Kumekuepo na hadaa za wanasiasa matapeli kuhubiri mabadiliko ya sheria za uchaguzi nnje kabisa ya wakati wa mabadiliko ya sheria na katiba, kana kwamba hayo ndiyo mahitaji muhimu zaidi kwa wananchi wa Tanzania kuliko maji, afya, elimu, kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara, miundombinu, usafirishaji n.k
Lakini pia,
matapeli hao wa kisiasa nchini wanaendelea kuhadaa wananchi zaidi kwamba hitaji la waTanzania ni vyeo na mamlaka. Kwamba wananchi wanahitaji sana matapeli hao wa kisiasa wapate vyeo, kuliko mahitaji yao muhimu ya kila siku.
Na ndio maana,
agenda kubwa za wanasiasa hao waliofilisika hoja zimekua ni kujadili umri wa makamu mwenyekiti wa CCM bara, na na ubaguzi dhidi ya ukanda anakotoka rais Dr. Samia Suluhu Hassan na jinsia yake, kana kwamba ukiwa kiongozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka upande wa Zanzibari Bara, ni kosa na ni anasa kubwa mno, huku wakijua wazi kabisa kua hakuna mtu anaweza kupata uongozi wa kitaifa Tanzania bila waZanzibari.
Ni vizuri kama wanasiasa kuibua hoja zenye mashiko kwa wakati sahihi na muafaka, kuliko kubwekabweka na kuwahadaa wananchi kwa vimisemo vitakavyowaathiri wenyewe na kuwakosesha fursa na haki zao za msingi, ikiwa ni pamoja na haki ya kupiga kura kuchagua viongozi ambao wanawataka kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi.
Kumbuka,
hata mtua aimbe, alie, acheke, acheze au abwekebweke namna gani, uchaguzi mkuu wa kihistoria Tanzania upo pale pale, ni Oct.2025
Mungu Ibariki Tanzania
ASKOFU DKT. BAGONZA: KWA MUJIBU WA KIAPO CHA URAIS NA FALSAFA YA 4R YA RAIS SAMIA SASA RAIS SAMIA ANAO WAJIBU WA KIKATIBA KUIKARABATI MIFUMO INAYOTUMIKA KUFANIKISHA UHALIFU WA KISIASA KATIKA CHAGUZI AMBAPO UHALIFU HUO UNAOTEKELEZWA NA WANASIASA MATAPELI WANAOFUATA NYAYO ZA HAYATI RAIS JOHN POMBE MAGUFULI
Je, kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, na hasa kwa mujibu wa kiapo cha urais wake, Rais Samia Suluhu Hassan anao wajibu wa kikatiba kujitenga na mifumo inayotumika kufanikisha uhalifu wa kisiasa katika chaguzi, uhalifu huo ukiwa unatekelezwa na wanasiasa matapeli wanaofuata nyayo za hayati Rais John Pombe Magufuli?
Ndiyo. Ni kweli kwamba Rais Samia anatoka chama kile kile kilichokuwa kinaongozwa na hayati Rais John Pombe Magufuli.
Ndiyo. Hakuna utata kwamba Rais Samia alikuwa Makamu wa Rais wa hayati Rais John Pombe Magufuli.
Ndiyo. Ni wazi kwamba Rais Samia ni miongoni mwa wanufaika wakuu wa uhalifu wa kisiasa uliofanyika katika chaguzi ukiwa unatekelezwa na wanasiasa matapeli waliokuwa wanafuata maagizo ya hayati Rais John Pombe Magufuli.
Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan HALAZIMIKI kurithi misimamo haramu ya JPM kuhusu chaguzi zetu na HALAZIMIKI kuendeleza mahusiano yaliyogubikwa na uhasama kati yake na vyama vya upinzani.
Misimamo hiyo ya JPM ilivunja katiba ya nchi aliyokuwa ameapa kuilinda, ilivunja haki za binadamu na iliifunga nchi kiasi cha kututenganisha na dunia ya wanademokrasia.
Ndiyo maana, mara tu baada ya kiapo chake kama Rais mpya wa Tanzania, Rais Samia alifanya maboresho kwa kiasi fulani.
Mfano, aliamua kuondoa mazuio ya mikutano yaliyokuwa yanavunja katiba, alitamka hadharani kufungua nchi na alizindua falsafa ya 4R.
Lengo lake lilikuwa na huenda bado ni kuliepusha taifa na sifa mbaya ya kuvunja haki za binadamu na kukiuka kanuni za kikatiba kuhusu utawala bora.
Kuhusu chaguzi zetu, yeye binafsi na pia wasaidizi wake walitamka hadharani kuwa yaliyotokea 2019 na 2020 hayapaswi kujitokeza tena.
