Nilivyonusurika Kifo baada ya Mzee kunitimua nyumbani - 21.
Gari ilitembea tukaikamata njia ya Sirari,sasa tukawa kama tunaelekea Musoma.Yule jamaa akamwambia yule demu aliyekua akiendesha gari ya kwamba inapaswa tuweke kituo kwanza Lamadi tukapate msosi kisha ndiyo tuondoke.
Baada ya kufika lamadi na kupata Msosi tuliondoka kuelekea Bariadi,sikuwahi kufika bariadi ni hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika huko,sasa baada ya kuiacha bariadi tulianza kuingia vijijini huko ndani ndani ambako sikuvifahamu kwa haraka maana sikuwa mwenyeji huko.
Kituo chetu cha mwisho kilikuwa kwenye kijiji cha Mwanaungu ambako baada ya kushushwa hapo,yule jamaa alimwambia yule demu kwamba amsubiri kwanza atupeleke halafu waondoke!.
Mtatiro "Mwanangu kwahiyo mnatuacha?"
Jamaa "Tutarudi kuwachukua ondoa shaka!"
Tulitembea kwa umbali mrefu kidogo hatimaye tukafika kwenye mji mmoja ambao ulikuwa umezungushiwa minyaa ya kutosha,baada ya kufika hapo tulikuta kuna vijumba vingi vya nyasi huku kukiwa na watu ambao wengine walikuwa wamelala kwenye majamvi huku wengine wakiendelea na shughuli zao!.Kuna mwanamke akaja kutupokea kwa salamu ya kisukuma huku akipiga magoti,sasa mimi kwakuwa nilikaa usukumani kwa kipindi fulani wakati baba yangu mdogo akiwa headmaster,ile salamu haikunipa taabu kabisa!,na siyo salamu tu,naweza kukizungumza kisukuma ingawaje cha kuombea maji!.
Baada ya ile salamu yule mwanamke alituletea viti ambavyo havikuwa na watu kwa wakati huo.Basi baada ya muda mfupi yule mwanamke akaja na daftari akatutaka kila mmoja wetu kutaja jina lake na kuandikwa,sasa tulipoandikwa akatuchania vikaratasi vikiwa na namba,mimi nilipewa namba 16 na Mtatiro akapewa namba 17,yule jamaa yeye akamwambia yule mwanamke kwamba anahitaji kuonana na Mwami(Ng'wana Mwami).Yule mwanamke akamtaka asubiri kwanza.
Baada ya muda yule mwanamke akaja akamuita yule jamaa akampeleka mpaka kwenye kinyumba cha nyasi kilichokuwa kikubwa kati ya vile vinyumba tulivyovikuta pale.Baada ya muda yule jamaa akatoka akaja akatuambia angerudi baada ya siku mbili,hatukujua alipoingia mle ndani alienda kuzungumza kitu gani na huyo aliyekuwa humo ndani!.Jamaa aliondoka akatuacha pale,hiyo ilikuwa mida ya mchana saa 7.
Ilipofika mida ya saa 10,kuna mwanamke alitoka kwenye kile kijumba huku akijinyoosha kana kwamba alikuwa amechoka sana!.Alianza kuwazungukiwa watu kadhaa waliokuwa pale nje huku akiongea nao kisukuma na kiswahili!.Alipofika kwetu alitusalimia kisukuma na kama kawaida nami nilimuitikia kisukuma,sasa Mtatiro halikuwa haelewi kabisa hata salamu ndipo nilimwambia yule mama ya kwamba mwenzangu haelewi kisukuma,aliamua kumsalimu kiswahili kisha akaendelea na watu wengine!.Yule mama ndiye aliyekuwa mwenyeji wetu na alikuwa mganga!.
Mtatiro "Mwanangu kisukuma kumbe unakipiga fresh"
Mimi "Nimekaa nao,dingi yangu mdogo alikuwa headmaster shule moja huko Tabora hivyo nilikinyaka kiasi fulani"
Ilipofika mida ya saa 12 jioni kuna watu takribani 7 ambao walikuwa wanaume 3 na wanawake 4 waliingia pale nyumbani huku wakiwa wamebeba majembe,mimi nilidhani ni ndugu tu wanaoishi hapo kumbe walikuwa wateja wa huyo mama.Sasa utaratibu ulikuwa ni kwamba,unapofika kwa huyo mama unapewa namba kama sisi tulivyopewa,wakati ukiendelea kusubiri ili namba yako iitwe ilipaswa kila kunapokucha ukamate jembe umfuate mwenyeji akakuelekeze shamba la kulima na ulikuwa unapewa kipande chako ili upambane nacho,na kipande chenyewe hakikuwa cha kitoto,yaani kama ukimaliza kile kipande ndipo unaambiwa sasa umekolifai kupatiwa matibabu na yule mama.Sasa wakati unasubiri matibabu ndipo mnaitwa kwa namba ambazo hata sisi tulipewa.(Yule mganga alikuwa mjanja sana,badala ya kulima mashamba yake,sisi wapumbavu ambao tulifahamika kama wateja wake ndio tuliomlimia wakati yeye akiwa ametulia nyumbani,Daaah![emoji23][emoji23],na kila mtu aliyefika hapo kwake ni lazima ilikuwa akamatishwe jembe aingie shambani![emoji23][emoji23]).
