Niko safarini mawazo mengi kweli kichwani, najiuliza kama kweli nimefanya kitu sahihi. Wazazi wangu najia wana roho nzuri sana lakini hili suala nililofanya litaleta picha gani kwao ?? Isitoshe nimefanya maamuzi ya haraka wakati bado mimi mdogo na kwa asilimia kubwa sana nawategemea wao. Haya nikajiuliza tena; Vipi kuhusu ndugu zangu sasa, watalichukuliaje hili jambo ?? Niliwaza mengi sana siku ile.
Safari ikaisha na tukashuka stendi, wale wamama tuliosafiri nao walikuwa wananiangalia macho ya hiana sana lakini nikasema wangenionesha heshima huenda tusingefika hapa tulipofika. Yule mama Mchagga alikuwa ananiangalia na mimi nikamkazia macho hadi yule dada wa jirani akanimbia "Kaka Malcom ona wale wamama wanavyokuangalia!" nikaropoka kwa nguvu kidogo "Achana nao, watu wazima hovyo" kuna mzee moja jirani pale alisikia akacheka akaniita mwanangu njoo. Mimi nikamfuata pale alipo, huku anatabasamu akaniambia bado tu hayajakuisha moyoni ?? Mimi sikujibu kitu, akaendelea kusema kwamba mimi ni jasiri lakini nijitahadi kuitawala hasira yangu, akasema "Hawa mama zetu ndivyo walivyo, wameumbwa kuongea sana hivyo usiwachukie kabisa, pili hao ni wakubwa zako"
Nilisikiliza busara za yule mzee halafu nikaagana naye nikiapa kichwani mwangu kwamba sintabishana tena na wanawake.
Nikakodi taxi ambayo ilinifikisha mpaka nyumbani kwetu. Ile kabla sijafika ndani ndugu waliokuwepo wakiongozwa na dada zangu walitoka nje kunipokea kwa furaha, lakini ghafla yule binti wa balozi alivyoshuka na mtoto furaha ikawapungua usoni. Nikawaona wanaanza kuangaliana na nikajua nini wanakiwaza kwasababu yule binti wa balozi tulikaa naye mtaa moja miaka ya nyuma na alicheza na dada zangu. Basi wakajibaraguza kama wanampokea mtoto na kumkaribisha yule binti na kuulizana habari za siku; Lakini mimi nikacheka nikajua kabisa hawa wanafiki wangu wanawaza ujinga kichwani.
Nilivyoingia ndani mama akanipokea na kumkaribisha yule binti, basi alikuwa amechoka sana akaomba wampeleke chooni basi dada yangu akaambiwa ampeleke akajipoteza na kumwita Msichana wetu wa kazi ampeleke. Ile yule dada ametoka tu pale sebuleni huku mama kampokea yule mtoto, pipo zikakimbilia kukaa kwenye kochi langu na kuanza kuuliza. "Malcom umefanya nini ?, mtoto wa nani huyu ?" mimi nikacheka tu, mama akakaza sura na kuuliza kwa ukali unacheka nini sasa ? Yaani Malcom umeanza michezo ya kaka zako kweli ? Akaniambia nilikuwa nang'ang'ania kwenda kwenye ule mkoa wakati niko likizo form five na six kumbe naenda kufanya ufuska: Akasema sasa unapata vihela kidogo, ukipata nyingi si ndiyo utanijazia watoto hapa ndani ? Huku dada zangu wanacheka hawana mbavu, wanasema kweli watu wakimya ni hatari kwasababu mimi katika kaka zangu ndiyo nilikuwaga domo zege pale mtaani: Wao walikuwa wananiita KIAZI au ANDAZI.
Mimi nikawasimulia ule mkasa wote na yule dada akawapa ile barua ya mzee wake na mama akaisoma na kuvuta pumzi ndefu kweli. Akaniangalia na kunyamaza akarudisha ile barua kwenye bahasha na kujaribu kuweka tabasamu la kulazimisha usoni. Nilijua kabisa hawezi kumkataa yule mtoto lakini kitendo cha mimi kujichukulia maamuzi mazito kama yale kilimkera sana. Dada zangu wakaanza kuntania na kuuliza jina la mtoto lakini hata jina mtoto mwenyewe hana; Dada niliyefuatana naye mimi akampa jina yule mtoto akamwita jina ******** , mama akamalizia ****** MALCOM huku akielekea chumbani kwake. Huku sebuleni watu hawana mbavu wanaleta masikhara tu.
Kufanya hili simulizi fupi,
Siku ile sikuwa na raha kwasababu nilikuwa nawaza mwenye nyumba akirudi na alivyo anapenda Ubabe hasa kwangu pale ndani pangewaka moto. Mwishowe usiku alirudi na walikaa sana chumbani na mama na akaalia chakula mle chumbani kitu kisicho cha kawaida. Mara dada mkubwa aitwe mle chumbani na akitoka naona hataki kabisa kusema na mimi. Mwishoni nikaitwa huku miguu inatetemeka lakini nikasema potelea pote, ntapambana kiume. Baba aliniuliza "Hivi wewe bwana mdogo umejiona umekuwa sana siku hizi ?. Hivi haya maamuzi unajichukulia tu unadhani hii nyumba ni yako ?? Haya hebu niambie nini kilikutuma kufanya hivi ?" Mimi mara ya kwanza sikujibu nikamwangalia mama nikijua kabisa atanisaidia kujibu kwasababu tuliongea naye mchana kwa kirefu. Heee, mama naye kaniruka futi mia kabisa akasema "Unaniangalia mimi, mjibu baba yako" Mzee kanitolea macho na yamekuwa mekundu mwili wake unapepesuka hasira.
