Kama alivyopinga Kenyatta hilo la kuwa na dola/serikali moja, hata mimi nalipinga leo hii, haya mataifa tuko tofauti kabisa, kimtazamo, kimalengo, Mtanzania na Mkenya tuko tofauti kwa kila hatua, nimeishi Tanzania kwa muda mrefu hivyo najua ninachokisema.
Ingekua rahisi kutuunganisha kwa miaka ya zamani hata kabla ya uhuru, enzi zile Waafrika walikua bikira kimtazamo na kimawazo. Lakini baada ya mifumo ya kikoloni ya kiutawala, kila mmoja akawa na mtazamo tofauti. Kwa jinsi Mkenya alivyo mshindani, mwenye kuhoji kila kitu na kila hatua, kumuweka aishi na Mtanzania ambaye yeye amezoea kuendeshwa endeshwa, kwamba yupo yupo tu, kila kitu kwake shwari, utakua unawavuruga na ndio maana likija suala la kufunguliana, kwa Afrika yote Tanzania huwa anaogopa sana Mkenya. Mfumo wa ujamaa wa Nyerere uliwalemaza Watanzania.
Suala la muungano ambao tunaujadili humu, sio kwamba tunataka tuungane tuwe nchi moja chini ya serikali moja, la hasha, haliwezekani na baadhi yetu tutalikatalia mbali, tunachokitaka ni kuwa na soko la pamoja, kwamba Mkenya anaweza akauza matikiti yake Misri bila kupitia urasimu wa kiajabu ajabu.
Leo hii watu tumewekeana mipaka yaani hata gunia la mihogo kuvuka nalo mpakani unavurugwa utadhani ueiba benki kuu na kuhujumu uchumi. Hili nilishangaa lipo hata baina ya Tanganyika na Zanzibar, pale kuvusha chochote unalipia kodi na ukaguzi wa ajabu ilhali ni nchi moja chini ya Jamhuri moja.
Kuhusu ugunduzi wa gesi, Nyerere hakugundua chochote, yeye alijua vipo lakini hakua na uwezo huo wa kitaalam, ndio akafanya busara ya kusubiri mpate elimu, lakini la kushangaza miaka yote hiyo imepita, mumepelekwa vyuoni lakini mumeganda, hamna tofauti ya Mtanzania wa leo na yule wa enzi zile, imebidi mjukuu wa mbeberu aje aigundue hiyo gesi, akawaandikia mkataba wa kisanii nyie wajukuu wa Nyerere na kuanza kuchuma na kuipeleka kwao. Hicho hicho alichokua anazuia babu yenu akisubiri wajukuu waelimike, ndicho kinaliwa na wajukuu wa mbeberu na kuwaacha wajukuu wa Nyerere kuwa maskini wa kutupwa.