Tozo ilipaswa ijenge madarasa lakini inaliwa huo ndiyo ukweli wenyewe. Tulisema mfumo mzima wa muundo wa serikali ya mitaa ufumuliwe na kusukwa upya wahusika wamedinda.
Rais kuteua wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri ndiyo chimbuko la wizi na ubadhirifu kwa sababu wateuliwa hawa hawawajibiki moja kwa moja kwa wananchi na hivyo kudhoofisha uwajibikaji.
Kulingana na rasimu ya marekebisho ya katiba ya Warioba wananchi walishauri mamlaka ya Rais yapunguzwe na kurudishiwa wananchi wenyewe lakini uroho wa madaraka na hulka ya kuwazawadia ajira makada wa CCM umesitisha mageuzi muhimu katika uendeshaji wa nchi. Wizi huu wa kutisha unafanywa na makada wa CCM waliopewa dhamana kwenye nyadhifa tajwa! Tungependa kukolezea kwa kutamka hadharani hakuna mteule hata mmoja wa Rais anachagulika na wapigakura kwenye eneo analolihudumia leo. Huu ni uwakilishi haramu. Pale penye uwakilishi haramu hakuna uwajibikaji na kujenga mazingira hatarishi ya watumishi kujichotea hela watakavyo!
Hata mkamue wananchi vipi kama ni Rais ataendelea kutubandikia maswahiba wake na jamaa zake wa karibu nyadhifa za wakuu wa mikoa, wilaya na DEDs basi hakutakuwa na maendeleo bali tutakuwa tunafukuzana na kashfa za wizi na ubadhirifu.
Tulisema Waziri Mkuu atimuliwe kwa kushindwa kuongoza mabadiliko ya muundo wa serikali za mitaa lakini hakuna mwenye masikio.
Hivi mna matatizo gani?
Hoja ya ukabila imesambaratishwa na ugatuzi Kenya.
Ukelele wa ugatuzi utaidhoofisha serikali kuu pia imegalagazwa na ugatuzi Kenya.
Tatizo la TZ ni kufanya kazi kwa mazoea. Mifumo ya uongozi aliyoiacha mkoloni miaka 60 iliyopita inakumbatiwa ili kulinda ajira za makada wa CCM ambao ndiyo viwavi jeshi.
Bila kuwawezesha wapigakura kuwaajiri wakuu wa mikoa, wilaya na madiwani kuwa waajiri wa watumishi wote kwenye halmashauri zao na kuendelea na huu mfumo wa Rais kuwateua watu ambao hata hawajui ila kwa kushauriwa na wasaidizi wenye masilahi yao tuendelee kutegemea uwajibikaji kwa wapigakura kukosekana na kuwa kichocheo cha wizi na ubadhirifu