Nilivyonusurika Kifo baada ya Mzee kunitimua nyumbani - 2.
Kwakuwa mzee alikuwa amesema nisionekane pale nyumbani na nisije kumtambua kama baba yangu,kulipokucha asubuhi alirudia hayo maneno mbele ya mama na akamwambia endapo akirudi akinikuta,basi mimi na mama tutaondoka wote!,kibaya zaidi hakutaka kabisa nikanyage kwa ndugu zake wa hapo Tarime,yaani baba zangu wadogo na mashangazi.Hakukuwa na namna ilibidi nifungashe virago vyangu na kuondoka!.
Mama "Sasa utaenda wapi baba"
Mimi "Nitajua huko huko mbele ya safari"
Kiukweli nilichafukwa sana wakati huo na nilimuona mzee wangu ni mkatili sana kuniadhibu mbele ya dogo!.Nilifahamu kabisa ya kwamba nilitenda kosa na kama ni adhabu nilikuwa tayari nishapewa lakini suala la mzee kunitimua nyumbani niliona kabisa alipofika ilikuwa ni hatua mbaya sana.
Mzee wangu alikuwa mfanyabiashara wa nyumba za kupanga pamoja na nyumba za kulala wageni(Guest houses)za kutosha pale Tarime mjini,ingawaje leo amebaki kukodoa macho tu kama kabanwa na mlango asijue la kufanya baada ya kujiingiza kwenye siasa na kujikuta ana madeni ya kufa mtu na kuanza kuuza moja baada ya nyingine!.Kibaya zaidi siasa zenyewe bora angekuwa chama tawala wangemlinda,yeye aliamua kuwa upande wa pili!.
Mama "Uende kwa mama yako mkubwa"
Aliendelea "Hebu shika hii"
Basi mama akanipatia shilingi elfu 5 ya kitanzania na kunitaka niifanye kama nauli ya kunitoa hapo Tarime mjini kuelekea kijiji cha Gamasara alipokuwa akikaa mama yangu mkubwa!.Niliipokea ile hela nikaikunja na kuitumbukiza kwenye mfuko wa suruali!.Kwakuwa nilikuwa sina pa kwenda,ilibidi niondoke tu hivyo hivyo kishingo upande kuelekea kwa mama yangu mkubwa!.
Baada ya kufika stendi nilikamata hiace iliyokuwa ikipakia abiria wa Musoma na nikampa konda shilingi 1500 nikamwambia nashukia kijiji cha Gamasara.Mama aliniambia nikifika kwa dada yake nisiwaambie kilichotokea,aliniambia endapo mama yangu mkubwa akiniuliza basi nimwambie tu nilienda kuwasalimu kwa muda wakati huo yeye huku nyumbani akiendelea kumshawishi mzee ili nirudi kuishi nyumbani na ikiwezekana anipatie pesa ya mtaji niweze kufanya biashara!.
Basi ile Hiace baada ya kujaza abiria kadhaa ikawa kama inaondoka huku konda akiendelea kuita abiria,sasa ilipokuwa ikifika umbali kadhaa inageuka tena inarudi stendi taratibu huku konda akiendelea kupiga kelele akiita abiria!.Kile kitendo kilikuwa kinawachukiza abiria wengi kwasababu ilionekana kama usumbufu na upotevu wa Muda.Yaani ilikuwa inatoka na kutembea hata umbali wa Km 1 halafu inageuka tena,sasa kile kitendo kilifanyika mpaka abiria walipolijaza lile gari.Abiria wengi walichukia lakini hakukuwa na lakunya!.
Baada ya mwendo mrefu kidogo,hatimaye ile gari ikasimama pale senta kando ya barabara ya kijiji cha Gamasara na mwanaume nikashuka!.Sikutaka kushangaa na kupoteza muda,nikaondoka mdogo mdogo kuelekea kwa mama yangu mkubwa!.
Ma'mkubwa "Eeenh mwanangu umekuwa mkubwa!"
