Ameandika Baba Askofu Benson Lwakalinda Bagonza
TOZO YA MIHAMALA na KODI YA MAJENGO.
Mwigulu Ayaone haya:
1. Wasamaria wema wamemuokota aliyegongwa na gari barabarani. Wakamkimbiza hospitali. Daktari anataka laki tatu kumtibu. Linaundwa group kuchangisha. Serikali inakata tozo badala ya kulipia matibabu ya raia wake!
2. Wawili wamependana. Wanatualika tule pilau au waoane. Tunachangishana ili kuwapunguzia makali. Serikali inakata tozo badala ya kuwachangia ili waoane vizuri.
3. Mjaluo kafia Dar alikoenda kutoa mahari ya mke wa Saba. Sharti aziikwe Taarime. Tunachangishana kusafirisha. Serikali inakata tozo badala ya kuchangia ubani ili tulio msibani tule Kamongo.
5. Wakurya wamejifunza kutumia choo. Wameamua kujenga choo shuleni kwao. Wakatuma michango kupitia what's up. TOZO ya serikali sawa na shimo moja. Hivi Serikali haijawazuia Wakurya kutumia choo ili waendelee kujisaidia vichakani?
5. Shule ya kata inalipia umeme kwa Luku, makanisa, misikiti, mortuary, vyoo vya umma,nk vinalipia umeme kupitia LUKU. Majengo haya yamesamehewa kulipa kodi ya majengo. Je kulipia kodi hii kupitia LUKU hakufuti misamaha hiyo?
6. Viwango vya tozo na kodi ya pango ni vikubwa. Miundo mbinu ya kampuni za simu imegharimu fedha nyingi sana na tayari wanalipa kodi na kutoa ajira. Watumiaji wa umeme vijijini wengi ni Maskini Sana wanaoishi kwa huruma ya TASAF isiyo rasmi. Wanahitaji kunyweshwa maziwa badala ya kukamuliwa.
7. Tumeulizwa tuna mapendekezo gani ya kuzipa pengo la bajeti endapo tozo zitafutwa? Kama mko tayari kusikiliza tutapendekeza. Wengi tunatamani serikali inayosikiliza kuliko inayodai kusikilizwa. TOZO ni mbaya na ni kubwa. Kodi ya pango kupitia LUKU ni kero na inazua maswali mengi. RUDINI mezani, punguza kusema, ongeza kusikiliza. Sikiliza wanaokosoa kuliko wanaopongeza.
Kifo cha mbwa huanza kwa kupoteza uwezo wa kunusa.