Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,771
- 41,027
Na. M. M. Mwanakijiji
Tunajua sana. Tunajua hata mambo mengine ambayo wanadhania hatujui; tunajua hata yale ambayo wao wanasema ni ya 'siri' au yaliyopigwa mihuri ile myekundi ya "Siri Kubwa". Tunajua yanayofanywa nao maofisini na hata mitaani. Kimsingi, sasa hivi tuna taifa la wanaojua sana.
Kile kinachoitwa "utitiri" wa vyombo vya habari vimetufanya tuwe na uhuru wa kupata habari nyingi na kujua mambo mengi kiasi kwamba tumefika mahali hakuna kinachotushtua tena. Tumekuwa kama tuliopigwa ganzi ya aina fulani kiasi kwamba ili tusikie maumivu inahitajika jeraha kubwa kweli, lakini haya madogo madogo tunashtuka tuna makovu tu hatukumbuki lini tuliiumia na lini tulipona.
Vyombo hivi vya habari vimepita lengo la kutoa taarifa tu na vimekuwa pia vilele vya maoni huru na malumbano ya kijamii na kisiasa. Mengine haya maoni yoyote isipokuwa kutueleza nani kala nini, wapi na kalala na nani! Wenyewe tumeyakubali na kuyaweka kwenye kundi la Udaku.
Tunajua mipango yao mingi "ya maendeleo" kwani imeandikwa kwenye vitabu na nyaraka nyingi. Mipango hiyo ambayo imepewa majina matamu matamu na ya kukumbuka inaelezea kila kitu tunachotaka kujua kuhusu ujenzi wa taifa letu. Fikiria kuna MKUKUTA, MKURABITA, na miradi mingine ya kila aina kwenye wizara na idara mbalimbali. Wakati mwingine nafikiria kuna watu wameajiriwa kuja na hii "miradi".
Tunajua jinsi kashfa mbalimbali zimeligubika taifa letu na wahusika wake wakuu; na siyo tu kujua hivi hivi tunajua kama kwa kukariri. Huwezi kwa mfano kuzungumzia Richmond bila kuzungumzia Dowans; huwezi kuzungumzia Deep Green bila kuzungumzia Meremeta na huwezi kuzungumzia Meremeta bila kugusa Tangold; huwezi kuzungumzia EPA bila ya kugusa Kagoda kama vile usivyoweza kugusa CIS halafu ukaacha kuigusa Benki Kuu. Tunajua nini kimefanyika, wapi kimefanyika, na nani amefanya nini. Na hata pale tusipojua nani amefanya nini tunajua kabisa tukitaka kujua tunaweza!
Tunajua kuwa CCM haiwezi kushinda inavyoshinda hivi sasa kama kungekuwa na kanuni huru na zenye kuweka mazingira sawa ya kiushindani katika ulingo wa kisiasa. Tunajua kuwa hatuna ujanja wa kubadili mfumo huo na hivyo tunajjikuta tunaendelea kushiriki chaguzi zile zile chini ya kanuni zile zile tukitarajia matokeo tofauti. Hata mahali ambapo ni rahisi kushinda kama kusukuma gari mteremkoni tunashuhudi ugumu wa ajabu kiasi kwamba kumsukuma mlevi inakuwa mbinde!
Kwa kweli tunajua sana hadi wakati mwingine inaudhi. Kuna wakati naombea tusijue vitu fulani fulani kwani wakati mwingine kutokujua kunakuzuia usiumie au kujisikia hatia. Kuna vitu binafsi nisingependa kuvijua.
- Nisingependa kujua kuwa Rais wetu anajua kuwa asilimia 30 ya bajeti inaishia mifukoni mwa maafisa wa ngazi za juu!
- Nisingependa kujua kuwa Mwendesha Mashtaka wetu Mkuu anawajua walioiba kwa kupitia Kagoda na anajua kuwa walikuwa wametumwa lakini hawezi kuwachukulia hatua kwa sababu anajua akifanya hivyo atailetea matatizo serikali yake!
- Nisingependa kujua kuwa CCM iliahidi kutafuta suluhisho la mahakama ya kadhi lakini badala ya kufanya juhudi hizo miaka 20 iliyopita inajikuta inatuburuza taifa zima na kuleta mgawanyiko. Tungekuwa na mahakama hizo wakati huo nadhani sote tunajua kuwa kusingekuwa na tishio la baadhi ya viongozi wa Waislamu dhidi ya CCM!
- Nisingependa kujua kuwa viongozi wa kanisa ambao wametoa mwongozo wa kuchagua viongozi bora ndio hao hao wanakuwa wa kwanza kuwaalika viongozi wabovu kwenye shughuli zao za kufungua na kuzindua shughuli za kanisa! Laiti nisingejua jinsi gani walivyo wanafiki!
Kwa kweli kuna wakati mambo mengine nisingependa kujua kabisa. Baada ya ziara ya ka"nzi" Costa Rica na ile ziara ambayo nusura imvunje mbawa zake kule Upanga, amekuja na kunijulisha undani wa Meremeta undani ambao naamini kabisa na kwa kiasi kikubwa naelewa kwanini Pinda ameapa kutoligusa hilo.
Laiti nami nisingejua kile anachokijua Pinda na baadhi ya watu jeshini na serikalini (wabunge hawajui kwa hiyo heri yao!). Bahati mbaya sasa nakijua na kimenifanya nikubali kweli Meremeta ni suala la usalama wa Taifa! Ninaijua Meremeta kuliko habari zote zilioandikwa katika magazeti kuhusu kampuni hiyo na sasa kichwa kinaniuma kama ni bora nijue tu yaishe. Laiti wasingefanya hicho walichofanya kwa kupitia Meremeta labda wengine tusingejua.
Lakini swali linalonisumbua zaidi ni kuwa hivi tunajua ili kiwe nini? Ujuzi wetu wa mambo yanayohusu hali ya nchi yetu, siasa zetu, viongozi wetu unatusaidia vipi? Tunajua mambo haya yote na kupeana taarifa kila baada ya sekunde halafu nini kinafuata?
Je tunajua ili kuridhisha udadisi wetu ili na sisi tuwe miongoni mwa wajuao? Tunajua ili na sisi tuoneshe kuwa tunajua na si mbumbumbu? Tunajua haya yote na mengine mengi tunayoyapata kijiweni halafu yanatubadilisha sisi tuweje? Kama katika kujua kwako hujabadilika kwa namna yoyote sasa si bora kuishi bila ya kujua?
Hili la Meremeta kwa mfano hivi likishatoka na kuwekwa hadharani na kuanikwa juani kama mahindi ya kukobolewa ambayo harufu yake hupeperushwa kwenda mbali na upepo wenye vumbi na watu wakajua halafu kitakuwa nini? Kama wabunge waliamua kutokujua na Spika akakubali wasijue na Waziri Mkuu na Sumari wote wakihakikisha watu hawajui sasa sisi tukilifanya lijulikane tunafanya hivyo kwa faida gani?
Je si bora vingine waendelee kujua hao wachache na sisi wengine tuendelee kujua vile wanavyotaka tujue tu? Na hii ndiyo sababu nyingine ya kuweka mchango kidogo kwenye suala hili ili kuchuja wale wanaotaka kujua isije kuwa tukafanya kitu tukidhania tunafanya la maana kumbe tunaendeleza kupiga watu ganzi?
Je ni lazima watu wote wajue kila kitu au wakati mwingine ni bora wachache wajue kwa niaba ya wengi? Unajua hilo?