Niliwahi kueleza kuwa mimi “ninaogopa” kuamini ahadi hizo kwa kuwa hazina misingi ya kisheria na kikatiba.
Lakini kwa kuwa zilitolewa na viongozi walioapa kwa kutumia misahafu kuilinda katiba ya nchi niliamua kuishi kwa imani.
Imani yangu hii ndio inanifanya kuuliza na kujaribu kujibu baadhi ya maswali kuhusu mfumo wetu wa uchaguzi. Maswali na majibu yangu yanafuata.
Swali 01: Kwa Nini Tunapaswa Kukubaliana Kwamba Uchaguzi Ufanyike Baada ya Marekebisho ya Maeneo Muhimu ya Katiba ambayo yatakuwa ni “Minimum Reforms”?
Kufuatia kuapishwa kuwa Rais baada ya uchaguzi wa 2015, JPM alitoa amri ya mdomo ya kukataza shughuli za kisiasa za vyama vya upinzani.
Amri hiyo ilikiuka Katiba ya JMT hususan Ibara za 12 hadi 21.
Kwa bahati mbaya watu na taasisi waliotegemewa kupinga au hata kukemea ukiukwaji huo wa Katiba ya JMT, walikaa kimya kana kwamba jambo hilo haliwahusu.
Wafuatao walipaswa angalau KUNUNA kwa sababu ya ukiukwaji huo:
- CCM na UONGOZI WA JUMUIYA ZAKE. Kwa kuwa CCM haina baraza la Wazee, wale wazee wachache waliofunua midomo yao na kunong'ona, JPM aliwatisha kuwa wakome "kuwashwa washwa"
- Bunge la JMT lenye mamlaka ya kuishauri na kuisimamia Serikali nalo liliufyata na kuanza kuimba masifu na mapambio kwa JPM
- Mwanasheria mkuu wa Serikali
- .Msajili wa Vyama vya siasa.
- Viongozi wa Asasi za Kiraia zinazohusika na utetezi wa HAKI ZA BINADAMU
- Viongozi wa Makanisa yanayowafundisha kwamba "MUNGU WETU NI MUNGU WA HAKI" na kwamba "MAMLAKA YOTE HUTOKA KWA MUNGU" huyo.
- Viongozi wa Misikiti wanaomwakilisha Mungu anayetaka HAKI SAWA KWA WOTE.
- Jumuiya ya Kimataifa inayohimiza serikali za dunia kuheshimu tunu na kanuni za demokrasia na utawala bora.
- Raia mmoja mmoja mwenye jukumu la kulinda ukamilifu wa Katiba ya nchi kwa kupinga utawala holela wenye sura ya uongozi wa kiimla.
Pamoja na hayo Mtu pekee aliyejitokeza kupinga ukiukwaji huo wa haki za Kilatiba kwa njia ya UJASIRI na UWAZI ni mmoja tu.
Yaani TUNDU ANTIPAS LISSU ambaye alikuwa Rais wa TLS wakati huo.
Matokeo yake alishambuliwa kwa risasi nyingi.
Ni Rais Samia pekee aliyejitoa mhanga akiwa Makamu wa Rais aliyefika Nairobi kumjulia hali Tundu Lisu.
Ilipofika 2019, Rais JPM alitoa tamko jingine la kuvunja KATIBA pale alipowaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini (DED) kutowatangaza wapinzani kama Washindi kwenye chaguzi zote za Serikali ukiwemo Uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Kwa uwazi kabisa amri hiyo ya JPM ilikiuka matakwa ya Katiba ya Tanzania inayosema kuwa Tanzania ni dola ambayo ni Jamhuri ya Kikatiba na Kidemokrasia.
Kwa mujibu wa Katiba hii mamlaka yote ya kiutawala yanapaswa kutoka kwa umma wa wapiga kura, kwa njia ya uvhaguzi ulio huru, wazi na shindanishi, kama ilivyoandikwa kwenye ibara ya 8 ya Katiba(1977).
Na, kama ilivyokuwa kwa amri ya awali ya katazo la shughuli za kisiasa za vyama vya upinzani, WADAU WOTE WALIOPASWA KUIPINGA UKIUKWAJI WA KATIBA YANNCHI walinyamaza kimya.
Baada ya kifo cha JPM, Rais Samia Suluhu Hassan, hatimaye alitengua katazo la shughuli za mikutano ya kisiasa nchini
Lakini Rais Samia, BILA SHAKA KWA MAKUSUDI hakusema kitu juu ya Amri ya pili ya mtangulizi wake, ya kuzuia washindi wa upinzani kutangazwa kama washindi halali pale wanaposhinda.