Mama mkubwa baada ya kuniona alifurahi sana,alichukua begi langu akawa ameliingiza ndani!.Mama yangu mkubwa kwa wakati huo alikuwa na mabinti wawili na kijana wake mmoja ambao alikuwa akiishi nao hapo,mabinti zake wawili wakubwa walikuwa na miji yao tayari,mmoja alikuwa ameolewa Mwanza na mwingine alikuwa hapo hapo Tarime mjini.
Basi baada ya kukaa kwenye kiti nililetewa Togwa na viazi nikaanza kupooza njaa!.Kiukweli ulikuwa ukiniangalia ni lazima ungejua kulikuwa kuna shida,nilijikaza na kutabasamu kishingo upande lakini moyo wangu ulikuwa ukiniuma sana!.
Ma'mkubwa "Mama yako mzima mwanangu"
Mimi "Yeye mzima,anawasalimia tu"
Ma'mkubwa "Hata hivyo ni siku nyingi sijaenda"
Aliendelea "Ulishamaliza shule?"
Mimi "Nilimaliza mbona muda tu mama,ila matokeo hayakuwa mazuri"
Ma'mkubwa "Kwahiyo utaenda chuo?"
Mimi "Hapana mama labda nirudie shule"
Ma'mkubwa "Bora umwambie baba yako akupe hela ufanye biashara ya kukodisha punda"
Mimi "Kukodisha punda tena!"
Ma'mkubwa "Eeeh mbona mwenzio Matiko amefanya na tayari amenunua gari yake"
Mimi "Matiko?,Matiko yupi?"
Ma'mkubwa "Ina maana humfahamu Matiko wa mjomba wako Wegesa?"
Mimi "Mimi watoto wa mjomba Wegesa ninao wafahamu ni wawili tu,huyo Matiko sijawahi kumuona"
Ma'mkubwa "Eeee ni kweli mwanangu,hata hivyo nyie mlikuwa bado wadogo"
Sasa mama yangu huyu alikuwa ni mtu qa stori nyingi mno,yaani atakupigisha stori za watu ndani ya ukoo ambao hata wengine sikuwahi kuwaona waka kuwafahamu,sasa kwenye maelezo yake alitaka mzee anipatie hela ninunue punda niwe nawakodisha kwa watu kwa ajili ya kubeba mizigo,aliniambia ile biashara ilikuwa ikilipa sana kwa wakati huo!.Sikutaka kumkatisha maongezi yake ikaonekana nina dharau,hiyo biashara ya punda kiukweli haikuniingia akili kabisa!,kwakuwa alikuwa ni mama niliamua kumsikiliza tu!.Mpaka wakati huo hakufahamu kabisa ya kwamba kule nyumbani nilikuwa nimetimuliwa na baba yangu!.
Maisha ya pale kijijini Gamasara yalichukua nafasi na nilianza kuyazoea ingawaje hayakuwa maisha bora kama ilivyokuwa kwa nyumbani kwetu!.Mama yangu huyo mkubwa alikuwa na vimbuzi na vikondoo kadhaa ambavyo kila siku niliamka kuwasaidia kuchunga,yule dogo ambaye ni mtoto wa mama yangu mkubwa yeye alikuwa bado akisoma,sasa mara moja moja wikiendi ndiyo tulikuwa tukichunga nae!.Niliendelea kuwajibika pale nyumbani ili nionekane mtoto mwema!
Sasa kuna siku nikiwa nawatoa wale mbuzi na kondoo hapo nyumbani ili niwavushe barabara ya lami niwaingize upande wa pili kwa ajili ya malisho,kuna Hiace ilikuwa imesimama ikimshusha mtu na mzigo wake hapo kando ya barabara,sasa nikaona konda akishuka kwa haraka akaelekea nyuma ya ile gari ambako ile buti ya gari ilikuwa imefungwa kwa kukazwa na kamba,sasa wakati jamaa anafungua na kushusha ule mzigo ndipo nikammaki vizuri alikuwa jamaa yangu mmoja ambaye tulikuwa tukiishi nae kule mtaani Rebu!.
Mimi "Mtatiro mambo vipi mwanangu"
Mtatiro "Ahaa mwanangu Umughaka,mambo vipi wewe!"
Mimi "Poa mwanangu za siku"
Mtatiro "Na huku unafanya nini?"