Mimi na Matatiro tulikomaa na vipande vyetu ambavyo tulivianza siku iliyofuata kwasababu siku tuliyofika tulikuwa tumechelewa,bahati nzuri ilikuwa ni palizi na hakukuwa na nyasi sana!.Siku hiyo tulipomaliza kupalilia lile shamba ilikuwa mida ya saa 9 alasiri,tuliporudi hapo nyumbani kiukweli tulikuwa tumechafuka miguu na kunuka majasho hatari,sasa nilimfuata yule mama aliyetupokea siku ile nikawa nimemwambia atupatie maji ili tuoge,alituambia inapaswa tuwasubiri wenzetu ambao nao walikuwa hawajamaliza sehemu zao ili tupate chakula kwa pamoja kisha ndio tuoge!.
Wale walipotoka huko shambani,tulitengewa ugali wa udaga kwa na furu wa kuchemsha.Sasa tulipaswa kukaa watu watatu watatu kwa ajili ya chakula,mimi nilikaa na Mtatiro kama kawaida pamoja na jamaa mmoja ambaye alikuwa mteja kama sisi!.Siku hiyo ikapita kapa bila kuitwa namba lakini kuna watu wao waliitwa wakaendelea kupewa huduma kama kawaida!.
Siku iliyofuata tukaitwa majina watu kama wanne,sasa kwakuwa mimi na Mtatiro tulikuwa na shida moja ilibidi tuambiwe tusubiri kwanza amalizane na wale wa wawili.Zamu yetu ilifika na tukaitwa ndani kwa yule mama,hatukujieleza hata kidogo bali tulipoingia ndani alitutaka tuvue shati ili kitendo cha kupigwa chale kuchukue nafasi!.
Yule mama alitupiga chale kwa kutumia kisu kilichokuwa kikali kama wembe,alituchanja kila sehemu aliyoona yeye inafaa,baada ya hapo alituchanja pia kwenye ulimi kila mtu!.Alipomaliza kutuchanja na kutupaka dawa,alichukua kitu kilichokuwa kimefungwa na kukazwa sana na kutakiwa kila mmoja akivae kiunoni,ile alituambia ni irizi na asije akatokea mtu akaivua,alisema endapo ikitokea ukaivua basi usije ukamlaumu!.
Mpaka wakati huo hatukufahamu kwa huyo mganga tulipelekwa kufanya nini,ingawa tuliambiwa tunakwenda kutengenezwa ili hatukujua utengenezwaji ulikuwa na faida gani katika ile kazi yetu mpya ambayo tungeianza siku chache zilizokuwa mbele yetu!.
Yule mama alituambia ya kwamba,ile irizi haikupaswa kabisa kutolewa kiunoni hata iweje. Basi baada ya kumaliza ile shughuli tulitoka nje tukaendelea kumsubiri jamaa aliyetuambia angekuja kutuchukua!.Ile siku jamaa hakutokea kabisa,hivyo ikatubidi tulale tena kwa yule mama.
Yale mazingira yalikuwa ya hovyo sana lakini ilibidi tukubaliane na hali kwasababu tuliitamani pesa!.Ilipofika mida ya saa 5 asubuhi ya siku iliyofuata yule jamaa alirudi kutuchukua na kisha tukaondoka,sasa tulipoingia kwenye ile Noah tulikuta kuna mabegi kadhaa na kulikuwa na jamaa mmoja akiwa amekaa siti za abiria,dereva alikuwa ni yuleyule demu ambaye alikuwaga azungumzi na mtu!.
Jamaa "Wanangu safari ni moja kwa moja Arusha"
Mtatiro "Kaka mngeturudisha kwanza tukachukue nguo"
Jamaa "Nguo sio sehemu ya kuwazia,utazikuta huko"
Hatukuwa na swali,tuliamua kukausha na safari kuanza.Tulitembea sana na hatimaye tukaikamata lami kuelekea Musoma,baada ya kuivuka lamadi kwa mbele,tukaikamata geti la Ndabaka linaloingia Serengeti.