Naona Katibu Mkuu wa CCM ameanza kulifanyia kazi suala la ardhi. Hii imeriporiwa na gazeti la Mwananchi la Leo
Agizo la CCM kwa Wizara ya Ardhi
THURSDAY MAY 20 2021
Dar es Salaam. Katibu mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ameitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuongeza kasi ya utatuzi wa migogoro ya ardhi inayosababisha malalamiko kwa wananchi.
Ameyasema hayo leo Alhamisi Mei 20, 2021 katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma huku akirejea ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/25 inayoeleza kasi ya umilikishaji wa ardhi kwa wananchi.
"Hatua hii itawafanya wananchi wawe na usalama zaidi wa maeneo yao na ni muhimu. CCM italifuatilia kwa karibu kuona utekelezaji wake," amesema Chongolo.
Amesema kwa sasa ni wananchi wachache wanaomiliki ardhi kisheria, huku asilimia kubwa wakimiliki kiasili au bila utaratibu wa kisheria, ambapo mtu ananunua ardhi na kujenga nyumba ya thamani kuwa na umiliki halali wa kiwanja hicho.
Aidha, Chongolo amesema chama hicho kinaelekeza kufanyika kwa uthaminishaji na fidia kwa wananchi waliotwaliwa maeneo yao kwa shughuli za umma pamoja na uimarishwaji wa mfuko wa fidia.
"Viongozi wote wa Serikali kuanzia ngazi za vijiji na mitaa mpaka wizara wanapaswa kuhakikisha wanatatua na kuandaa siku mahsusi za kutatua migogoro ya ardhi kwa haraka na wakati.”
"Chama kinaelekeza kumaliza migogoro ya ardhi katika Wilaya za Kondoa, Kitero, Kongwa, Morogoro, Kilombero na pembezoni mwa hifadhi mbalimbali ambayo imekuwepo kwa muda mrefu na kuwasumbua wananchi," amesema.