleo wajibu wetu ni kumwombea Rais wetu, ili aendelee kufanya kazi hii kwa upendo kama anavyofanya sasa, vilevile tuwaombee wasaidizi wake,” alisema.
Nchimbi aliwataka wananchi wawaombee Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi na waandisi na wale wenye roho za wizi waombewe roho hizo zitoke.
Akizungumza na wananchi wa Hedaru, mkoani Kilimanjaro, Balozi Nchimbi alisisitiza umoja na mshikamano wa taifa kwamba amani na utulivu vilivyopo havijaokotwa bali vimetengenezwa na kufanyiwa kazi na wazee na viongozi, wakiwamo waasisi wa taifa. Aliwakumbusha wananchi kuhusu kulinda amani ya nchi.
“Ninataka kusisitiza, kinachovuruga amani sehemu yoyote duniani ni ndimi zetu, kutochagua maneno ya kusema. Kuna watu wengine huwa wanasema kwanza halafu na kufikiri baadaye. Wengine wanafikiri kwanza ndipo wanasema,” alisema.
Balozi Nchimbi aliwaomba viongozi wote wa siasa kutoka CCM na vyama vingine wanapotekeleza wajibu wao kwa jamii, wanapozungumza na wananchi, wawe wanafiriki kwanza kabla ya kutenda.
“Katika kila wanachosema tafakari maisha ya Watanzania, tafakari utakachosema kitachochea amani au kitachochea uvunjifu wa amani au kitaongeza mtengamano kwa watanzania.
“Wote wana CCM tushirikiane kuongea mambo ambayo hayawachanganyi Watanzania, hayawafarakanishi, hayawagombanishi ili nchi tuliyokabidhiwa na wazee wetu waasisi wetu na sisi tunakabidhi watoto na wajukuu zetu ikiendelea kuwa nchi yenye amani, upendo na mshikamano,” alisema.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPA Amos Makalla, aliwaahidi wananchi kwamba watafanya ziara nyingine na kuzifika wilaya zote.
DAWA ZA KULEVYA
Katika hatua nyingine, CCM imewaonya wauzaji wa dawa za kulevya kuwa wanapanda mbegu ya uharibifu katika taifa na kutoa wito kwa Watanzania kufanya kila linalowezekana kuachana na matumizi ya dawa hizo.
Balozi Emmanuel Nchimbi, alisema hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mwanga, mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kutembelea mikoa mitano.
Nchimbi alisema changamoto kubwa ya wananchi wengi kujikita kwenye matumizi ya dawa za kulevya ambazo zinaua msingi wa ufanyaji kazi kwa vijana.
Alisema vijana wengi kwa sasa wapo kwenye matibabu ya matumizi ya dawa za kulevya na wao hawafiki asilimia 10 ya wale walioathirika.
“Ninaomba wazazi na viongozi wa dini wote mshiriki katika kazi ya kuhakikisha tunafanya kila linalowezekana watoto wetu wanakuwa watoto bora na waandaliwe kuja kulitumikia taifa.
“Njia moja ya kuwaandaa ni kuwapa mazingira mazuri ya na kuwatenganisha na uwezekano wa kuathirika na matumizi ya dawa za kulevya,” alisema.
Balozi Nchimbi alitaka kila mwenye uwezo ambaye anajihusisha na dawa za kulevya ajue anapanda mbegu ya uharibifu katika taifa lake.
Pia alitaka kila mtu apate moyo wa uzalendo wa kulipenda taifa lake na kuacha vitu vinavyoleta madhara ya muda mrefu kwa taifa.
Nipashe