Sehemu ya Kumi na Saba:
Kweli nilipambana kadiri nilivyoweza, nilipiga kelele nilipoweza na nilipapatuka kama samaki nje ya maji, bado sikuweza kufurukuta kwenye mikono ya bwana yule.
Niliona kifo hiki hapa, kinabisha hodi mlangoni mwangu na sina namna ya kukabiliana nacho, sasa naacha kinitwae niende nikakutane na baba yangu mzazi.
Nikiwa nimeshakubali, sina nguvu tena ya kupambana na pumzi inaniishia kifuani mwangu, mara nilisikia mtu akisema jambo, sijui alisema nini, sikumbuki kwakweli lakini punde nilistaajabu mikono ilonikaba kwanguvu imeniacha ghafla, pumzi ndefu imeingia kwenye mapafu yangu, nikakohoa kikohozi cha uzima!
Sikuamini kama nimebaki salama na hai, niliona kama miujiza ya kutembea juu ya maji.
Sijawahi kukikaribia kifo namna ile.
Niliangaza nikamwona Amiri akiwa anamtuliza bwana Mgaya, anamwambia acha acha utaua alafu ujisababishie kesi kubwa, tafadhali acha mwana wa kwetu.
Mgaya alikuwa amefura, hakutaka kuelewa, alipambana na hasira zake lakini Amiri aliweza kummudu, akatulia akisema anamtaka mwanae la sivyo atasababisha tafafani kubwa asipatikane wa kuja kumzuia, si polisi wala majeshi.
Alimgeukia Amiri akaanza kumfokea kwanini ameingia chumbani mwake pasipo ruhusa, hana adabu, anawezaje kufanya hivyo wakati anajua kabisa mule ndani anaishi mtu na mwenzi wake?
Amiri alijitahidi kujitetea ya kwamba alinisikia ninatapatapa na ndipo akaona aje kutoa msaada haraka iwezekanavyo, lakini pia hakusita kuomba msamaha kwa jambo hilo akiahidi hatorudia tena.
Lakini nini maana kwa mtu mwenye ghadhabu? Mgaya hakumwelewa, alimfukuza kama mbwa atoke chumbani mwake mbali na upeo wa macho yake tena kabla hajamfinyanga kama udongo.
Amiri akawa hana la kufanya, akanitazama kisha akashika njia aende zake, kufika mlangoni alisimama alafu akamtazama bwana Mgaya na kumwambia mtoto yuko nje, alikuwa pamoja naye tokea asubuhi alipokuwa anakamua ng'ombe, alipomaliza akaenda zake asingoje neno lingine.
Hapo ndo' bwana Mgaya akawa hana tena neno, haya imevamia uso wake, alitazama chini kwa aibu, sasa alishajua mtoto yupo alinikabia kiasi kile cha nini?
Mimi nilitoka nikaenda kuonana na mtoto maana enyewe sikuwa naamini kama mtoto angalikuwapo, kule nje kweli nikamwona, ana afya tele, anatabasamu kuniona na akaja kunisalimu.
Nilimkagua kila upande wa mwili wake, alikuwa yu sawa sawia, hana hata kovu wala jeraha bichi, nikamkumbatia na kumwambia kamwe asiwe anatoka ndani bila kuniaga maana leo nilipatwa na hofu sana, akaitikia sawa mama, lakini ile 'sawa' ya mtoto mdogo, sidhani kama kweli alikuwa anamaanisha anachokiongea ila mimi sikujali sana, cha muhimu alikuwa mzima wa afya.
Baadae kidogo, haikupita masaa mengi, nikiwa hapo nyumbani nashika hili na lile, Amiri alinifuata akanambia kuna jambo fulani anataka kunieleza.
Alifanya hivyo baada ya kumaliza kazi zake zote za asubuhi kule mabandani.
Niliacha shughuli zangu nikamwazima sikio, akanambia hana lingine la kusema ila tu anataka kuondoka zake kurudi nyumbani, muda alokaa hapo unatosha sasa, acha aende akashikane na mengine ya maisha.
Habari hiyo ikanishtua, sikutegemea kuisikia kitu kama hicho kwa muda huo, nikamuuliza kwanini amefikia maamuzi yake hayo?
Wapi tulipomkwaza tuombe msamaha?