Matokeo yake uliotegemewa kuwa uchaguzi wa Serikali za mitaa wa 2024 umechukua sura ile ile ya uchaguzi wa 2019. Yaani:
- Kutoandikisha wapiga kura kwenye ngome za wapinzani,
- Kuwaengua wagombea wao wengi,
- Kutowaruhusu mawakala wa vyama vya upinzani na
- Kutowatangaza wapinzani hata pale walipoonekana kushinda.
Hili ni donda ndugu linalochafua uhalali (“legitimacy”) wa viongozi wetu wa vitongoji waliopatikana kutokana na mchakato huo haramu, maana malengo halali ya kuunda serikali hayapaswi kuhalalisha mbinu haramu za uchaguzi.
Kama ilivyokuwa mwaka 2019 na mwaka 2020, mchakato wote wa Uchaguzi wa 2024 umekiuka Katiba ya JMT, sheria zote husika na misingi ya kuendesha Uchaguzi kwa jamii inayojitambulisha kama Taifa ambalo ni Jamhuri ya Kidemokrasia na inayopaswa kujiheshimu kulingana na utambulisho huo wa Kikatiba.
PIA, MILA ZETU ZA KIAFRIKA ZINASISITIZA KWAMBA KUNA KIWANGO CHA CHINI KABISA CHA MTU AU JAMII KATIKA SUALA LA KUJIHESHIMU, ISIPOKUWA KAMA MTU NI PUNGUANI.
Swali 02: Kama tukishindwa kukubaliana kuhusu umuhimu na ulazima wa mageuzi ya kimfumo kabla ya uchaguzi wa 2025 na hivyo tukalazimishwa kwenda kwenye uchaguzi wa 2025 kabla ya marekebisho ya kimfumo kufanyika kutatokea nini?
Kwa maoni yangu, kama tukisoma alama za nyakati kwa umakini tutakubaliana kuwa endapo tutaenda kwenye uchaguzi wa 2025 kabla ya marekebisho ya kimfumo basi uhalifu uliofanyika kwenye chaguzi za 2019, 2020 na 2024 utafanyika tena.
Hatimaye Raia wa Tanzania wataendelea kuishi kama watumwa ndani ya nchi yao kwa sababu ya kutawaliwa na serikali haramu kama ilivyokuwa enzi za ukoloni wa Wazungu na zama za utumwa wa Waarabu.
Nitaeleza kwa nini natabiri hivyo na kwa tunapswa kuepuka haya ninayoyatabiri.
Kwanza, Rais Samia bado hajatengua amri ya JPM ya KUWAKATAZA ma DED kuwatangaza WAPINZANI kama washindi wa Ubunge na Udiwani.
Pili, Tume ya Uchaguzi iliyobatizwa jina la HURU bado ni ileile kuanzia uteuzi wa Mwenyekiti na Makamu wake na wajumbe wengine.
Ni hivyo hivyo kwa Mkurugenzi na Sekretarieti ya Tume.
Tatu, watendaji wengi walioratibu na kutekeleza hujuma za uchaguzi wa 2019, 2020 na 2024 bado wako ofisini wakuwa na uzoefu wao wa kihalifu.
Na jambo baya zaidi ni kwamba, uchaguzi wa 2019, 2020 na 2024 UMESABABISHA MAJERAHA MAKUBWA KWA DHAMIRI ZA WATANZANIA WOTE walioshiriki kuuandaa, kuusimamia na kutangaza Matokeo yake.
Waasisi wa Taifa letu na hususan Mwalimu J.K Nyerere walifanya kazi kubwa ya kutufanya wamoja.
TUNAISHI, TUNAFANYA SHUGHULI ZOOTE ZA KISIASA, KIJAMII, KIDINI bila kujali makabila yetu, dini zetu, rangi zetu, hali ya maisha nk.
Kwa sababu hiyo hakuna siri miongoni mwa Watanzania kuhusu uhalifu wa kiuchaguzi unaofanywa na serikali ya CCM mwaka hadi mwaka.
Hujuma zote zilizofanyika kwenye chaguzi zetu zinajulikana na zimesamba kabisa miongoni mwa Watanzania.
Nne, uhalifu wa kisiasa unaofanyika kupitia uchaguzi utaendelea kujenga ujasiri wa kihalifu katika mioyo ya watu kwenye sekta baki za maisha ya kila siku.
Hakuna ubishi kwamba kutokana na chaguzi hizo haramu CCM na Serikali yake wamefanikiwa kujenga jamii ya mamilioni ya watu wengi wenye dhamiri zilizokufa kimaadili.
