Nyerere alikuwa mwanamikakati hodari sana.
Yoda,
Unaijua historia ya Hamza Mwapachu (1913 - 1962) na aliyofanya kuwapata vijana wasomi kupigania uhuru wa Tanganyika?
Soma hapo chini:
MWALIMU WA MWALIMU:
HAMZA KIBWANA MWAPACHU (1913 - 1962)
Balozi Mwapachu afichua barua ya Shujaa Hamza
Na Bakari Mwakangwale
BALOZI Juma Hamza Mwapachu, ameiweka hadharani barua ya baba yake Mzee Hamza Kibwana Mwapachu, aliyomwandikia Mwalimu Julius K. Nyerere, mwaka 1949.
Barua hiyo imewekwa hadharani Watanzania wakielekea kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika na baadae Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius K. Nyerere, aliyefariki dunia Oktoba 14, 1999.
Akizungumzia barua hiyo, mtafiti na mwandishi wa vitabu vya historia sahihi ya Tanganyika, Mohammed Said Salum, amesema barua hiyo karibu sasa itafikia miaka 70, tokea kuandikwa kwake.
Akitoa maoni yake Mohamed Said, alisema anadhani sababu ya kuiweka barua hiyo hadharani wakati huu, pengine ni kutaka kuwazindua Watanzania kuhusu kupotoshwa kwa historia ya wananchi wa Tanganyika katika kujikomboa kutoka katika makucha ya ukoloni wa Waingereza.
“Kumekuwa na tatizo kubwa katika kutafiti na kuandika kwa usahihi historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika, sasa naona Balozi Juma Mwapachu ameiweka hadharani barua ya baba yake Hamza Kibwana Mwapachu (1913 1962) aliyomwandikia Julius Nyerere, mwaka wa 1949, ili pengine kulizindua Taifa.
Amesema Mzee Said.
Akifafanua Mohamed Said amesema, mengi yaliyoandikwa kuhusu historia ya Tanganyika, yamemtaja Julius Nyerere, peke yake kiasi cha kufanya iaminike kuwa kabla yake hapakuwa na wanasiasa wala hapakuwapo na watu waliofanya juhudi zozote za kutaka kuikomboa Tanganyika kutoka kwa wakoloni, isipokuwa Mwalimu Julius Nyerere peke yake hali iliyopelekea nchi kukosa kuwatambua mashujaa wake.
Alisema, barua hiyo imedhihirisha ukweli kuwa historia ya uhuru wa Tanganyika, ipo katika vichwa vya watu na wengi wao wameshatangulia mbele ya haki na hata nyaraka nyingi zinazoonyesha mawasiliano ya kudai uhuru wakati huo pia zipo mikononi mwa watu binafsi.
Aidha Mohamed Said alisema, barua hiyo pia imefungua mlango na kuwawezesha watafiti wa historia ya Tanganyika kuchungulia ndani kusoma na kufahamu nini Mzee Hamza Mwapachu, alikuwa anasema kumwambia Mwalimu Nyerere, katika mipango ya kudai uhuru wa Tanganyika.
“Barua hii ni muhimu na kwa haraka iwekwe katika Makumbusho ya Taifa kwa faida ya vizazi vijavyo na naamini katika Maktaba ya Mh. Balozi Juma Mwapachu, yapo mengi mbali na aliyohifadhi kichwani kwake."
Amesema Mzee Said.
Akasema, Mtafiti yeyote katika historia ya uhuru wa Tanganyika, kama atakuwa makini hatoweza kumuepuka Mzee Hamza Mwapachu, kwani ni vigumu kumtaja Mwalimu Julius Nyerere na usimtaje Mzee Hamza Mwapachu.
Akiizungumzia barua hiyo alisema, hiyo (barua) ni matokeo ya barua ambayo Mwalimu Nyerere, alimwandikia Mzee Mwapachu, kuhusu mambo muhimu waliyozungumza siku za nyuma.
