Nilitembelea makaburi ya Watakatifu ambayo kisiasa huitwa mashujaa

Nilitembelea makaburi ya Watakatifu ambayo kisiasa huitwa mashujaa

Robert Heriel Mtibeli

Platinum Member
Joined
Mar 24, 2018
Posts
40,153
Reaction score
93,069
NILITEMBELEA MAKABURI YA WATAKATIFU AMBAYO KISIASA HUITWA MASHUJAA

Anaandika, Robert Heriel Mtibeli.
Taikon wa Fasihi.

Basi nikasema, mimi naam ndio mimi mwenyewe. Nitaenda kwenye makaburi. Yalipo makaburi ya Watakatifu.
Tena nikiwa njiani kumbe katika njia hiyo sikujua kuna makaburi mengine ambayo sikujuzwa yapo njia hiyohiyo. Makaburi ya Watakakitu. Mamaa!

Sasa watakatifu na watakatifu waliishi pamoja. Wakatumia jua na mvua moja. Leo wapo ardhi moja lakini maeneo tofauti. Bado nilikuwa nikiwaza.

Sijui kwa nini nilishauriwa niende usiku. Mlinzi wa makaburi ambaye tulijuana kwenye maktaba ya taifa alinikuta nikisoma kitabu kisemacho Dunia ya wafu. Akavutiwa na kitabu hicho. Ndipo akaniambia kazi yake ni mlinzi wa makaburini.
Alinihadithia mambo mengi sana kuhusu Makaburi kwa ujumla wake.

Nikamuuliza, katika kazi yake ya ulinzi wa makaburi aliwahi kupata kazi ya kulinda Makaburi ya mashujaa wa taifa au labda makaburi ya watakatifu.

Yule mlinzi akaniambia sijui anijibu kwa namna ipi. Lakini kwa vile ninataka kujua basi kabla sijasoma kitabu cha Dunia ya Wafu, na kabla hajanijibu basi niende kwenye makaburi ya watakatifu yaliyopo makumbusho ya taifa.

Wapi huko? Nikamuuliza na akanielekeza. Lakini alinipa onyo na ilani. Akaniambia niende usiku. Naam usiku ndiko roho na miili ya wafu huamka. Macho yao huona. Na sauti zao husikika.

Na vipi mchana, akaniambia nisichelewe. Maswali mengine tukionana siku nyingine. Akaniachia namba zake za simu.
Kisha tukaagana.

Basi ndio maana Mimi Mtibeli, TaikonMaster nikasema leo nitawatembelea Wafu, waliolala, hao ambao waliitwa watakatifu.

Usiku nikafika hapo, hapo nilipoelekezwa. Makaburi ya watakatifu. Usiku ukiwa mwingi. Giza na upepo vikinipapasa mwili wangu. Hisia za wafu zikaja bila kuitwa. Nikaziona bila macho. Nikasikia bila maskio. Hivyo ndivyo ilivyokuwa,.
******

Lakini yale makaburi yalikuwa kama silaha za kivita. Yalilala kama vifaru vya shetani. Heee! Ndio kama majini hivi.

Yapo makaburi yaliyokuwa yamechoka, yapo yaliyokuwa yamejengwa kwa ufahari na fedha, yapo yaliyopotea kama yaliyosahaulika.
Yapo ambayo majina yake yalisomeka kama yaliyoandikwa jana kwa wino wa risasi.

Yapo ambayo yalifutika.
Ghafla bin Vuu nikaona juu ya kaburi moja kiumbe mfano wa nguchiro sio nguchiro. Nikamtambua, alikuwa Kicheche.
Nikaona akila mzoga. Sikujua ni mzoga wa maiti ya mtu na sikutaka kujua. Nikaamua kuondoka.

Lakini

Nilikuwa tayari nimegeuka kuondoka.
Miguu yangu ilikuwa imeanza kuiacha ile sehemu ya wafu na mawe kama nyumba zao. Nilikuwa nimebeba maswali mengi kuliko majibu. Lakini nilihisi nimejifunza nilichokuja kujifunza.
Ndipo ikatokea sauti.
"Simama..."

Sauti nyepesi. Sauti ya mbali kama hatua ishirini hivi.
Lakini sauti hiyo ilikuwa ya wazi kiasi cha kunifanya nigande. Nikabaki nimesimama.

Mapigo ya moyo yakaanza kubadilika. Sikujua kama ni hofu au mshangao. Nikageuka taratibu nyuma. Hakukuwa na mtu. WalaHakukuwa na kivuli.
wala Hakukuwa na mwanga.
Ilikuwa ni mimi, makaburi na giza la wafu.

Nikatikisa kichwa. Nikajisemea labda ni mawazo yangu. Au Labda ni upepo. Au Labda ni uchovu.

Nikaanza kutembea tena.
"Usiondoke bado..."
Sauti ileIle ikarudi.
lakini Safari hii ilikuwa karibu zaidi.

Mwili wangu wote ukasisimka. Roho yangu yote. Vyote nilivyonavyo.
Hofu na kutokuamini vikanipiga kwa wakati mmoja.

