Ni nani anaweza kutatua matatizo ya watoto kuchelewa/kushindwa kuongea?

Ni nani anaweza kutatua matatizo ya watoto kuchelewa/kushindwa kuongea?

Joined
Oct 5, 2018
Posts
33
Reaction score
58
Swali kubwa ninaulizwa na wazazi/walezi kila siku juu ya matatizo ya watoto kuchelewa kuongea ni: Nani anaweza kunisaidia kulimaliza tatizo hili la kuchelewa kuongea kwa mtoto wangu?

Binafsi huwa nakosa jibu rahisi la kuwapa wazazi/walezi moja kwa moja mpaka nimuone mtoto na shida yake ni ipi. Kila mtoto anatakiwa asaidiwe na mtaalamu anayeendana na tatizo lake.

Kama nilivyoandika katika makala yangu iliyopita, sababu za watoto kuchelewa kuongea ni nyingi, hivyo, kila tatizo linatakiwa litatuliwe na mtaalamu husika kuendana na tatizo na chanzo cha tatizo la mtoto au kwa wataalamu kutoka kada mbalimbali kushirikiana. Nimeona watoto wengi wakipatiwa huduma na mtaalamu mmoja na kushindwa kukaa sawa kwa wakati kutokana na wataalamu kutaka kuyatatua baadhi ya matatizo bila kushirikiana kuendana na taaluma zao.

Wapo watoto wanaohitaji kupewa tiba za madawa na upasuaji, upewaji wa vifaa na mazoezi, msaada wa lugha na elimu n.k Tatizo la watoto kuchelewa au kushindwa kabisa kuongea binafsi naona ni tatizo ambalo haliwezi kutatuliwa na mtaalamu wa kada moja tu. Nafikiri wataalamu wa kada mbalimbali wanaweza kuwa na mchango tofautitofauti katika kutatua tatizo hili:-

Katika makala hii nimelijibu swali la wazazi/walezi wengi, swali la : Nani anaweza kuwamsaada katika suluhu la tatizo hili:-

1. Wataalamu wa elimu maalumu ya watoto. Walimu/waelimishaji wanajihusisha na uhamasishaji, uchocheaji na ukuzaji wa fikra za watoto kwa kuwafundisha mambo mapya. Kuchelewa kwa lugha kwa watoto ambako hakuhusishi magojwa au matatizo ya kimwili ambayo yanahitaji tiba ya kimadawa (medical treatment au upasuaji mdogo (Minor Surgery) kama midomo kushikana au majeraha kwenye ubongo wa mtoto kunaweza kabisa kutatuliwa na wataalamu wa elimu maalumu ya watoto. Walimu/waelimishaji wa elimu maalumu wanaweza kumsaidia mtoto akajifunza lugha na kuitumia lugha. Wanaweza kumsaidia mtoto kujiamini na kujieleza mbele za watu. Wanaweza kumsaidia mtoto kufanya mazoezi. Cha muhimu mtaalamu huyu ni lazima awe na historia ya matibabu ya mtoto wako kutoka hospitali yoyote iliyopo karibu na wewe.

Ni ngumu mtaalamu wa elimu maalumu kujua anapambana na nini kama mtoto hatofanyiwa vipimo na uchuguzi kutoka hospitalini. Wataalamu hawa wa elimu maalumu wanapatikana kwenye shule mbalimbali nchini, ambao pia unaweza kuwaajiri kama walimu binafsi wa tution (Private tutors) ili wakusaidie kupata matokeo ya haraka.

2. Wataalamu wa lugha na matamshi. Hili ni kundi lingine linaloweza kutoa suluhu la baadhi ya matatizo ya lugha au kuchelewa kuongea kwa watoto. Kuna matatizo mengi ya kuchelewa kuongea kwa watoto ni ya kilugha tu, yaani hayahitaji vifaa, madawa wala upasuaji bali ni kujengewa uwezo wa kuisikia, kuielewa na kuizungumza lugha. Wataalamu wa lugha wanaweza kukifanya hiki vizuri zaidi kwani kipo ndani ya eneo la utaalamu wao. Wataalamu hawa wanapatikana katika taasisi mbalimbali za elimu au za lugha.

3. Wataalamu wa sauti (Audiologist). Kundi hili wanaweza kufanya mambo mengi katika kupambana na tatizo la kushindwa au kuchelewa kuongea kwa watoto lakini wanaweza kufanya vizuri zaidi kwenye matatizo yanayosababishwa na watoto kushindwa kusikia vizuri. Wao wanaweza kumpatia namna nzuri ya kuwasiliana kwa ishara, kuongeza uwezo wa mtoto kusikia, kumpatia vifaa vya kiteknolojia vyenye kuweza kumpa uwezo wa kusikia zaidi na mengineyo. Kwa Tanzania wataalamu hawa wanapatikana sana kwenye hospitali mbalimbali.

4. Wataalamu wa akili na magonjwa ya akili. Hawa wana nafasi yao kubwa sana katika kuwasaidia watoto katika tatizo hili la kuchelewa kuongea hususani endapo sababu kuu ya kuchelewa kwa mtoto kuongea ni matatizo ya akili. Mtoto mwenye majeraha kwenye ubongo au usonji (autism) anaweza kuhudumiwa vizuri sana na mtaalamu wa akili kuliko ambavyo atahudumiwa na wataalamu wengine. Kwa maono yangu binafsi nafikiri, ili mtaalamu wa akili na magonjwa ya akili afanywe vizuri zaidi atatakiwa ashirikiana na kusaidiwa na wataalamu wengine wa matatizo ya kuchelewa kwa lugha kwa watoto.

5. Wazazi na walezi wa mtoto. Katika dunia ya sasa maarifa yapo wazi juu ya kila kitu. Kama mzazi/mlezi anaona mtoto wake ana tatizo la kuchelewa au kushindwa kuongea na hawezi kumudu gharama za kuwalipa wataalamu kila siku, basi anaweza kuamua kujielimisha kwa kusoma au kufundishwa na wataalamu ili aweze kumsaidia mtoto wake yeye mwenyewe. Mambo mengi yanayofanywa na wataalamu wazazi/walezi wanaweza wakayafanya wao wenyewe. Kwa mfano kumfanya mtoto aanze kujifunza lugha na kuitumia kuwasiliana vizuri. Kumfanyisha mtoto mazoezi mbalimbali kama vile ya mazoezi ya kinywa na mengineyo.

Tatizo hili linachukua sana muda kulimaliza endapo mzazi/mlezi atawategemea wataalamu tu kwani hata kama watamuhudumia mtoto wako, wanaweza kumuhudumia mara moja kwa wiki. Tatizo hili linaweza kuchukua muda mfupi kutatuliwa kama mzazi/mlezi atashiriki moja kwa moja, kikaribu.

Hitimisho: Ni muhimu wazazi/walezi mkitambua ya kwamba tatizo la kuchelewa kuongea au kushindwa kabisa kuongea kwa watoto ni jambo ambalo kwa asilimia kubwa lipo mikononi mwenu kulitatua hivyo hata kama utaenda hospitali au kwa mtaalamu yeyote yule jitahidi kujielimisha wewe mwenyewe ili uwe mstari wa mbele kumsaidia mtoto kuweza kutumia lugha vizuri. Pia, ni muhimu kila mtu akatambua ya kuwa tatizo hili ili liweze kutatuliwa vizuri ni lazima wataalamu wa kada tofauti tofauti kuweza kushirikiana kwa namna moja ama nyingine.

MWISHO​
 
Back
Top Bottom