Hakusema kitu, alisihi anataka tu kurudi nyumbani, basi nikamwambia akae kungoja ipatikane nauli ya kwendea nyumbani, anipe kama wiki moja ama mbili pesa itakuwa imepatikana, ajabu akakataa, alisema pesa ya nauli anayo hivyo ataondoka tu, haina haja ya kumtafutia.
Aliposema hayo aliondoka zake nikabaki na maswali nini kimemkumba kijana huyo? Nilimpigia simu bwana Mgaya nikamtaarifu kuhusu habari za Amiri, nikamwambia ona majibizano yake yamemfanya kijana huyo anataka kuondoka, sasa akienda ni nani atakayetusaidia na kazi za mifugo?
Bwana Mgaya akanambia nimwache aende zake, vijana wako wengi tu wa kufanya kazi, yeye asitubabaishe kabisa, tena kama ni kuondoka aondoke mapema tu.
Nikashangazwa kweli na majibu hayo lakini ningefanya nini? Bwana Mgaya ndiye alimleta Amiri kwenye nyumba ile akimtoa huko anapopajua yeye, mimi hakuna ninalolijua, basi nikaona ninyamaze tu japo niliumizwa sana na jambo lile.
Sikutamani kabisa Amiri aondoke maana nilishamzoea na mengi ameshanisaidia, nilitamani kufanya kila ninaloweza lakini ilikuwa 'too late', pande zote mbili hazikuwa na haja ya maridhiano yangu, nikakaa pembeni kutazama filamu.
Baadae nikiwa chumbani mwangu, mtoto alinifuata akanambia mama mama mbona anko Amiri anaondoka? Macho yake yalikuwa yanavuja machozi na mdomo wake umeshika umbo la kilio, kutoka kwenda kutazama sikumkuta Amiri, nilitazama huku na kule hata nikaita na kuita, Amiri hakuonekana.
Nilitaka hata nimuage, nimpe basi hata pesa kidogo ya kula njiani lakini sikufanikiwa, kijana yule aliondoka zake kama kivuli, hakuulizia barabara, kituo cha mabasi wala muda wa kusafiri!
Nikashangaa kwa muda ule atapata gari gani? Atalala wapi? Nilitegemea ataondoka asubuhi ya mapema lakini wapi! Aliondoka zake kama vile bwana Mgaya alivyosema ya kuwa aondoke muda wowote ule.
Nikajikuta namngoja bwana Mgaya kwa hamu, arudi anieleze kijana yule alikuwa amemkosea nini na kwake kuyafanya yote yale yalikuwa bure, yani mpaka anamtaka kijana huyo aende zake kama mbwa?
Baadae bwana Mgaya alipofika, nilimvaa nikamporomoshea maneno ya shutuma na lawama, nilisema kwa kila ninalolijua, nilipomaliza bwana huyo akanambia kama na mimi nataka kumfuata huyo Amiri basi nifungashe kila kilichochangu niende na njia.
Alinambia alishawahi kunisikia nikimtaja Amiri usingizini, tena si mara moja, namwita Amiri Amiri, kwahiyo kama nitam-miss basi nifanye hima kuondoka tukaotane vema.
Sikuongea naye tena baada ya hapo, kila mmoja alipambana na mambo yake pasipo kumwongelesha mwingine.
Hata chakula changu hakugusa bwana yule, alipitiliza kwenda ndani kuoga na kisha kulala.
Kesho yake bwana Mgaya alirudi nyumbani na kijana mwingine aliyeitwa Salim, sijui kijana yule alimtoa wapi, lakini kwa kumtazama tu nilimwona ni kijana goigoi asiyeweza kazi, na kweli baada ya siku kadhaa bwana Mgaya alianza kukiri mwenyewe kuwa kijana yule hafai, ni mzito na mgumu kupokea maelekezo anayopewa.
Alimleta tena kijana mwingine lakini hamna kilichobadilika, hamna aliyeweza kuvivaa viatu vya Amiri.
Kijana yule wa pili alikuwa ni mlemavu wa kusikia, ni mpaka akutazame mdomo wako ndo' akuelewe unachosema, yani ukitaka kuzungumza naye mpaka akuelewe inabidi uwe umeshiba maana zoezi ni pevu.
Kijana huyo alipata kudumu zaidi kuliko yule wa kwanza maana angalau yeye alikuwa akielezeka japo kumweleza ndo' shughuli yenyewe.
