Madai
Video inayosambazwa mitandaoni inadaiwa kuonyesha mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na Marekani dhidi ya miundombinu ya mafuta nchini Iran wakati wa mapigano ya hivi karibuni kati ya mataifa hayo mawili.
Uhalisia
Ufuatiliaji wa JamiiCheck umebaini kuwa madai hayo si ya kweli. Ingawa Marekani ilifanya
mashambulizi katika maeneo mbalimbali nchini Iran mwezi Julai 2026, video inayosambazwa hairekodi tukio hilo, bali imetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya Akili Unde (AI).
Video hiyo ina viashiria kadhaa vinavyoonyesha kuwa si halisi, ikiwemo:
Mtu anayeonekana akikimbia mwanzoni mwa video anatoweka ghafla baada ya kuanguka, hali isiyoendana na matukio halisi.
Baadhi ya watu wanaonekana wamepinda, wameunganishwa isivyo kawaida au wana maumbo yasiyo ya kawaida, jambo linaloonekana mara kwa mara katika maudhui yanayotengenezwa kwa AI.
Kofia nyeupe walizovaa baadhi ya wahusika hubadilika rangi na kuwa za njano wanapokimbia, ishara nyingine ya hitilafu za AI.
Aidha, uchambuzi uliofanywa na zana ya kugundua maudhui ya AI ya Hive Moderation ulionyesha kuwa kuna uwezekano wa asilimia 85 kwamba video hiyo imetengenezwa kwa kutumia Akili Mnemba.
Ufuatiliaji kupitia Google reverse image search pia ulibaini kuwa
video hiyo ilichapishwa kwa mara ya kwanza tarehe 31 Machi 2026 na akaunti ya Instagram inayojulikana kwa kuchapisha maudhui yanayotengenezwa kwa AI, kabla ya kudaiwa kuhusishwa na mashambulizi ya Julai 2026.
Hivyo madai kwamba video hiyo inaonyesha mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran ni ya uongo. Video hiyo imetengenezwa kwa kutumia Akili Mnemba (AI) na haihusiani na mashambulizi halisi yaliyotokea nchini Iran mwezi Julai 2026.