Ndugu yangu,
Ahsante sana,
Makala hiyo imeandikwa na rafiki yangu Godfrey Dilunga ( Raia Mwema)
Pamoja na kuwa ni kazi nzuri, lakini mimi nimekiona pia ambacho labda wengi wenu hamjakiona.
Maana, mtu mzima unaweza hata kujifunza kwa mtoto wa miaka sita. Unachotakiwa ni kuwa na utayari wa kujifunza. Kuna siku mtoto wangu wa miaka sita alinifundisha hili; " Niliandaa uji wa ulezi wa asubuhi . Akawa wa kwanza kuamka kabla ya wenzake. Nikamwambia; " Nenda mezani, chai tayari!".
Akaenda, baada ya sekunde chache akaniita; " Baba njoo!"
Nikaenda, akaniangalia usoni na kuniambia; " Baba hii sio chai, huu ni uji!"
Nikakiri mapungufu. Na mapungufu yale kwangu ni ya kimalezi, wengi tunayo. Tukiwa kuruta JKT enzi zile nakumbuka na usomi wetu wa form six, pale kambini Itende JKT, baada ya mchakamchaka wa alfajiri na usafi tuliambiwa na Afande Paul; " Kuruta nendeni mkanywe chai!".
Wote tuliokuwa pale Kambini Itende, wengine tumo nao humu JF ni mashahidi, kuwa pale Itende tulikunywa maji ya moto yaliyochemshwa pamoja na vumbi la kahawa na sukari. Haikuwa chai. Lakini ni nani kati yetu alithubutu kumwambia afande Paul; " Hii sio chai, ni kahawa, ingawa si kahawa hasa!"
Tatizo hilo la kimalezi linatusumbua wengi wetu mpaka hii leo. Unaona kwa macho kuwa bwana mkubwa anakupa chungwa, halafu anakwambia; "pokea embe hili!" Wewe unakubali!
Mtoto wangu wa miaka sita anatupeleka kwenye kutafakari alichoandika ; Godfrey Dilunga; " Nimeona waschotaka kukiona" ( Raia Mwema)
Dilunga anaandika;
"Nguvu ya utulivu na usikivu ya mkusanyiko wa watu zaidi ya 40,000 niliyoshuhudia Ifakara ndiyo iliyojitokeza Lupiro-Mahenge, Njombe, Songea na Iringa."
Anaendelea kuandika; "Kama leo mkusanyiko wa walalahoi zaidi ya 40,000 katika kila mkutano wanakua watulivu, ipo siku utulivu na usikivu ule utafanyiwa kazi na walalahoi hao hao. Siku hiyo itafika kama watawala watazidi kujenga wananchi wa mfano wa mama muuza ndizi." ( Dilunga, Raia Mwema)
Sasa hapa sijamwona aliyehoji na kudadisi uhakika wa anachokiandika Dilunga. Hivi ni kweli pale Ifakara Dilunga aliwaona watu 40, 000? Ifakara sikuwapo, lakini pale Mwembetogwa Iringa nilikuwapo. Watu waliofika pale hawakuzidi 5000. Ukubwa wa uwanja wa Mwembetogwa na maeneo ya jirani hauwezi ukajaa watu zaidi ya 5000 na wakaweza kumsikia anayezungumza achilia mbali kumwona kwa sura.
Ndio tatizo letu, tunapenda kusikia tunavyotaka kusikia, na kuona tunavyotaka kuona. Shilingi ina pande mbili, tuwe na ujasiri wa kuangalia upande wa pili wa shilingi. Ujasiri wa kuangalia tusivyotaka kuangalia, kusikiliza tusivyotaka kusikia. Sina cha kuhofia katika kuandika fikra zangu, maana ni fikra zangu. Fikra huru. Na najua kuwa mimi si malaika, nina mapungufu yangu. Ndio maana tukaitwa wanadamu. Najifunza kila siku, hata ninapokutana na mchoma mahindi pale Kitonga. Kijana aliyeishia darasa la saba, naamini nina nitakachojifunza kutoka kwake. Na kwa mwanadamu, katika yote unayayotakiwa kuyakubali. Usisahau kuukubali ushamba. Nimezaliwa mjini na kukulia mjini, tena Ilala, Dar. Lakini siku zote natanguliza ‘ushamba ' wangu. Ndivyo nilivyo.