Kijana huyo alikuwa akiitwa Shija.
Siku moja, kabla Shija hajaondoka zake pale nyumbani baada ya kushindwana na bwana Mgaya, majira ya usiku mkubwa, nilikumbwa na uchungu mkali sana wa tumbo.
Siku hiyo tumbo lilinikata kweli pasi na masikhara.
Nilishindwa hata kulala, nagugumia kwa maumivu upande huu na upande ule.
Niling'ata meno kujikaza lakini maumivu hayakukoma, niliendelea kulia na kulalama mpaka bwana Mgaya akaamka kutazama kulikoni, hali ilipokuwa mbaya zaidi, alinibeba na gari yake tukaenda hospitali.
Huko nilifanyiwa vipimo nikapewa na dawa kutokana na hali nilokuwa nayo, na siku hiyo ndo' bwana Mgaya alitambua ya kwamba nina ujauzito kwani daktari alimweleza jambo hilo.
Habari hiyo ikamshangaza sana, lakini pia akafurahi sana na kunipongeza.
Nashukuru Mungu swala lile la tumbo lilikoma baada ya kupata matibabu na hivyo tulirejea nyumbani katika majira ya saa kumi ama kumi na moja hivi ya alfajiri.
Tulipofika nyumbani, tulimkuta Shija akiwa amelala chumbani kwetu, taa za kila chumba zimewashwa, milango yote imefungwa kwa funguo, ati alikuwa anaogopa kulala mwenyewe!
Tulibisha hodi mpaka vidole vikauma, tuligonga dirisha kumwita, tulipiga honi ya gari lakini hatukufua dafu, Shija hakusikia kitu na yale masikio yake.
Ni mpaka pale bwana Mgaya alipochota maji na kumwagia kupitia diriahani ndipo alikurupuka kama mwivi akatufungulia milango.
Kesho yake bwana Mgaya akakata shauri kumwambia kijana yule aende zake. Alimlipa kiwango cha pesa alofanyia kazi kisha akampatia na nauli ya kwendea, sasa tukabaki rasmi pale nyumbani bila kijana wa kazi.
Huwezi amini yote hayo yalitokea ndani ya mwezi mmoja tu tangu Amiri aende zake.
Sasa tukabaki wenyewe pasipo kuwa na kijana wa kazi, muda huo ujauzito nilokuwa nao bado unaniendesha kweli, si nyumbani wala kazini, kote huko siwezi kuyatimiza majukumu yangu vema.
Nilimshauri bwana Mgaya afanye kumrejesha Amiri nyumbani maana kwa hali nilokuwa nayo nisingekuwa na msaada wowote kule mabandani na majukumu yake ni mengi.
Shiida ikaja ataanzia wapi?
Alimfukuza kijana yule kama mbwa, hakujua wala hakujali kama alifika nyumbani au lah.
Hakujisumbua hata kumpigia simu mlezi wake na ingali alimchukua Amiri mikononi mwake, leo anaanzia wapi kumpigia tena kumtaka aje?
Ainiomba niongee na mlezi wake Amiri kwa niaba yake, nimwombee msamaha kwa yale yote yalotokea na kama Amiri yupo naye basi amwombee arudi, gharama zote za nauli atazikaimu na hata mshahara wake atauongeza maradufu.
Hima nikafanya hivyo.
Nilimtafuta bwana yule ambaye ni mlezi wa Amiri, lakini nilivyomweleza haja ya simu yangu, bwana huyo alihamaki akisema hajui Amiri alipo.
Tangu Amiri alipokuja huku Dar hakupata kurejea tena nyumbani, muda wote huo anajua kijana huyo yupo kwangu akifanya kazi.
Nilikata simu nikabakiwa na mawazo sana, sasa Amiri yuko wapi? Vipi kama amepotea katika jiji hili kubwa au amefariki huko mitaani na sisi tumekaa hatuna habari?
Nilikosa amani kabisa.
Nilimwambia bwana Mgaya habari hizo naye akatingwa na fikira na woga.
Sasa alijua madhara ya maamuzi yake ya kukurupuka, tayari alishayatibua mambo.
Alipanga aende kituo cha polisi kutoa taarifa ya kumtafuta kijana huyo ili kama ni mzima basi apatikane na kama atakuwa amefariki basi yeye apate kuwa salama na mkono wa sheria.
