Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bw. Antony Blinken alifanya ziara nchini Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC na Rwanda wiki iliyopita, ambapo alitangaza "mkakati mpya wa Marekani kuhusu Afrika Kusini mwa Sahara." Hata hivyo, mkakati huo hauna jipya na umeonyesha kuwa serikali ya Marekani inayoongozwa na rais Joe Biden bado haijajifunza kutokana na makosa ziliyofanya serikali za awamu zilizopita kuhusu sera za Afrika.
Kwanza, Marekani inaendelea kuiweka Afrika katika ushindani wake na nchi nyingine kubwa, licha ya kauli ya Bw. Blinken kwamba "sera ya Marekani kuhusu Afrika haiilengi nchi nje ya Afrika , ila tu uhusiano wa wenzi sawa." Lakini gazeti la "Foreign Policy" la Marekani lilichapisha makala ikisema Marekani inasisitiza kuwa haizingatii ushindani wa siasa za kijiografia, lakini mkakati wake huo mpya kuhusu Afrika umejaa maudhui yanayolenga Russia na China.
Akielezea mkakati huo mjini Pretoria, Afrika Kusini, Bw. Blinken alisema "Marekani na dunia zinatazamia nchi za Afrika kutetea utaratibu wa kimataifa wanaouunda," akilenga mgogoro kati ya Russia na Ukraine. Pia katika hotuba yake aliishutumu China kwa kuendeleza maslahi yake ya kibiashara na kijiografia barani Afrika, kudhoofisha uwazi, na kuharibu nyanja muhimu ya mawasiliano kati ya Marekani na watu na serikali ya nchi za Afrika. Kuhusiana na hayo, waziri wa uhusiano wa kimataifa na ushirikiano wa Afrika Kusini Dkt. Naledi Pandor alimwambia Bw. Blinken kuwa "Afrika Kusini ni nchi huru, na hairuhusu nchi nyingine kutaja kile kinachoitwa 'kuchagua upande', na lazima kusiwe na kitu kama Afrika itaadhibiwa na Marekani kwa sababu ya kufanya jambo fulani."
Pili, Bw. Blinken haonekani kuelewa kwamba viongozi wa nchi za Afrika wamechoka na kuambiwa kuhusu mawazo ya demokrasia na haki za binadamu ambayo hata Marekani yenyewe imeshindwa kuyafikia. Mkakati huo mpya kuhusu Afrika unasisitiza kuwa Marekani itaipatia Afrika faida za demokrasia na usalama katika miaka mitano ijayo. Nchini DRC, Bw.
Blinken alitangaza kutoa fedha za kuimarisha kile kinachoitwa "uwazi wa uchaguzi na usimamizi wa uchaguzi" ili kuingilia kati uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utakaofanyika mwaka kesho. Nchini Rwanda, Marekani imeonyesha maana ya “kutoendana kwa maneno na matendo” kwa uwazi. Kwanza, aliitaka serikali kumwachia huru Bw. Paul Rusesabagina aliyeigizwa katika filamu ya ''Hotel Rwanda'' ambaye kwa sasa ni raia wa Marekani, na wakati huo huo kwa mujibu wa kile kinachoitwa ripoti, inaitangazia serikali ya Rwanda kuunga mkono waasi wa M23 katika nchi jirani ya DRC.
Juu ya hilo, kuna mwanamtandao alisema, "Rwanda si nchi ambayo unaweza kucheza na sheria. Tumechoshwa na ripoti zako za uongo kuhusu haki za binadamu." Hali halisi ni kuwa waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Vincent Biruta alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari pamoja na mwenzake wa Marekani Bw.
Antony Blinken kuwa “tunawataka washirika wetu kuheshimu mamlaka ya Rwanda, sheria na taasisi za Rwanda, na Rwanda haitakubali shinikizo lolote kutoka nje.” Ni wazi kwamba hakuna nchi yoyote barani Afrika itakayokubali kuingiliwa ndani na nchi za kigeni, ikiwemo Marekani, kwa majina ya demokrasia na haki za binadamu.
Tatu, katika mkakati mpya wa Marekani kuhusu Afrika wenye kurasa 17, kuna sehemu moja tu inayotaja Ajenda ya Umoja wa Afrika 2063, ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Afrika. Ni wazi kwamba Marekani haijali hata kidogo nchi za Afrika zinafikiria nini, na maana ya "Marekani Kwanza" bado ina nguvu. Kwa mfano, lengo la kwanza la mkakati huo mpya ni kwamba Marekani itakuza uwazi na jamii wazi barani Afrika.
Mchambuzi wa masuala ya siasa wa Marekani Don DeBar alisema kuwa neno "jamii wazi" lina kejeli sana kutokana na hali ya sasa ya sera ya Marekani barani Afrika. Mantiki nyuma ya lengo hili ni kwamba Afrika kwa sasa inakaliwa kwa mabavu na nchi fulani, na Marekani imetengwa mbali. Kwa hiyo, Marekani inazitaka nchi za Afrika kuwa wazi ili izitawale yenyewe. Wakati wa ziara yake hii Bw.
Blinken hata alisema wazi kwamba utajiri wa Afrika katika suala la idadi ya vijana, madini muhimu na mikakati utalifanya bara hilo kuwa kipaumbele kwa sera ya mambo ya nje ya Marekani. Kwa mfano wa DRC, utajiri wa Cobalt na Coltan nchini humo ni malighafi muhimu kwa vifaa vya kielektroniki, vifaa vya anga ya juu na teknolojia ya nishati safi. Ili kujenga minyororo ya ugavi, Marekani haipendi kuziachia rasilimali nyingi za Afrika kwa nchi nyingine, na inajaribu kupata faida ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya uwekezaji katika madini na nyanja nyinginezo.
Katika miaka ya hivi karibuni, mfululizo wa ghilba za serikali ya Marekani zimeharibu maslahi ya nchi za Afrika, na hivyo kudhoofisha sana uaminifu wake kwa Afrika. Sasa inarejea Afrika kwa kuimba kujenga ushirikiano kati ya Marekani na Afrika katika karne ya 21, lakini "mkakati huo mpya kuhusu Afrika" unaonyesha wazi kwamba Marekani bado imebweteka kwenye fikra za kibeberu -- ikipuuza mahitaji ya Afrika na kuitumia Afrika kama daraja la mikakati yake ya ndani na nje, jambo ambalo halitakubaliwa na nchi na watu wa Afrika.