Nilitaka nisome comments nicheke wee alafu niende kwenye uzi mwingine. Tayari nimecheka ila nimekuonea huruma kwa sababu mzazi wangu aliwahi kupitia hali kama yako na kiukweli ilikuwa kipindi kigumu kwake.
Mimi nafanya biashara. Nimewahi kujaribu biashara 17. Biashara tatu tu ndio zimeingiza faida. Na ni biashara moja tu katika hizo tatu zimeniletea mafanikio makubwa. Katika safari hii nimegundua kitu kimoja. Unatafuta biashara kwanza ndio ufikirie pesa ya kuifanya na sio kupata pesa kwanza kisha ndio uamue biashara.
Nakushauri kaa chini wewe na mkeo na fanyeni tathmini ya nini nguvu zenu. Mna ujuzi gani ambao mnadhani utakuwa wa manufaa kwa watu wengine? Au mnajuana na nani ambae ana ujuzi unaoweza kusaidia watu wengine? Kuna kitu ambacho nyinyi wenyewe kinawasumbua na hamjapata suluhisho? Kuna kitu ambacho watu wanakusifia wewe au mke wako mnajua au mmebarikiwa?
Nasema hivi kwa sababu kuna biashara aina mbili kuu. Kuna hizi za trading ambazo zimezoeleka mfano mayai, kilimo na pia kuna biashara za huduma ambazo ni kama kuosha magari na watu kama tax consultant. Katika kufikiria nguvu zenu na ujuzi wenu fikirieni jinsi mnaweza kutumia katika huu upande wa huduma kwa kuwa mtaji unaohitajika huwa si mwingi ukilinganisha na upande wa pili ya bidhaa za kushikika. Pia faida huwa kubwa zaidi.
Kama haujui mifano ya biashara hizi za huduma, unaweza kugoogle 'service and knowledge businesses to start' kupata mifano.
Mfano mimi nilikuwa na biashara ya kufundisha wanafunzi wa A level kufaulu mitihani ya kuingia vyuo vya Marekani na Uingereza. Nilianzishaje? Baada ya kuambiwa kipindi niko shule kuwa ninajua kuelezea somo likaeleweka. Biashara ile ilikuja kuajiri hadi watu 5 kabla ya mimi kubidi kumuachia partner wangu ili nikuze biashara nyingine.
Ni ngumu sana kufanya tathmini ya undani na ukashindwa kugundua chochote katika maswali niliyokuwekea awali. Ila kama hilo la kwanza likishindikana fikiria ni nani unamjua ana jambo la kusaidia watu wengine ili pamoja muweze kuanzisha biashara.
Ni vizuri ukiamua kufanya partnership na mtu ikajulikana mapema kabisa yupi anapata lipi. Na ni vizuri ikawa mtu ambae ulishamuamini na jukumu kubwa kabla ya kuanza nae biashara. Sio jambo jema kufanya kazi na mtu ambae haujawahi kumuamini katika jukumu lingine au hauna historia yake ya jinsi alivyofanya kazi na watu wengine kabla yako. Na hapa bado nashauri kuangalia jinsi ya kufanya biashara ya huduma.
Mfano katika biashara yangu moja nina mfanyakazi ambae anapenda sana urembo. Nilipoona hili nikamuambia tuanzishe biashara ya urembo wa asili kutumia bidhaa kama aloevera na zinginezo kutatua matatizo ya ngozi. Jukumu lake ni kuandaa masomo katika mitandao ya kijamii kuvutia wateja na jukumu langu ni kutengeza mifumo itayohakikisha wateja wananunua. Mimi nimemuongezea mshahara kiasi kizuri kwa kazi yake na upande wa pili mimi nachukua mzigo wa faida au hasara katika biashara. Kila mmoja ameridhika.
Hivyo ndugu tafuteni jambo ndani yenu ambalo mnaweza kutumia kuanzisha biashara ili mtapoanzisha na kuanza kuona mafanikio, mkopo huo utumike kuikuza. Hii itaepusha kuchoma hela ya mkopo kwa kujaribu hili na lile.