Kweli asubuhi yake alinipigia simu ndo' ametoka kituoni kutimiza wajibu huo.
Ajabu hiyo siku, Mgaya aliporejea kutoka kazini, katika majira ya usiku wa saa nne ama saa tano hivi, tulipata ugeni kwa kugongewa geti, kwenda kutazama alikuwa ni Amiri!
Amesimama akishikilia begi lake mkononi.
Kama ilivyokuwa siku yake ya kwanza kuja pale nyumbani ndivyo ilikuwa na siku ile, alikuwa amevaa vilevile, begi lilelile, kalishika vilevile.
Lakini yule hakuwa Amiri tulokuwa tunamfahamu hapo awali, yule alikuwa ni Amiri mpya kabisa, sio yule alotuacha akaenda zake.
Ama basi kama ndiye yule basi alikuwa amerejea pale kwaajili ya kutuadhibu tu, kutuadhibu kwa lile tulilomtenda maana mguu wake pale haukuleta neema yoyote bali kilio.
Hatukufahamu kuondoka kwa bwana yule kwetu ilikuwa ni salama na baraka, laiti tungelijua tungelibeba sadaka ya shukrani kwenda kumtolea Mungu kwa kutuepushia janga.
Kweli usilolijua ...
Tulimkaribisha Amiri nyumbani kwa bashasha zote.
Aliiweka mizigo yake ndani na baada ya kuoga tulipata kuzungumza naye kwa ufupi.
Alituambia kwa muda wote huo alikuwa amejihifadhi pahali fulani akifanya kazi sokoni, taarifa za kurudi pale nyumbani alizipata kutoka kwa mlezi wake baada ya kumpigia siku hiyo majira ya asubuhi kumsalimu.
Basi yote hayo ya nini? Alimradi Amiri alikuwa amerejea kila mtu alikuwa na furaha na alitarajia maisha yatakuwa kama hapo mwanzoni, hata mwanangu pia alifurahi kumwona Amiri, rafiki wake wa kale.
Haikupita muda mrefu tangu Amiri arejee pale nyumbani, ndoto ile niloota kipindi kile, mtoto akinikimbia nisijue anaelekea wapi kule kizani, ikanijia tena!
Muda huu bwana Mgaya hakuwapo, siku hiyo alinambia hatorejea nyumbani kwasababu zake za kikazi.
Nilikurupuka kitandani nikakimbilia kumtazama mtoto kama yupo kando yangu, mtoto nikamwona.
Yu salama salmin.
Lakini palipokucha nilistaajabu kuona pale getini, kwa upande wa nje, kuna chapa za miguu ya mtoto, chapa ambazo zilikuwa zinawiana kwa usawa kabisa na miguu ya mwanangu!
Chapa hizo zilikuwa zinaelekea upande wa magharibi mwa geti, na kadiri zilivyokuwa zinasogea zilikuwa zinazidi kuachana kwa umbali, umbali wa kuonyesha mhusika alikuwa anakimbia.
Nilizifuata chapa hizo mpaka zikaingia ndani ya pori.
Zlipozama humo sikuziona tena, sasa yalikuwa mawe miba na majani...
Nami sikutaka kuingia humo maana niliogopa, palikuwa kimya sana na si pema kupatazama.
Niliendelea na shughuli ilonipeleka nje; kwenda kuweka pesa kwenye simu yangu kwaajili ya kutuma nyumbani, nilipokamilisha zoezi hilo nilirejea nyumbani nikamkuta mtoto akiwa tayari ameamka.
Nilimsalimu na kumjulia hali, nilitamani kumuuliza kuhusu zile chapa za miguu nje lakini nikaona ujinga, sasa atanijibu nini?
Nikiwa katika fikira hizo, mwanangu akanambia, mama mama mguu unaniuma.
Nilimuuliza anaumwa wapi haswa akanambia ni kwenye nyayo, kumtazama nikakuta jeraha la kujikata katika uvungu wa unyayo wake, jeraha bichi lenye kukaukiwa na damu.
Nilipobinyabinya hapo aligugumia kwa maumivu, mama panauma! Nikamuuliza amepatia wapi jeraha hilo? Jana jioni alikuwa wapi?
***