Heshima kwenu wanajamvi,
Wakuu leo asubuhi nimeamka na tafakari juu ya siasa na muelekeo wake hasa kipindi hiki kilichogubikwa na sakata la Dowans na suala la katiba mpya.
Ukifuatilia mjadala mzima wa masuala haya unabaini serekali na chama tawala haipo kwaajili ya kuwatetea,kuwakilisha,kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida.Serekali ya sasa ni kikundi kidogo cha wateule ambao wapo kwaajili ya maslahi yao binafsi na familia zao.
Serekali na chama tawala wanapokosa hoja za kutetea ubadhirifu,ufisadi au maamuzi mabovu wanakimbilia hoja za kugawa wananchi kupitia mdudu udini.Ni ajabu sana mkuu wa nchi anatoa hotuba ndani ya bunge kwamba sasa Tanzania kuna udini pasipo kuchukua hatua madhubuti za kuondoa udini badala yake tunashuhudia chama chake kikiwatumia mashehe kuunga mkono mauaji ya polisi [Maandamano ya Arusha].
Udini Tanzania umeletwa,unakuzwa,unapaliliwa,unatiwa mbolea na kumwagiliwa maji na CCM kwa nia ya kuendelea kubaki madarakani pasipo mwisho.Bahati mbaya wapanga mkakati wengi ndani ya CCM ni watu wenye uwezo mdogo wa kuona mbali wamewekeza kweye siasa za muda mfupi sana.Wapo wanaCCM wenye uwezo mkubwa sana wa kufikiri na kupanga mikakati mizuri kwaajili ya wananchi lakini bahati mbaya CCM ya sasa hawana nafasi na wanachama wa aina hiyo wenye nafasi nzuri ni wanachama wa aina ya Tambwe Hiza na Yusuph Makamba.
Kuthibitisha hoja yangu kwamba CCM wamekuwa wakitumia karata ya udini muda mrefu sana nitaanzia uchaguzi wa mwaka 1995.CCM waliwaamisha watanzania wengi kwamba CUF ni chama cha kiIslam lakini kauli hizo walikuwa wanakwepa kuzitoa kwenye mikoa yenye waIslam wengi kama Lindi,Tanga na pwani.Wakati huo huo walitumia wanazuoni waIslamu kupaka matope mgombea wa NCCR mageuzi A L Mrema kwamba ni adui mkubwa wa waIslam kanda za kaseti zitisambazwa kwenye misikiti na vijiwe vya kahawa bila kizuizi chochote.CCM walikuwa wakichekelea sana dhambi hiyo kwakuwa ilikuwa inawanufaisha na kuwahakikishia ushindi.Sheckh wa mkoa wa Arusha Bwana Kisiwa alijengewa nyumba maeneo ya Njiro na mheshimiwa B Mkapa kwa kufanisha zoezi la kutawanya kanda kwenye misikiti yote ikiwa ni pamoja na kutoa mihadhara ya kumbomoa A L Mrema.
Mwaka 2005 CCM waliweka ndani ya ilani yake kipengele cha kuanzisha mahakama ya Kadhi kama wananchi wangewapa ridhaa ya kuongoza tena.CCM si wajinga walijua wangeanzisha mahakama ya kadhi wangekuwa wanavunja katiba ya JMT walichokuwa wanahitaji ni kurejea magogoni kwa gharama yoyote.
Mwaka 2010 mgombea wa CHADEMA Dr W Slaa alikuwa tishio kwa mgombea dhaifu wa CCM mheshimiwa Jakaya Kikwete amaye alikuwa ameshindwa kusimamia vyema rasilimali za watanzania na vita ya ufisadi.Karata ya udini ikaanzishwa tena kwamba Dr W Slaa ni mkatoliki wakasahau Nyerere pia alikuwa mkatoliki.Wakajitahidi sana kuwasahaulisha watanzania sifa za Dr W Slaa dhidi ya ufisadi wapo watanzania wajinga walioingia kwenye kundi hili siwezi kuwalaumu kwasababu sifa kubwa ya mtanzania ni kusahau haraka.Bahati nzuri wapo watanzania zaidi ya milioni mbili waliokataa usungura wa CCM.
Mwaka huu wa 2011 maandamano ya Arusha CCM walijitahidi sana kuyageuza na kuyapa sura ya udini bahati mbaya kama nilivyotangulia kusema awali CCM hawana wana mkakati wenye akili sawa sawa.Mpaka mwaka huu umalizike tutashudia wenyewe mikakati ya kutupachikia udini zikiendelezwa kwa juhudi kubwa kwakuwa watawala wetu hawana tena majibu ya matatizo yetu.Usishangae maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu yakahusushwa na udini !.
Matatizo ya watanzania si udini viongozi wanaokimbilia hoja za udini hawana sifa za kuongoza.Shida za wananchi ni maradhi,ujinga na umaskini viongozi waonyeshe njia sahihi za kukabiliana nayo.Athari za kuporomoka kwa shilingi y kitanzania kunawaumiza waIlsam na waKristo,upanda holela wa bei ya umeme hakuchagui kama wewe ni mkristo au muIslam wote tutaumia sana tusikubali kutumiwa.