Iweje wafu waseme?
Iweje waliokufa waongee?
Iweje sauti itoke mahali ambapo kimya kimeishi kwa miaka mingi kuliko uhai wenyewe?
Basi nikageuka kutazama mahali ilipotokea ile sauti.
Mbele kidogo kulikuwa na kaburi moja.

Lilikuwa limejengwa kwa marumaru nyeupe zilizong'aa hata katika giza. Lakini katikati yake kulikuwa na udongo mweusi kana kwamba kuna mtu aliuchimbua jana na kuurudisha tena kwa haraka.
Nikalisogelea kwa tahadhari.
Hatua moja.
Kisha nyingine.
Kisha nyingine tena. Sasa mtibeli nilijiona katika Filamu za ajabu, filamu za kutisha au pengine niite ndoto za majinamizi.

Lakini hakukuwa na sauti.
Hakuna. Ile sauti iliyoniongelesha haikuwepo kama haikuwahi kuwepo. Dadeki!
Kilichokuwepo ni milio ya wadudu wa usiku. Walikuwa wakilia kwa namna ya ajabu.
Kama ala za muziki wa kuzimu.
Milio yao ilipanda na kushuka.

Wakati mwingine ilisikika kama nyimbo. Nyimbo? Ndio nyimbo ambazo hazikuzoeleka nyakati za mchana mbele ya halaiki.

Wakati mwingine Zililia kama maombolezo. Naam maombolezo au kilio cha watoto wachanga walioachwa na Mama zao.

Wakati mwingine Zililia kama kicheko cha mtu aliyepoteza akili. Hahaha! Kicheko cha Mwendawazimu.

Nikahisi baridi ikipanda mgongoni. Kisha ile baridi ikashuka nakushuka mpaka magotini miguuni. Nguvu zangu zikapungua.

Nikatazama lile kaburi kwa makini zaidi. Kulikuwa na maandishi.
Lakini muda ulikuwa umeyala. Sehemu kubwa ilikuwa imefutika.
Kilichobaki ni maneno machache tu.
"...aliyesifiwa na wengi..."
"...aliyependwa na watu..."
"...aliyekuwa mtakatifu..."
Kisha maandishi yakakatika. Au niseme yalifutika. Yalifutwa na upepo na mvua za pale makaburini.

Nikakaa kimya. Macho yangu yakawa yameganda kwenye lile neno. Yanatazama.

Mtakatifu.

Neno ambalo wanadamu hulitamka kwa urahisi sana.
Neno ambalo mara nyingi hulivaa watu kama vazi.
Lakini mara chache sana hulielewa.
Ndipo sauti ile ikarudi tena.
Safari hii haikutoka hewani.
Wala Haikutoka ardhini.

Tena Haikutoka ndani ya kaburi.
Ilikuwa kana kwamba imetokea ndani ya fikra zangu mwenyewe.
"Kwa nini mnatujia?"
Nikameza mate.
Sikujibu.
"Kwa nini mnakuja kutafuta watakatifu makaburini?"

Usiku ule ulionekana kusimama.
Hata upepo ulionekana kusita kuvuma. Nikahisi swali lile likinifuata. Mimi tuu? Hapana Si mimi tu. Bali wanadamu wote.

Kwa nini tunakuja makaburini?
Kwa nini tunatafuta waliokufa?
Kwa nini tunashika mawe yao?
Kwa nini tunapiga picha makaburi yao?
Kwa nini tunachukua udongo wao?
Je, ni kwa sababu tunawapenda?
Au ni kwa sababu tumeshindwa kuiga maisha yao?

Nikainama kidogo.
Nikachukua udongo kwenye kiganja changu kutoka katikati ya lile kaburi.
Udongo ulikuwa wa kawaida tu.
Hakukuwa na tofauti kati yake na udongo wa sehemu nyingine yoyote duniani.

Ndipo nikatambua jambo.
Mwili wa mtakatifu na mwili wa mwizi, mwisho wake hugeuka udongo uleule.
Mwili wa mfalme na mwili wa maskini, mwisho wake hugeuka udongo uleule.
Tofauti haikuwa ndani ya kaburi na kaburi.
Tofauti ilikuwa ndani ya maisha waliyoishi kabla ya kulifikia kaburi.
Nilipoinua macho yangu tena, nilihisi kana kwamba lile kaburi halikuwa linanizungumza mimi.
Lilikuwa linazungumza na kizazi kizima. Jamii nzima. Waliohai.

Kizazi kinachopenda matukio kuliko kuweka legacy.
Kizazi kinachopenda mashujaa na watakatifu kuliko kufuata njia za kishujaa na kitakatifu.
Kizazi kinachopenda kutembelea makaburi ya watakatifu kuliko kuishi maisha yanayoweza kuacha urithi wa utakatifu.

Mlio wa wale wadudu ukaongezeka maradufu lakini kwa mpangilio kama kwaya za akapella za wa sabato.

Nikajikuta nikipoteza fahamu. Kisha giza likayakumba macho yangu.

Kisha kukawa giza na kimya.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa.

Niite TaikonMaster. Mwanafasihi wa miondoko ya kidijitali.

Kwa sasa Dar es da
 
Back
Top Bottom