Nigeria jana Jumatatu ilirejesha huduma ya usafiri wa treni kati ya mji mkuu Abuja na mji wa kaskazini wa Kaduna, miezi minane baada ya kusitishwa kufuatia moja ya mashambulizi makubwa zaidi kutokea nchini humo.
Machi 28, watu wenye silaha walitumia vilipuzi kulipua reli na kushambulia kwa risasi treni iliyokuwa ikisafiri kati ya Abuja na Kaduna, na kusababisha vifo vya watu wanane, wengine 26 kujeruhiwa, na idadi isiyojulikana ya abiria walitekwa nyara.
Mateka waliachiliwa kwa vikundi kufuatia mazungumzo na watekaji, ambao waliaminika kuwa wamechukua fedha nyingi kutoka kwa familia za mateka hao.