Alisema, katika barua hiyo, Mzee Mwapachu, ameorodhesha moja baada ya jingine katika yale waliyozungumza ambayo ni ''Trusteeship as compared to Protectorate and Mandate, White Paper 191, White Settlement in Tanganyika.''
Anafafanua zaidi Mohamed Said kuwa, katika ukurasa wa kwanza katika barua hiyo yenye kurasa tatu, unaonyesha mambo manane lakini kwa uchache ameyataja hayo matatu ambayo (kwa Kiswahili) ni udhamini wa Tanganyika chini ya Waingereza, Mjadala wa Afrika Mashariki na Ukazi wa Wazungu Tanganyika.
“Haya yalikuwa mambo mazito, makubwa na ya kuzungumzwa kwa siri sana baina ya Waafrika, sasa inawezekana vipi historia kama hii ikaachwa ipotee hivi hivi tu?''
Amesema na kuhoji mwanahistoria Mohamed Said.
Alisema, jambo la kusikitisha ni pale inapojaribiwa, ingawa kwa kuchelewa kuwaenzi mashujaa walio pambana na ukoloni, hujitokeza maswali mengi, ambayo hakuna awezaye kuyajibu kwa uhakika na kwa ithibati ya kuaminika.
Mathalani, akahoji kuwa inawezekana vipi kutolewa Medali ya Mwenge wa Uhuru kwa Abdulwahid na Ally Sykes, (ndugu wawili) waliokuwa kati ya waasisi 17 wa TANU, ukawaacha waasisi wengine kama Saadan Abdul Kandoro na Japhet Kirilo (kwa kuwataja wachache).
Mohamed Said akasema, itoshe tu kueleza kuwa medali hizo zimetolewa kwa kuchelewa miaka 50, kwani Ally Sykes, kapokea medali yake akiwa katika mwisho wa maisha yake akiwa mgonjwa, miaka miwili kabla ya kifo chake mwaka 2013.
“Lakini swali linakuja, vipi utawapa medali mashujaa hawa wa uhuru usimpe medali Mzee Hamza Mwapachu, ambae ushahidi wa historia unaonyesha kuwa ndiyo alikuwa, "mentor," wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Abdul Sykes?”
“Hawa wote waliokuja kudai uhuru katika nafasi zao tofauti na baada ya uhuru kupatikana wakaja kuwa viongozi wa Tanganyika huru."
Amesema Mzee Said.
Akichimbua zaidi kumbukumbu ya historia alisema kuwa Dr. Vedasto Kyaruzi, alipata kumwambia Juma Mwapachu, kuwa kama si mpango waliouweka Hamza Mwapachu na Abdul Sykes, basi Tanganyika isingepata uhuru wake mwaka wa 1961.
“Dr. Kyaruzi, akaongeza kwa kumwambia Juma Mwapachu, kuwa kule Nansio Kisiwani, alikopelekwa baba yake na Waingereza, ile ilikuwa ni jela ya kumtia kizuizini ili kumzuia asishiriki katika siasa.”
Akasema, wazalendo hao ndio waliochora ramani ya njia ipi ichukuliwe kuidai Tanganyika na kuitoa katika mikono ya Waingereza kwa salama.
Mohamed Said, akasema kwa wale waliokuwapo katika 'circle’ ya kupambana na Waingereza hakuna ambae hakuwa anajua kuwa Hamza Mwapachu, ndiye aliyekuwa akisukuma mambo nyuma ya pazia.
Alisema, kazi hiyo aliifanya iwe yuko Nansio au Rungwe, sehemu ambazo ni za mbali alizotupwa na wakoloni ili asiwasumbue kwa kumtoa karibu na miji mikuu ambako ndiko yalipokuwa mashina ya kupinga ukoloni.
Kulia: Abdulwahid Kleist Sykes (1924 - 1968) na Hamza Kibwana Mwapachu (1913 - 1962)