Bahati mbaya sana yule mtoto akaanza kulia sana kule nje, mama na sista walivyosikia ile sauti wakacheka kwa nguvu sana. Mama akasema "tunacheka utafikiria ni mazuri" . Mimi nikakaza nikawaambia kwanza wanisamehe kwa kile kitendo nilchofanya, lakini kiukweli nilifanya vile kwasababu nilimuonea yule mtoto huruma. Mama akachochea zaidi akasema unaona huruma lakini hapa nyumbani hakuna wa kumlea huyo mtoto kibaya zaidi wao wanaelekea uzeeni. Walivyotulea na kutusomesha sisi inatosha hivyo kwanini mimi sikuwaonea huruma ? Mzee alisema ananipa nauli yule mtoto wa balozi ni msindikize na amrudishe yule mtoto alikotoka. Akasema kama ni ubinadamu kwanini yule Mzee Balozi na yule Mhindi hawakukubali kumpokea huyo mtoto.
Tulikwaruzana sana nikapandisha hasira nikauliza mbona ninyi mmelea watu baki hapa nyumbani ambao mpaka leo hii hata fadhila hawakumbuki. Nikawapa ni mifano hai kabisa kwamba fulani na fulani walikataa kumpokea mdogo wangu nyumbani kwao alivyokuwa anaanza shule ilibidi alale hotelini. Mzee akasimama ananisogelea kwa ukali, anauliza "Wewe balehe yako imepanda hadi kichwani eeh, yani umeota vindevu hivyo unajihisi na wewe umeshakuwa baba?" Ile nataka kujibu "Akaongezea jingine, hivi unamletea mama yako mzigo nu mke wako huyu ? Haya mimi niliwalea wale watu kwasababu nina nyumba yangu na pesa zangu, wewe una nyumba yako iko wapi ?" Nikawa mdogo ghafla maana najua huyu jamaa akisimama huchelewei kupigwa kichwa au ngumi za uso. Nikasema tu naomba wanisamehe lakini wamfikirie yule mtoto. Sista akasema Malcom umekosea sana, kwanza hujui hata huyo mtoto atakuwa amewekewa nini, anaweza akawa na mikosi na misinambi pale nyumbani pasikalike kabisa kikubwa hatujui ana magonjwa gani, anaweza akawa na Ukimwi halafu hapa nyumbani ukaja kuleta balaa.
Akili ya kumrudisha yule mtoto ilikuja na mzee mzee akamaliza kile kikao, mimi nikaenda kulala nikiwa nimekata kabisa tamaa. Nyumba yote ilikuwa na ukimya siyo kidogo basi usiku ule nilichelewa sana kulala nimejaa mawazo na kujiona mjinga sana kwasababu nilichukua maamuzi ya kijinga, nilipata usingizi mida kama ya saa tisa hivi. Ile nimelala naona mtu kaja kaniamsha, nastuka nakuta Baba. Mida kama ya saa kumi na nusu usiku, nikajua huyu Mzee ananiamsha niende Stendi mapema maana ni mtu mwenye misimamo sijapa kuona. Lakini cha kushangaza sauti yake ilikuwa ya kipole sana siku ile, akaniambia vaa twende. Mimi nikaswaki kidogo na kuanza kubeba nguo, akanifuata chumbani akauliza mbona nachelewa nikasema napaki nguvo, akasema unapaki unaenda wapi ? Nikasema si ulisema safari leo ? Akanijibu niachane na hizo nguo twende. Tuliondoka usiku ule tukaenda kukaa sehemu moja hivi na lile giza, moyoni nawaza sijui anaenda kunipa laana gani huyu mzee sasa.
Akaanza kuniuliza Malcom mwanangu, umejisikia vibaya nilivyoongea na wewe jana ?
Mimi kujibaraguza nikaangalia chini tu, nikasema hakuna baba mimi ndiyo mwenye makosa.
Akasema bado sijajibu swali lake, mimi nikanyamaza tu. Akaniambia anajua nimejisikia vibaya ukichukulia mimi huwa sipendi kukaripiwa mbele za watu kama mtoto. Akaniambia hivi "Siku nyingine usiwe mtu mwepesi kuchukua tu maamuzi ya haraka kwasababu huwezi kujua huyo mtoto hata kama ni mtu. Ule mkoa una mambo mengi sana na kizazi chenu siku hizi mambo ya Ushirikina hayapo nje nje" Baba yangu siyo mtu wa kuzungumza haya mambo na nilishangaa sanaa siku ile anayazungumzia. Akanitajia mambo mengi sana, akasema unawezakuta mtoto aliibwa sehemu na wewe ukaja pata matatizo tu yasiyo na msingi.
Kikubwa alichosema akasema umefanya jambo la kibinadamu sana MALCOM lakini siku nyingine nishirikishe Mzazi wako.
Yeye anajua kwamba mimi nilikuwa na nia njema tu lakini nikumbuke kuwa pale nyumbani kuna watoto wa kike na wadogo zangu. Wangeona kwamba nimefurahia tu kile kitendo basi wanaweza siku wakazaa nyumbani na kufikiria kwamba wazazi watalea tu, mbona MALCOM alileta mtoto asiyekuwa wakwetu na akakubaliwa. Kifupi alisema nimekuwa mtu mzima na haina haja ya kunificha kitu tena, akasema yule mtoto amemkubali lakini sharti ni kwamba mimi nitawasaidia kumlea kwasababu mimi ndiyo niliyemleta nyumbani. Nilifurahi sana na kujiona kama mimi ndiye kidume kweli lakini kubwa ilikuwa ni huruma kwa yule kiumbe asiye na hatia.
NTAREJEA SIYO PUNDE........