Wengi wao wanaamini kuwa malengo halali ya kisiasa yanaweza kufukuziwa kwa kutumia mbinu zozote bila kujali kama ni halali, nusu halali au haramu. Hii ni itikadi hatari ya Umachiaveli.
Watu hawa sasa wamegeuka matapeli wa siasa kutokana na tabia yao isiyokoma ya kufanya UDANGANYIFU wa wazi kwenye hatua zote za mchakato wa uchaguzi utafikuri ni wapagani.
Hawa ni pamoja na baadhi ya:
- Wakuu wa mikoa--Ma RC,
- Makatibu Tawala wa Mikoa--Ma-RAS,
- Wakuu wa Wilaya--Ma-DC,
- Makatibu Tawala wa Wilaya--ma-DAS,
- Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya--Ma-DED,
- Maafisa Watendaji wa Kata --Ma-WEO
- Maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama,
- Mahakimu na majaji wanaoshughulikia kesi za uchaguzi
- Wasimamizi wa uchaguzi vituoni ambao kwa sasa ni watumishi wa Umma kama vile Walimu.
- Na baadhi ya mawakala wa vyama vya siasa wenye hulka ya kuganga njaa.
Tukiondoa wahusika ambao ni makada wa CCM, watu waliobaki wanatii amri ili kutunza ajira zao.
Si ajabu hata mimi Askofu Bagonza ningefanya utii kama wao labda kwa sababu ya nidhamu ya woga.
Lakini sasa matokeo yake sasa tumegeuka Taifa la WEZI, Taifa la WAONGO, Taifa la WALAGHAI, Taifa la MATAPELI, Taifa la WANAOGHUSH matokeo nk.
Watu ni waongo, mifumo ya Tehama inachezewa, na taifa linabomolewa na watu wanaoitwa wataalam wa TEHAMA (ICT).
Tukiendekeza wizi na ulaghai kwenye chaguzi zetu, tutazidi kubomoa JINA na HESHIMA YA NCHI YETU ILIYOJENGWA KWA JUHUDI, MAARIFA NA KUJITOA SANA KWA WAASISI WETU. SASA TUNAKARIBIA KUIPIKU NCHI YA NIGERIA.
Mambo haya yanaathiri utambulisho wa taifa letu. Baadhi yetu tumefaidi matunda ya jina zuri la taifa letu lililojengwa kwa gharama kubwa na waasisi wa taifa letu.
Niliwasikia kwa masikio yangu baadhi ya viongozi wa sasa wa serikali yetu wakijiapiza kuwa “yaliyojitokeza katika awamu ya tano, yasiruhusiwe tena”.
Rais Samia ana historia ya kujenga na tayari anayo. Ana Legacy ya kuacha, si kubebana na ya awamu ya tano.
Lakini pia CCM bado inao uwezo mkubwa wa kushinda chaguzi bila ulazima wa “kuonekana” inaiba kura.
Naogopa kuamini kuwa sifa ya mwana CCM ni kuiba kura! Inatisha.
Si dalili njema kuona vijana wengi wameanza kushabikia uongozi wa kibabe (Trump na Traore) huku wakibeza demokrasia.
Na wengine wengi wanamkumbuka JPM na kutamani arudi.
JPM alikuwa na mazuri yake lakini si katika eneo hili la demokrasia na utawala bora.
Swali 03: Kusudi tuweze kuepuka madhara haya tufanye nini ili tuweze kulirejesha Taifa la Tanzania kwenye misingi ya dola ambayo ni Jamhuri ya Kikatiba na Kidemokrasia katika mtazamo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kama ilivyoandikwa kwenye Katiba yetu?
Binafsi nawasihi Watanzania wote tuamke. Sote tuingie ulingoni, tupaze sauti. Mageuzi ya kimfumo niliyoyaongelea hapo juu ni ajenda yetu sote.
Tusiruhusu madai ya mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi kumilikiwa na chama chochote cha siasa, azaki yoyote, au kikundi kingine chochote cha kisekta.
Hii ni kazi ya watu wote wenye mapenzi mema na taifa letu.
Hivyo namwalika kila mmoja na kila kikundi katika nafasi yake kuandaa "TAMKO LA KUUNGA MKONO MAGEUZI YA KIMFUMO KABLA YA UCHAGUZI MKUU WA 2025" na kulitangaza tamko hilo kwa umma ili kujenga hamasa na kulipa uzito suala hili.
Mie tayari nimetimiza wajibu wangu wa kutoa "tamko" kupitia andiko hiki.
Nawe tafakari na chukua hatua leo. Liwezekanalo leo lisingoje kesho.