Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) Zachary Kakobe, amesema madai ya udini kwenye Uchaguzi Mkuu ujao ni dhana ya kufikirika isiyo na mantiki na inapaswa kupuuzwa na Watanzania wote.
Askofu Kakobe alisema kuzua jambo hilo wakati halipo, ni kosa kubwa linaloweza kutoa mwanya wa kuliumba na kuliingiza vichwani mwa watu bila sababu za msingi.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Askofu Kakobe alieleza kusikitishwa kwake na tetesi za madai kuhusu kuwepo mkakati wa wananchi kupiga kura kwa misingi ya udini Oktoba 31 mwaka huu na kufafanua kuwa jambo hilo ni uzushi na 'linapikwa' kwa makusudi.
"Hili wimbi la maneno ya udini ni dhana ya kufikirika tu, haipo. Inasikitisha tunapoona jambo hili linavaliwa njuga na kusemwa sana wakati huu. Udini usiokuwepo unapotajwatajwa sana, huko ndiko kuupalilia, tunatengeneza kitu kisichokuwepo na kukiingiza vichwani mwa Watanzania, hii ni hatari!" alionya Askofu Kakobe.
Alipuuza propaganda hizo na kueleza kuwa kama kuna udini, mbona mwaka 2000, alipanda jukwaani kumpinga mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Benjamini Mkapa (ambaye ni Mkristo mwenzake)?
Alisema kadhalika mwaka 2005, baadhi ya maaskofu walipoibuka na kudai mmoja wa wagombea ni chaguo la Mungu hakuna aliyedai kuwepo tishio la udini kwenye uchaguzi huo.
"Mwaka 2005 napo wakaibuka baadhi ya maaskofu wakasema mmoja wa wagombea ni chaguo la Mungu, udini haukusemwa, leo hii haya yanatoka wapi? Au wameona kuna mtu fulani hatajwi ndio maana", alisema Askofu Kakobe.
Alitoa mfano wa Kanisa lake kubadili ratiba ya ibada siku ya uchaguzi mwaka huu ambapo badala ya kufanyika Jumapili, itafanyika Jumamosi ili kutoa nafasi kwa waumini kupiga kura. alisema jambo ambalo hilo si udini bali ni kuwapa nafasi waumini hao kutekeleza haki yao ya msingi kwa taifa.
Alisisitiza kwamba jambo hilo si udini hata kidogo na mamlaka husika zilipaswa kumpongeza kwa hatua hiyo ya kuchangia kufanikisha shughuli ya upigaji kura ambayo ni haki ya msingi kikatiba kwa kila raia mwenye sifa.
"Kwa mfano hapa kwangu mimi nimesema ibada zitakuwa Jumamosi badala ya Jumapili ili kuwapa waumini nafasi kushiriki vyema kupiga kura. Mimi nilidhani wangefurahi na kutupongeza kwa kusaidia kufanikisha zoezi hilo. Hapa kwangu wote ni mashahidi, sijamwambia yeyote amchague nani. Kila mtu ana utashi wake. Kumbe basi kila chama kina kura hapa. Wanaopinga mkakati huu wanajua waumini hawa watampigia kura nani? Bila shaka wako watakaowapigia kura Chama tawala, na wako watakaowapigia kura vyama vya Upinzani.", alisema Askofu Kakobe.
Askofu Kakobe alilinganisha sera zinazoendelea kunadiwa majukwaani na bidhaa zinazouzwa madukani na kufafanua kwamba wateja daima huvutwa na kununua bidhaa bora.
"Sera ndizo zinazomuuza mgombea, sera ni sawa na bidhaa sokoni au madukani kama vile shati na gauni. Mtu yeyote wa dini yeyote atavutwa na nguo kutokana na kuridhishwa na ubora wake. Shati bora litanunuliwa na yeyote awe muislamu, mkristo hata mpagani, kudai mtu ananunua kwa misingi ya dini ni dhana potofu ya kufikirika.
"Bidhaa ikiwa nzuri mtu yeyote ataihitaji, hata awe mpagani atainunua tu", alisema Askofu Kakobe na kuzidi kufafanua:
"Kama sera ni nzuri zitanunuliwa na mtu yeyote mwenye dini na asiye na dini. Sera nzuri ni bidhaa inayouzika kwa kila mtu. Ni jukumu la wanasiasa kufafanua sera zao zieleweke kwa wananchi. Hapa hakuna suala la udini.
"Wagombea wajue sera ndizo zinazowauza, unaweza kuuza sera zikakataliwa usitafute visingizio, zitengeneze zikubalike. Kelele zinazopigwa sasa kuhusu udini ni vitu vya kufikirika. Ukizungumza sana kitu hata kama cha uwongo baadaye vitakuwepo, ukitaja sana ukabila, udini ndio unaviumba", alionya.
CHANZO: Majira 25.10.2010