Mimi "Nipo kwa maza mkubwa nimekuja kuwasalimia"
Mtatiro "Nina haraka,naingia MS(Musoma) mara moja,ila nageuka"
Mimi "Haina noma mwanangu"
Basi kwakuwa jamaa alikuwa na haraka,alifunga ile buti na kuikaza tena kwa kamba na kuondoka!.Yule jamaa ni mtu fulani ambae alikuwaga hachagui kazi kabisa,kuna muda unamkuta anaosha magari!,kuna muda unaweza kumkuta anapiga debe!.Sasa nilitamani kuongea nae sana lakini sikuweza kwakuwa alikuwa na haraka sana!.
Basi kuna siku pia ile jioni nikiwa pale senta na yule dogo wa mama yangu mkubwa ile gari aliyokuwa akifanyia kazi mtatiro ilipita ikiwa inatokeo Musoma na jamaa akawa ameniona na kunipungua mkono huku akianiambia kwa nguvu tungeonana kesho,Sasa kwakuwa nilielewa ilikuwa ni lazima ile Hiace ipite pale barabarani mida ya asubuhi kuelekea Musoma na kugeuka mida ya jioni,nilianza kuwa muhudhuriaji mzuri pale barabarani kila inapofika jioni ili nionane na Mtatiro niweze kumuomba na mimi aniunganishie kazi kama yake niweze kupata angalau tupesa twa kuzugia mtaani!.Nilikuwa nimeamua kabisa nitafanya kazi yoyote ili nijipatie kipato halali!.
Sasa kuna siku jamaa alipita hiyo mida ya asubuhi akawa amenifanyia ishara ya kidole kwamba anageuza muda si mrefu,sikutaka kabisa kucheza mbali,dogo alipotoka shule alikuwa na kawaida ya kunifata mahali nilipokuwa nikiwaangalia wale mbuzi ili tuweze kupiga stori za hapa na pale,sasa alipokuja hiyo mida ya saa 10 alasiri nilimwambia awaangalie wale mbuzi mara moja!.Nilitoka nikaelekea kule barabarani maana nilielewa kabisa ile gari ilikuwa ikipita mida ya saa 11 kuelekea saa 12 kurudi Tarime,basi mida hiyo nikawa yale maeneo.
Kweli!,mida hiyo ile gari nikawa naiona inakuja na iliponipita kwa mbele ikasimama na ilikuwa ikichukua abiria!.
Mtatiro "Twenzetu mwanangu tutageuka kesho"
Basi sikutaka kabisa kupoteza muda nikaikimbilia nikazama ndani!.Hakukuwa na Abiria wengi na viti vilikuwa tupu!.
Mtatiro "Mwanangu sikuhizi sikuoni kabisa mtaani,kumbe umezamia Gamasara"
Mimi "Nilikuja kumuona Maza mkubwa"
Mtatiro "Mwanangu mshauri mzee wako anunue chuma akukabidhi,siunaona watu wanavyopiga pesa"
Aliendelea "Sema dingi yako ni bahili mno,yule mkurya sijui wa wapi!,aloo!"
Jamaa alikuwa akiongea maneno mengine ambayo niliona kabisa yako serious ingawaje yalikuwa na utani ndani yake,alikuwa akinimbia nimwambie mzee wangu anunue Hiace iingiie barabarani ipige kazi!.Wakati huo hakufahamu kabisa mzee wangu alikuwa amenitimua nyumbani!.
Basi tulipofika Tarime mjini,ile gari ilipelekwa Car wash kuoshwa,na yeye Mtatiro ndiye aliyekuwa akiendesha baada ya dereva kumuachia!.Sasa sikutaka kumficha kitu ikabidi nimueleze kila kitu Mtatiro ambacho kilikuwa kinaendelea kati yangu na mzee wangu!.
Mtatiro "Sema mwanangu dingi yako ni mkuda mno!"
Aliendelea "Ila hapa mjini mbona wajanja wengi,wewe ngoja kesho mimi nitakuunga kwa mwanangu mmoja uwe unapiga deiwaka angalau upate hela zako"
Sehemu ya tatu soma
Nilivyonusurika Kifo baada ya Mzee kunitimua Nyumbani