The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Kujua haki na wajibu wako ni muhimu kila wakati, haswa ukiwa mtandaoni. Mtandao unapanua haki yetu ya uhuru wa kujieleza, lakini pamoja na uhuru huo, kuna wajibu wa kuwatendea wengine kwa kuzingatia utu na heshima.
Kuwatendea wengine kwa heshima ni muhimu mtandaoni kama tu ilivyo ana kwa ana. Kuwa “raia bora wa mtandaoni” (good netizen) ni kujua kile kinachofaa kufanya na kusema katika mazingira ya mtandaoni.
Ujio wa mazingira ya kidigitali – kimsingi mitandao ya kijamii – umechochea demokrasia na uanaharakati kwani umewapa watu uhuru wa kushiriki habari na mijadala mbalimbali. Lakini kwa upande mwingine, imekuwa njia ya watu wenye nia mbaya kuwadhulumu, kukejeli na kuumiza kihisia watumiaji wasio na hatia.
Leo, wapo watu wenye ujasiri wa kufedhehesha, kuaibisha na kutisha wengine mtandaoni bila kuwa na wasiwasi kuhusu jinsi mwathiriwa atakavyohisi. Kuongezeka kwa ukatili wa unyanyasaji mtandaoni kunaleta athari kubwa zaidi kwa wanaohusika.
Ukatili/Uonevu wa mtandaoni ni mbaya sana kwani hupenya katika kila nyanja ya maisha ya mwathirika na kusababisha matatizo ya kisaikolojia na kijamii. Katika baadhi ya matukio, wapo waliojiua kwa kathiriwa na unyanyasaji wa mtandaoni.
Unyanyasaji huu unaweza kuathiri kujithamini kwa waathiriwa; yaani wanaweza kuona aibu kujitokeza hadharani au kuchangamana na wengine kijamii. Hata hivyo, hakuna yeyote anayefaidika na unyanyasaji wa mtandao – hata wanaotenda unyanyasaji huo mwishowe hawanufaiki kwa namna yoyote.
Unyanyasaji huu ni rahisi kufanyika kuliko ule unaotekelezwa kwa namna nyingine kwani si lazima mhalifu kumkabili muathiriwa ana kwa ana. Lakini pia, unaweza kufanywa bila mhusika kujulikana na hivyo muathiriwa kutomjua ni nani anayemtendea.
Athari nyingi za kisaikolojia zinaweza kuwa mbaya kwa waathiriwa bila kujali umri. Hata hivyo, kwa sababu watoto na vijana bado wanajifunza kudhibiti hisia zao na namna ya kuchangamana kijamii, wako katika hatari zaidi na huathirika sana. Wanaweza kuathirika kwa kupata woga wa kutengwa na jamii, kufanya vibaya katika masomo, kukosa kujiamini, au kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya ili kutuliza maumivu yao ya kisaikolojia n.k.
Kwa mujibu wa ripoti wa taasisi ya Ipsos ya mwaka 2018, katika nchi za Afrika na Mashariki ya Kati, mitandao ya jamii ndiyo jukwaa linaloongoza kwa unyanyasaji wa mtandaoni kwa 61%, huku simu ikifuata katika 42%; ujumbe wa mtandaoni 36%; vyumba vya gumzo mtandaoni (chatrooms) 33%; barua pepe 18%; tovuti nyingine 13%; na teknolojia nyingine kwa 6%.
Kama maeneo mengine duniani, Tanzania pia ni moja ya nchi ambazo zina miongozo ya kisheria kusimamia maudhui na masuala mbalimbali ya mtandaoni. Kwa Tanzania Sheria ya Maudhui ya Mitandaoni (Online Content Regulation) 2020 inakataza na kutoa adhabu kwa urushaji wa maudhui yenye kudhalilisha ikiwamo picha/video za utupu, pamoja na lugha za udhalilishaji zinazokwenda kinyume na utamaduni wa Mtanzania.
Lakini pia, Sheria ya Kimakosa ya Mtandao 2015 (Cyber Crime Act) kupitia Kifungu chake cha 23 kinakataza na kupinga uonevu mtandaoni. Hii inamaanisha kuwa ni kosa kisheria kwa mtu yoyote kufanya uonevu wa aina yoyote kwa kutumia njia za kieleketroniki na yeyote atakayekutwa na kosa hilo atatumikia kifungo kisichozidi miaka 3 jela au zaidi, au kulipa faini isyopungua milioni tano (5) au vyote kwa pamoja.
Hata hivyo, taasisi ya WiLDAF Tanzania inasema pamoja na kuwepo Sheria hizo inaelezwa kuwa ukatili wa mitandaoni unazidi kukithiri kutokana na uelewa mdogo kwa wananchi juu ya sheria husika, hofu ya kuendelea kudhalilika hasa pale kesi zinapotaka kwenda Mahakamani na utamaduni wa jamii kwenye mitandao kukaa kimya badala ya kukemea wanapoona vitendo vya uaktili kwenye mitandao.
Ili kufanya mtandao kuwa sehemu salama kwa kila mmoja, kampuni ya Microsoft inahimiza watu kufikiria kuhusu tabia zao za mtandaoni, na jinsi inavyoathiri wengine. Haya ni baadhi ya mambo yanayoshauriwa kuzingatia kwa kila raia wa mtandaoni (netizen):
1. Ni vema kutenda kwa huruma na ubinadamu katika kila mwingiliano na kumtendea kila mtu unayeungana naye mtandaoni kwa hadhi na heshima, kama vile ambavyo ungetamani kutendewa na wengine.
2. Ni jambo muhimu sana pia kutambua tofauti za kitamaduni na kuheshimu mitazamo tofauti. Lakini pia, hata kama hukubaliani, ni muhimu kushiriki mtandaoni kwa uangalifu na kuepuka kuwaita wengine majina yasiyowapendeza na kuwashambulia kwa mambo yao binafsi.
3. Suala lingine muhimu ni kufikiria kabla ya kujibu mambo ambayo hukubaliani nayo, kutochapisha au kutotuma chochote ambacho kinaweza kuumiza mtu mwingine, kuharibu sifa ya mtu mwingine, au kutishia usalama wa wengine.
4. Lakini pia inashauriwa kusimama kwa ajili yako mwenyewe na wengine; kumwambia mtu endapo utahisi haupo salama, lakini pia kutoa msaada kwa wale wanaolengwa na matumizi mabaya ya mtandaoni. Mwisho, ingawa si kwa umuhimu, ni vema kuripoti shughuli zinazotishia usalama wa mtu yeyote, na kuhifadhi ushahidi wa tabia isiyofaa au isiyo salama.
Leo hii mtandaoni pamekuwa nyumbani, kazini, shuleni, uwanja wa mikutano na hata eneo la ibada kwa baadhi ya watu. Kwa kuzingatia haya, ni muhimu kuzingatia na kuheshimu ukweli kuwa kila mmoja anayeshiriki katika maeneo haya anapaswa kuheshimiwa kwa kiwango anachostahili. Kuwabugudhi wengine au kuwanyanyasa kwa namna yeyote ile ni ukiukaji wa haki zao kama vile tu ambavyo matendo hayo yangefanywa ana kwa ana.