Mramba, Yona wahaha kutoka rumande Keko
Shadrack Sagati
Daily News; Wednesday,November 26, 2008 @21:15
Masharti ya dhamana yaliyowekwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, yamezidi kuwaelemea mawaziri wawili wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona, na sasa wameonyesha nia ya kukata rufaa Mahakama Kuu.
Mawaziri hao wa zamani wanashitakiwa kwa kutumia vibaya madaraka waliyokuwa nayo ya uwaziri kwa kuipendelea Kampuni ya Alex Stewart na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7, kati ya mwaka 2003 na 2007.
Kampuni hiyo ilikuwa inajishughulisha na ukaguzi wa hesabu za kampuni zinazochimba dhahabu nchini. Mawakili wa upande wa utetezi jana waliwasilisha barua kwa Hakimu Mkazi Hezron Mwankenja ambaye ndiye aliyewapa sharti wanaloona gumu la kuweka fedha taslimu Sh bilioni 3.9 kila mmoja.
Barua hiyo inaiomba mahakama hiyo kuwapatia mawakili wa washitakiwa mwenendo wa shauri hilo ili wawasilishe rufani yao Mahakama Kuu kuomba kulegezwa kwa masharti hayo.
Masharti mengine yaliyotolewa na Hakimu Mwankenja ni washitakiwa kukabidhi hati zao za kusafiria kwa waendesha mashitaka na hawaruhusiwi kutoka nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama. Sehemu ya barua ya mawakili hao inaeleza kuwa,
"We request to be supplied with certified copies of the proceedings, ruling and order in respect of the above matter dated 25th November 2008 for our necessary action." Katika tafasiri isiyo rasmi mawakili hao wanasema kuwa wanaomba kupatiwa nakala ya mwenendo, uamuzi na amri za shauri hilo lilitolewa uamuzi Novemba 25, 2008 kwa ajili ya hatua zaidi.
Hakimu Mwankenja tayari ameagiza mahakama iwapatie haraka mwenendo wa shauri hilo ili wakamilishe taratibu zao za kutaka kukata rufaa. Washitakiwa wanatetewa na kundi la mawakili ambao ni Joseph Tadayo, Michael Nyaro, Mafuru Mafuru, Sam Mapande na Elisa Msuya.
Jopo hilo juzi liliomba mahakama iweke masharti nafuu ya dhamana. Juzi Tadayo aliomba mahakama wakati inatoa masharti ya dhamana kuhusu kipengele cha fedha taslimu, iangalie pia uwezekano wa kuweka sharti mbadala ambalo ni kuwa na hati yenye thamani ya nusu ya fedha zinazodiwa kusamehewa Kampuni ya Alex Stewart.
Sharti jingine ambalo Tadayo aliomba ni mahakama iangalie kanuni ya washitakiwa kuchangia kiasi hicho cha fedha kama sheria ya dhamana inavyoelekeza. Upande wa mashitaka unaoongozwa na wakili wa Serikali Boniface Stanislaus, haukuwa na pingamizi lolote kuhusu maombi hayo ya washitakiwa na wakaiomba mahakama itumie busara yake katika kuamua masharti.
Kutokana na mahakama kuweka masharti hayo, washitakiwa hao walishindwa kutimiza masharti hilo na kulazimika kupelekwa kortini. Mramba katika kesi hiyo anaguswa na mashitaka yote 13 wakati Yona anaguswa na mashtaka sita. Mashitaka yanayomgusa Yona ni yale ya kushiriki kuipendelea kampuni ya Alex Stewart kwa kuipa nyongeza ya mkataba.
Lakini pia waziri huyo wa zamani wa Nishati na Madini anatuhumiwa kuipendelea kampuni hiyo, kuiachia suala la ukaguzi wa hesabu za kampuni zinazochimba madini nchini kufanywa kiholela na kampuni hiyo bila kuishirikisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kutokana na kutokuwa makini, Yona anahusishwa kuchangia kuisababishia hasara ya Sh bilioni 11.7 Serikali ya Tanzania.
Mramba, licha ya kuguswa na mashitaka hayo, lakini pia anatuhumiwa kutoa misamaha mbalimbali ya kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart na kusababisha hasara hiyo ya Sh bilioni 11.7. Kesi hiyo itatajwa tena Desemba 2, mwaka huu kutokana na upande wa mashitaka kuendelea na upelelezi wa shauri hilo.
Serikali iliingia mkataba wa miaka miwili na kampuni hiyo Juni, 2003 kwa lengo la kuhakiki uzalishaji na gharama za usafirishaji wa dhahabu pamoja na uwekezaji na uendeshaji wa migodi mikubwa na mkataba huo ulimalizika Juni mwaka jana. Baada ya mkataba huo kumalizika, kampuni hiyo iliongezewa mkataba mwingine kinyemela.
Bunge liliwahi kuelezwa na serikali kuwa katika kipindi cha miaka miwili kampuni hiyo ilikuwa inalipwa zaidi ya dola za Marekani milioni 31 (zaidi ya Sh bilioni 38) kwa wakati huo. Baada ya kumalizika mkataba huo, serikali haikuitisha zabuni nyingine, bali kwa kifungu namba 2.4 cha mkataba iliongezewa tena mkataba huo kwa kile walichodai baada ya kuridhika na utendaji wake wa kazi.
Katika hatua nyingine, imefahamika kuwa baadhi ya wafanyabiashara nchini wamekuwa na vikao tangu juzi wakihaha kusaka fedha kwa ajili ya kuwadhamini mawaziri hao wa zamani. Imefahamika kuwa vikao hivyo vimekuwa vikiratibiwa na baadhi ya wafanyabiashara ambao ni watendaji katika kampuni mbalimbali kubwa nchini.
Aidha, imefahamika kuwa keshokutwa Jumamosi, binti wa Mramba anatarajia kufunga pingu za maisha Dar es Salaam, baada ya kuwa amekwisha kufanyiwa tafrija ya kuagwa hivi karibuni. Wakati huo huo, Iman Mwakyosa mshitakiwa pekee katika kesi ya kuchota mabilioni ya fedha katika Benki Kuu ambaye amebaki bila kudhaminiwa, amekata rufaa Mahakama Kuu kupinga masharti kadhaa ya dhamana.
Sharti analopinga Mwakyosa ni la kuweka fedha taslimu ambalo limewekwa na Hakimu Mwankenja. Wenzake watatu tayari wameshapata dhamana. Wenzake katika kesi hiyo, Esther Mary Komu, Bosco Kimela na Rajab Maranda wamedhaminiwa baada ya kutoa fedha taslimu zaidi ya Sh milioni 103.