Ukisikia kiitikio cha Wimbo wa Uswazi Take Away wa Said Nassor ‘Chegge’ lazima utajiuliza mara mbilimbili sauti ya kike inayosikika ni ya nani.
Jibu ni rahisi! Ni mmoja kati ya wasanii wa kike wasioshikika katika Bongo Fleva. Anaitwa Diana Malaika Exavery Clavery ama wengi tumezoea kumuita Malaika.
Ukiachana na Uswazi Take Away, Malaika anatambulika na ngoma kama Mwantumu, Nenda pamoja na Saresare aliyomshirikisha producer, Mesen Selekta wa De Fatality Music.
Pia katika utoaji tuzo za Kili Music mwaka 2015, Malaika alikuwa mmojawapo katika vipengele vya tuzo hizo akichuana na Lady Jay Dee, Linah, Grace Matata pamoja na Vannesa Mdee akiwania kipengele cha Mwimbaji Bora wa Kike Bongo Fleva ambapo tuzo ilikwenda kwa mwanadada, Vannesa Mdee.
Anasoma shule ya wasichana ya Kibosho huko Moshi. Na alipomaliza kidato cha nne akaingia jijini Dar na kufanya ‘field’ kwenye Ofisi za Uzazi na Vifo (RITA) na wakati mwingine alikuwa akifanya kazi kwa mtayarishaji wa video, Adam Juma wa Visual Lab kama ‘make up artist.’
Kitendo cha kuwa na Adam kwa muda mrefu na wasanii wengi wanakuja mahali pale, basi ikawa rahisi kwa Adam kumuunganisha na Chegge. Hapo ndipo historia ya muziki wake ilipoanzia rasmi.